Tuesday, March 20, 2012

CHF italeta afya bora na kupunguza umasikini-Pinda

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameagiza Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) uwe agenda ya Kitaifa kwa kuwa ndio njia pekee ya kufikia lengo la Afya Bora kwa wote na kupunguza vifo na umasikini kwa Watanzania. 

Kutokana na umuhimu huo, ameiagiza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kukaa na Uongozi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili kuandaa mkakati utakaohakikisha Watanzania wote wanapata huduma za Mfuko huo kwa lengo la kuwawezesha kuwa na afya njema. 

Waziri Mkuu Pinda aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya NHIF tangu kuanzishwa kwake sherehe zilizofanyika Makao Makuu ya Mfuko huo. 

“Tunaweza kutumia uzoefu kutoka nchi mbalimbali ambazo zimepiga hatua katika masuala ya Bima ya Afya lakini kwa kuzingatia utamaduni na mazingira ya kitanzania, kampeni za uhamasishaji ziwe endelevu kwa viongozi wa Serikali, wawakilishi wa wananchi na viongozi wa dini…wote tushiriki katika kampeni hii tukizingatia kuwa suala hili linamhusu kila mtu,” alisema Pinda. 

Akizungumzia matumizi ya fedha za uchangiaji na uboreshaji wa Huduma, Fedha ambazo hulipwa na NHIF, alisema huelekezwa zaidi katika uboreshaji wa huduma nchini na mpaka sasa Mfuko huo umelipa zaidi ya sh. Bilioni 140 kwa vituo mbalimbali vilivyosajiliwa na Serikali, Mashirika ya Dini na binafsi.  

Hata hivyo alisema kuwa pamoja na fedha hizo kulipwa kwa lengo hilo, huduma bado si za kuridhisha hatua iliyomfanya kumwagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua matumizi ya malipo yatokanayo na uchangiaji wa huduma za afya zikiwemo za NHIF, tele kwa tele na papo kwa papo lengo ni kuhakikisha matumizi bora ya fedha za Mfuko na kutoa huduma bora zaidi. 

“Wito wangu hasa kwa watoa huduma, mjipange vizuri zaidi ili kuboresha huduma zenu, muwe waadilifu ili mpate malipo halali…msijihusishe na madai ya kughushi yatakayotishia uhai wa Mfuko wetu na msiruhusu kuharibu mahusiano yaliyo kati yenu na Mfuko, eleweni kwamba maendeleo ya Mfuko ndio mkombozi kwa wananchi wetu,” alisema Pinda. 

Pamoja na hayo, aliuopongeza uongozi wa Mfuko kwa kitendo cha kuwatambua waasisi wa Mfuko huo ambao wamesadia kuleta ufanisi na ustawi wa Mfuko hivyo akautaka kuendelea na utaratibu huo kwa kuwa unatoa hamasa kwa wengine kutoa mchango wao wa hali na mali katika kufanikisha malengo yaliyopo. 

Naye Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa katika salaam zake aliutaka Mfuko kulinda mafanikio yaliyofikiwa, kufanya kazi kwa bidii na maarifa huku wakijua kuwa bado kuna kundi kubwa la Watanzania wanaohitaji huduma hasa vijijini. 

‘Msiogope kuthubutu kufanya mambo yanayolenga  kuboresha huduma za matibabu kwa watanzania hasa katika ujenzi wa vituo vya matibabu, kusaidia vifaa tiba na elimu zaidi ili uhai wa Mfuko ubaki kuwa imara,” alisema Rais Mkapa. 

Aidha aliwataka wananchi kutodanganywa kuhusu afya zao hivyo suala la uchangiaji ni la muhimu na Bima ya Afya ndio mtindo wa sasa wa maisha.

No comments:

Post a Comment