Thursday, September 8, 2011

Wahandisi wataka kujitosa kumaliza tatizo la umeme


Na Grace Michael

BODI ya Usajili ya Wahandisi (ERB), imesema tatizo la umeme linaloikabili nchi kwa sasa lisingefika hapo lilipo endapo serikali ingewashirikisha wataalam hao katika hatua mbalimbali.

Kutokana na hali hiyo, wameiomba serikali kuhakikisha inatoa ushirikiano wa kutosha katika mambo mbalimbali yanayohusu fani hiyo, ili kuepukana na matatizo kama tatizo la umeme kwa sasa.

Akitoa salamu za bodi hiyo wakati wa kufunga wa mkutano uliokutanisha bodi tatu za sekta ya ujenzi, Bw. Gema Modu, alisema kuwa; “Kungekuwa na ushirikishwaji wa uhakika katika suala la umeme, suluhu ingekuwa imepatikana, hata tatizo hili lisingefikia hapo lilipo,”

Aliongeza kuwa; “Tatizo hili la umeme kwa upande wetu tunalichukulia kwa sura mbili moja ikiwa ni tatizo na nyingine ni fursa kwetu ya kuingia kufanya kazi hiyo na katika hili tumejipanga na tutaingia huko kwa lengo la kusaidia.”

Bodi nyingine zilizoshiriki mkutano huo ni pamoja na Bodi ya Wakandarasi (CRB), Bodi ya Wasanifu na Wakadiria majengo ambao kwa pamoja walijadili masuala mbalimbali ya sekta ya ujenzi na hatimaye kutoka na maamuzi ambayo yatawasilishwa serikalini kwa lengo la kuboresha sekta hiyo.

Mkutano huo ambao ulifungwa na Waziri wa Miundombinu Dkt. John Magufuli kwa niaba ya Makamu wa Rais Dkt. Mohamed Gharib Bilali, aliwataka wataalam hao kuwa wawazi katika mambo wanayotaka serikali iyafanyie kazi hata kama ni makali.

Andikeni mahitaji yenu kwa uwazi, msiwe wanasiasa katika kazi zenu...hata kama ni maneno makali andikeni na wenyeviti wa bodi waweke saini zao nami nitayapeleka kwa rais bila kuchakachua kitu chochote,” alisema Dkt. Magufuli.

Aidha aliwataka wote kwa pamoja kushirikiana katika kazi na kuachana na utamaduni wa kupigana vijembe na rushwa katika kazi na badala yake watangulize uzalendo katika shughuli zao kwa kuwa fani za ujenzi ndizo zenye mwelekeo wa maendeleo ya nchi, lakini pia ndizo zimeshikilia uchumi wa nchi.

Kwa mujibu wa hotuba ya Makamu wa Rais, serikali itazidi kuwashirikisha katika kazi za umma na kutoa upendeleo kwa wazalendo katika kazi hizo, lakini akaonya kuwa wasifanye kazi ambazo ziko chini ya kiwango.

Tunatambua kuwa kuna tatizo la mitaji na katika hili tunatoa mwito kwa mabenki kuwatazama kwa jicho la pekee wakati mnapojitokeza kuomba mikopo...suala la msingi ni kufanya kazi zenye viwango kwa kuwa serikali tunachefuliwa sana na majengo mabovu na kazi zote ambazo ziko chini ya kiwango,” alisema hotuba hiyo.

Alisema kuwa serikali inatambua madeni inayodaiwa na wataalam hao na ikaahidi kuwa sehemu kubwa ya madeni hayo italipwa hivi karibuni.



Hata hivyo washiriki wa mkutano huo wamekubaliana kupambana na tatizo la rushwa na wakashauri kuwepo mjadala wa wazi ambao utajadili suala hilo kwa uwazi na bila kuoneana aibu kwa kuwa rushwa ni ugonjwa unaoweza kuliua taifa.

No comments:

Post a Comment