Mama Salma Kikwete akizindua rasmi huduma ya bima ya afya kwa vikundi vya wajasiriamali, kushoto ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii akishuhudia.
Desemba 20, 2012, Mwenyekiti wa Taaisisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Mama Salma Kikwete alizindua rasmi huduma ya bima ya afya kwa vikundi vya Wajasiriamali.
Katika uzinduzi huo, Mama Salma Kikwete aliwataka wanavikundi hao wanaotarajiwa kuanza mara moja kunufaika na huduma za bima ya afya kuitumia huduma hiyo kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Aidha aliwataka wanachama wote kwa ujumla kuwa walinzi wa huduma zitolewazo na NHIF lakini pia kutoa taarifa wanapokutana na lugha mbaya za watoa huduma wakati wa kupata huduma za matibabu.
Uzinduzi wa huduma hiyo umefungua milango kwa vikundi mbalimbali vya wajasiriamali nchini kuweza kujiunga na bima ya afya ili wawe na uhakika wa kupata matibabu wakati wowote.
Akitoa maelezo ya awali Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emanuel Humba alisema kuwa wanawake ni moja ya kundi lenye nguvu na linalobeba familia nyingi katika huduma mbalimbali hususan za afya.
Alisema kuwa mpaka sasa wanawake wachangiaji waliopo katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ni asilimia 41 ya wanachama wachangiaji wote na hii inaonesha ni jinsi gani wanawake walivyo na nchamgo mkubwa ndani ya jamii. |