WANANCHI wa Kijiji cha Hoyoyo katika Kata ya Mkuranga wameitikia mwito wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wa kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) baada ya kuhamasishwa na Mfuko huo kwa kushirikiana na Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA).
Kutokana na hali hiyo, jumla ya kaya 143 zilijiunga papo kwa papo na Mfuko huo, huku baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wakitoa ushuhuda wa namna wanavyonufaika na huduma za matibabu.
Akihamasisha wananchi hao kujiunga na CHF, Ofisa anayeshughulikia Mfuko wa Afya ya Jamii, Rehani Athuman aliwaelezea umuhimu wa kupata matibabu kwa njia ya kadi kwa kuwa ugonjwa unaweza ukamapata mtu wakati wowote.
"Ndugu zangu, nadhani mnatambua kuwa gharama za matibabu kwa sasa ni kubwa ambazo ni vigumu kuzimudu lakini ukijiunga na Mfuko huu utatibiwa wewe na familia yako kwa muda wa mwaka mzima lakini hii pia inasaidia hata kupunguza rushwa vituoni," alisema Rehani.
Aliwahoji wananchi hao kama wapo wanaotibiwa na Mfuko huo ili waweze kutoa ushuhuda kwa wenzao kuhusiana na huduma za matibabu ambapo alijitokeza mkazi wa kijiji hicho Sauda Kikeleko na kueleza kuwa tangu ajiunge na Mfuko huo anatibiwa bure yeye na familia yake na hajawahi kukumbana na kikwazo chochote.
"Jamani Mfuko huo ni mzuri na mimi ni mwanachama wake, tangu nijiunge napata huduma za matibabu bila kutoa hele mfuko na wanangu wakiugua nao wanapata huduma kama kawaida hivyo ni vyema mkajiunga," alisema.
Naye Mzee Iddi Mgeni ambaye ni mkazi wa Hoyoyo, alisema kuwa kinachotakiwa ni kuanza kujiunga mara moja bila kujali changamoto zinazoikabili sekta ya afya na kwa kuonesha mfano, alitoa mchango wake wa kujiunga hali iliyotoa hamasa kwa wananchi wengine kujiunga papo kwa papo.
Mbali na kujitokeza kwa wingi kujiunga na Mfuko huo, Diwani wa kata hiyo, Bw. Salum Kuga, naye hakusita kuonesha mfano kwa wananchi wake ambapo alichangia familia sita ili nazo zinufaike na huduma kupitia CHF.
Aliuomba Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuendelea kushirikiana na wananchi wa kata hiyo ili kaya zote ziweze kujiunga na Mfuko huo na kuondokana na gharama kubwa za matibabu zinazopanda kila uchao.
Wakati huo, wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wamechangia jumla ya kaya 53 za watoto yatima ili kuwawezesha kuwa na uhakika wa matibabu.
Wafanyakazi hao walifikia hatua hiyo kwa lengo la kuzisaidia familia hizo lakini pia kuonesha mchango wao kwa jamii wanayoitili kuonesha mfano kwa jamii wanayoitumikia.
Akizungumza kwa niaba ya WAMA, Philomena Marijani aliushukuru Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa hatua ya kutoa mafunzo kwa wananchi hao kwani hatua hiyo inakamilisha lengo la WAMA la kuwaunganisha wajasiliamali na watoa huduma.