Wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wakimsikiliza Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii alipofika kwa lengo la kuzungumza nao.
Kuna haja ya kuwa na
mdhibiti huduma za afya-Dk. Mwinyi
SERIKALI imesema kuna haja ya kuwepo kwa chombo maalum cha
kudhibiti mfumko wa bei katika sekta ya afya kwa lengo la kuwawezesha wananchi
wake kupata huduma hizo bila kuwepo kwa vikwazo vya gharama kubwa.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk.
Hussein Mwinyi wakati akizungumza na wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya (NHIF) alipotembelea Makao Makuu ya Mfuko huo.
Hatua ya Dk. Mwinyi kusema hayo ilitokana na ombi la
Wafanyakazi hao kupitia Mwenyekiti wa Tawi la Chama cha Wafanyakazi (TUGHE),
Baraka Maduhu, ambaye alisema kati ya mambo yanayowanyima faraja wafanyakazi wa
Mfuko huo ni pamoja na mfumko holela wa gharama za matibabu.
“Pamoja na mafanikio makubwa ambayo Mfuko umeyafikia lakini
bado kuna vikwazo ambavyo sisi kama wafanyakazi wa Mfuko vinatunyima faraja
likiwemo la upandishwaji holela wa gharama za matibabu hatua itakayowafanya
Watanzania na Mfuko kwa ujumla kushindwa kumudu gharama hizo hivyo ombi hili
tunalileta kwako,” alisema Mwenyekiti wa TUGHE.
Akijibu hoja mbalimbali ambazo ziliwasilishwa kwake kama kero
za wafanyakazi wa Mfuko, Dk. Mwinyi alikubaliana na ombi hilo na kusema kuna
haja kubwa ya kuwepo kwa chombo hicho ili kiweze kulinda walaji kwa kuwa suala
la kupata huduma za matibabu kwa mwananchi ni suala nyeti linalogusa maisha ya
mwananchi moja kwa moja.
Kutokana na hali hiyo, Waziri alisema kinachotakiwa kufanyika
kwa sasa ni kupata maoni ya wadau mbalimbali wa sekta ya afya ili kuangalia
namna ya utekelezaji wake.
Katika hatua nyingine Dk. Mwinyi aliupongeza Mfuko wa Taifa
wa Bima ya Afya kuwa ni moja ya Taasisi ambayo iko chini ya Wizara yake
inayofanya vizuri katika utekelezaji wa shughuli zake.
“Mkifanya vizuri tunapaswa kuwaambia na mnapokosea ni lazima
tuwaonye lakini ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba uongozi na wafanyakazi
kwa ujumla mnafanya vizuri hivyo ongezeni bidii ili kufikia malengo mliyoyaweka
nay a Serikali kwa ujumla,” alisema.
Akizungumzia suala kuwepo kwa chombo maalum chini ya wizara kitakachodhibiti
ubora wa huduma zinazotolewa na Bima za afya zikiwemo za binafsi na serikali
kama zinakidhi kiwango cha ubora wa huduma ikilinganishwa na michango ya
wanachama, Dk. Mwinyi alikubaliana na wazo hilo na kusema kuna haja ya suala
hilo kuwa chini ya wizara ili liweze kuwa na usimamizi mzuri.
“Pamoja na suala hili kuwa chini ya Wizara ya Fedha ambayo
inaangalia bima kwa ujumla wake lakini masuala ya afya ni masuala nyeti na
yanayotakiwa kuangaliwa kipekee hivyo kuna haja ya kuwa na chombo kinachosimamia
bima za afya,” alisema.
Akitoa maelezo ya utangulizi, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa
Taifa wa Bima ya Afya, Emanuel Humba, alisema kitendo cha Waziri kutembelea na
kuzungumza na wafanyakazi kinaleta faraja kwa wafanyakazi lakini pia kuongeza
juhudi ya utendaji zaidi hivyo akamwomba Waziri kutochoka kufanya hivyo mara
kwa mara.
|
No comments:
Post a Comment