Wednesday, September 19, 2012

Dk. Mwinyi afanya ziara NHIF

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Emanuel Humba akiongozana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi na wajumbe wa Bodi kukagua miradi ya Mfuko huo.

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emanuel Humba akitoa maelezo ya moja ya miradi ya Mfuko huo kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussen Mwinyi.

Mkurugenzi wa Uwekezaji na Fedha, Deusdedit Rutazaa akitoa maelezo ya Mradi kwa Waziri na viongozi wengine wa Mfuko.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi akitoa maelekezo kwa viongozi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuhusiana na miradi iliyowekezwa Makao Makuu ya Mfuko huo.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Ally Kiwenge akitoa salaam za Bodi kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii akizungumza na wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya alipofanya ziara makao makuu ya Mfuko huo leo.

Baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (walioko mbele) wakisikiliza kwa makini maelekezo ya Waziri wakati akizungumza na wafanyakazi.

Wafanyakazi wakisikiliza kwa makini maelekezo ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii.

Wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wakimsikiliza Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii alipofika kwa lengo la kuzungumza nao.
Kuna haja ya kuwa na mdhibiti huduma za afya-Dk. Mwinyi

SERIKALI imesema kuna haja ya kuwepo kwa chombo maalum cha kudhibiti mfumko wa bei katika sekta ya afya kwa lengo la kuwawezesha wananchi wake kupata huduma hizo bila kuwepo kwa vikwazo vya gharama kubwa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi wakati akizungumza na wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) alipotembelea Makao Makuu ya Mfuko huo.

Hatua ya Dk. Mwinyi kusema hayo ilitokana na ombi la Wafanyakazi hao kupitia Mwenyekiti wa Tawi la Chama cha Wafanyakazi (TUGHE), Baraka Maduhu, ambaye alisema kati ya mambo yanayowanyima faraja wafanyakazi wa Mfuko huo ni pamoja na mfumko holela wa gharama za matibabu.

“Pamoja na mafanikio makubwa ambayo Mfuko umeyafikia lakini bado kuna vikwazo ambavyo sisi kama wafanyakazi wa Mfuko vinatunyima faraja likiwemo la upandishwaji holela wa gharama za matibabu hatua itakayowafanya Watanzania na Mfuko kwa ujumla kushindwa kumudu gharama hizo hivyo ombi hili tunalileta kwako,” alisema Mwenyekiti wa TUGHE.

Akijibu hoja mbalimbali ambazo ziliwasilishwa kwake kama kero za wafanyakazi wa Mfuko, Dk. Mwinyi alikubaliana na ombi hilo na kusema kuna haja kubwa ya kuwepo kwa chombo hicho ili kiweze kulinda walaji kwa kuwa suala la kupata huduma za matibabu kwa mwananchi ni suala nyeti linalogusa maisha ya mwananchi moja kwa moja.

Kutokana na hali hiyo, Waziri alisema kinachotakiwa kufanyika kwa sasa ni kupata maoni ya wadau mbalimbali wa sekta ya afya ili kuangalia namna ya utekelezaji wake.

Katika hatua nyingine Dk. Mwinyi aliupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuwa ni moja ya Taasisi ambayo iko chini ya Wizara yake inayofanya vizuri katika utekelezaji wa shughuli zake.

“Mkifanya vizuri tunapaswa kuwaambia na mnapokosea ni lazima tuwaonye lakini ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba uongozi na wafanyakazi kwa ujumla mnafanya vizuri hivyo ongezeni bidii ili kufikia malengo mliyoyaweka nay a Serikali kwa ujumla,” alisema.

Akizungumzia suala kuwepo kwa chombo maalum chini ya wizara kitakachodhibiti ubora wa huduma zinazotolewa na Bima za afya zikiwemo za binafsi na serikali kama zinakidhi kiwango cha ubora wa huduma ikilinganishwa na michango ya wanachama, Dk. Mwinyi alikubaliana na wazo hilo na kusema kuna haja ya suala hilo kuwa chini ya wizara ili liweze kuwa na usimamizi mzuri.

“Pamoja na suala hili kuwa chini ya Wizara ya Fedha ambayo inaangalia bima kwa ujumla wake lakini masuala ya afya ni masuala nyeti na yanayotakiwa kuangaliwa kipekee hivyo kuna haja ya kuwa na chombo kinachosimamia bima za afya,” alisema.

Akitoa maelezo ya utangulizi, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Emanuel Humba, alisema kitendo cha Waziri kutembelea na kuzungumza na wafanyakazi kinaleta faraja kwa wafanyakazi lakini pia kuongeza juhudi ya utendaji zaidi hivyo akamwomba Waziri kutochoka kufanya hivyo mara kwa mara.
  



Tuesday, September 11, 2012

NHIF YAPONGEZWA KWA HUDUMA NZURI

Keki iliyotolewa kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mjumbe wa Central Board of Education (CBE) Imran Dhalla ambaye ameridhishwa na huduma za NHIF.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Beatus Chijumba akipokea keki kutoka kwa Imran Dhalla ambaye ni Mwanachama  aliyeridhishwa na huduma za Mfuko.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Beatus Chijumba akimkabidhi keki hiyo Meneja Uanachama Binafsi,Grace Lobulu ambaye alimhudumia mwanachama huyo.

Ofisa Masoko na Elimu kwa Umma akimpa kipande cha keki mmoja wa wanachama aliyekuwepo wakati wa tukio hilo.

Meneja Masoko na Elimu Anjela Mziray na Ofisa wake Grace Michael wakiangali keki iliyoletwa na Mwanachama kwa lengo la kuushukuru Mfuko kwa huduma nzuri alizozipata.  

Kutokana na huduma nzuri zinazotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), mmoja wa wanachama wa Mfuko huo, Imran Dhalla ambaye pia ni Mjumbe wa Central Board of Education (CBE) amefika katika Ofisi za Mfuko huo na kuupongeza kwa huduma nzuri na za haraka alizozipata.

Imran ambaye alikabidhi keki kwa Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Beatus Chijumba kama ishara ya kuridhishwa na huduma alizopata, alisema ushirikiano mkubwa alioupata ndio umemsukuma kuandaa keki hiyo na kufika ofisi za Mfuko huo kwa lengo la kuushukuru.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu Beatus Chijumba akipokea keki hiyo, alitoa mwito kwa wanachama kuupatia mfuko huo mrejesho wa huduma wanazopata ili uweze kuboresha zaidi.

"Mfuko uko tayari kupokea mrejesho wa aina yoyote, uwe mzuri au unaotutaka kuboresha zaidi...tunawaomba na wanachama wengine kuiga mfano huu ambao tunaamini utatusaidia sana kuboresha huduma zetu," alisema.

Imran alisema kuwa wafanyakazi wote wa mtandao wa shule za Al Muntazir wamejiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na mchakato unaendelea wa kuhakikisha wanafunzi nao wanajiunga na Mfuko huo ili wawe na uhakika wa matibabu.