Na Grace Michael, Iringa
UONGOZI wa Hospiali ya Mkoa wa Iringa, umesema wazi kuwa bila ya kuwepo kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Hospitali hiyo ingekuwa kwenye hali ngumu ya kiundeshaji.
Kutokana na hali hiyo, uongozi wa hospitali hiyo umeahidi kutoa huduma bora kwa wanachama wa mfuko na wananchi kwa ujumla ili waone matunda ya kujiunga lakini pia wananchi wengine waweze kuona umhimu wa kujiunga na utaratibu wa Bima ya Afya.
Akizungumza baada ya kupokea msaada wa mashuka yaliyotolewa na NHIF, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa Dk. Manyama, alisema kuwa msaada huo umekuja kwa wakati sahihi kutokana na uhitaji mkubwa wa mashuka unaosababishwa na idadi kubwa ya wagonjwa wanaofika hospitalini hapo.
"Tunashukuru sana wenzetu wa NHIF kwa kuliona hili, na nikiri tu kuwa bila ya uwepo wenu hata hii hospitali ingekuwa ni ngumu sana kuiendesha kwani mmekuwa mkitusaidia sana mambo mengi na fedha zenu ndizo zinatumika katika uboreshaji wa huduma za matibabu," alisema Dk. Manyama.
Alisema mahitaji ya mashuka katika hospitali hiyo ni makubwa kwa kuzingatia kwamba mashuka nane yanatakiwa kutumika kwa kila kitanda kila siku.
“Hospitali ina vitanda 365 na kwa wastani kila siku tuna wagonjwa 270 wanaolazwa huku mahitaji ya mashuka yakiwa ni nane kwa kila kitanda kwa kila siku,” alisema.
Shughuli ya kukabidhi msaada huo ilifanywa kwa nyakati tofauti jana na makamu Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Alli Kiwenge aliyekuwa ameambatana na maofisa mbalimbali wa mfuko huo.
Akiwa katika hospitali ya mkoa, Kiwenge ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (Tughe) alisema nchi inakabiliwa na changamoto kubwa ya utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wake hasa waishio vijijini.
Alisema Idara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wake wengine wa maendeleo wana wajibu wa kuwahamasisha wananchi hao wa vijijini kujiunga na Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF).
“Hii ni njia ya pekee ya kumkomboa mtanzania kwa kumpa uhakika wa kutibiwa yeye na familia yake kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii ambao upo chini ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,” alisema.
Alisema kwa kuzingatia kwamba gharama za matibabu zinapanda kila uchao na magonjwa yanaendelea kuwasibu watanzania bila kupiga hodi, mifuko hiyo ndiyo njia muafaka ya kunusuru afya zao hasa pale wanapokuwa hawana akiba ya fedha kwa ajili ya matibabu.
Alisema wanachama wa mifuko hiyo hawatakiwi kukosa matibabu au dawa na inapotokea wanakumbwa na tatizo hilo wanapaswa kutoa ripoti kwa uongozi wa NHIF ili hatua zinazohusika ikiwa ni pamoja na kufidiwa gharama za matibabu zifanyike.
Katika kituo cha Afya cha Ngome, Kiwenge aliwakumbusha wafanyakazi wa sekta ya afya kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na akasisitiza waache migomo pindi wanapotaka kudai maslahi yao.
“Fanyeni kazi, madai yenu ya mishahara na maslahi mengine tuachieni viongozi wenu, tutaendelea kuyadai kwa kukaa mezani na serikali,” alisema.
Tuesday, April 17, 2012
NHIF yatua Iringa, yatembelea hospitali na kutoa mashuka
Subscribe to:
Posts (Atom)