MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umevishauri vituo vinavyotoa huduma kwa wanachama wake ambavyo vimetenga maeneo maalum, kuhakisha vinatoa huduma hiyo kwa wazee katika maeneo hayo ili kuwaepusha na usumbufu wakati wa kupata huduma za matibabu.
Rai hiyo imekuwa ikitolewa kwa nyakati tofauti na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Emanuel Humba wakati wa kutembelea hospitali, vituo vya afya na zahanati zilizosajiriwa na Mfuko huo kwa lengo la kujionea huduma zinazotolewa kwa wanachama wake.
"Lazima tuwaenzi wazee wetu, wamefanya kazi kubwa ya kuifikisha nchi hii hapa ilipo hivyo kama Mfuko tungependa kuona mahali wanapotibiwa wanachama wetu na wazee wetu nao wapate huduma mahali hapo...si vyema kuona wakitaabika wakati wa kupata matibabu," alisema Humba.
Aliwataka watoa huduma kuhakikisha wanatumia fursa mbalimbali zinazotolewa na NHIF kuboresha huduma za matibabu kwa kuwa na vifaa vya kisasa, dawa na kuboresha mazingira ya vituo hivyo.
"Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unatoa fursa ya mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo ambao unalenga moja kwa moja kuboresha huduma za matibabu kwa wanachama wetu na wananchi kwa ujumla hivyo ni vyema wazee wetu nao wakapewa heshima kubwa wakati wa kupata matibabu," alisema Humba.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya ameushauri Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu ya afya kwa wananchi ili kupunguza gharama za matibabu.
Amesema elimu ya afya itasaidia wanachama na wananchi kwa ujumla kuepukana na maradhi ambayo yanagharimu fedha nyingi kwa ajili ya matibabu.
"Yapo maradhi yanayotokana na mtindo wa maisha kama kisukari, shinikizo la damu ambayo yanaweza kuepukika kwa wanachama wenu kupata elimu tu ya namna ya kula, kufanya mazoezi na mambo mengine," alisema Manyanya.
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, hivi karibuni umeendesha mikutano ya wadau wake katika mikoa mbalimbali nchini, ambayo kwa pamoja wameazimia kuifanya agenda ya Bima ya Afya kuwa ya kudumu.