Na Grace Michael, Mwanza
MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Mbigiro amezitaka Halmashauri mkoani humo kuzitumia fedha zinazolipwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) katika ununuzi wa dawa na si kuzielekeza katika masuala mengine kama ya kulipana posho.
Amesema kuwa fedha hizo zimekuwa zikitumika katika matumizi ambayo hayakukusudiwa jambo linalokwamisha uboreshaji wa huduma za matibabu katika vituo vya kutolea matibabu.
Agizo hilo amelitoa katika mkutano wa wadau wa Mfuko huo uliofanyika leo jijini Mwanza na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo watoa huduma, wanachama, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Wilaya na wengine.
"Wenzetu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wanatulipa fedha lakini fedha hizo ndo utazikuta zinalipwa posho huku vituo vikikosa dawa...hili halikubaliki ni lazima tuone fedha hizi zikinunua dawa na wananchi wakipata tiba na kuwa na afya njema," alisema Mbigiro.
Alisema kuwa yeye kama Mkuu wa Mkoa atajisikia faraja kuona akiongoza wananchi wenye afya njema kwa kuwa watakuwa na uhakika wa kuzalisha na kukuza pato lao na la Taifa kwa ujumla.
Alisema kuwa inashangaza Mkoa kama wa Mwanza kuwa nyuma katika suala la wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) huku ukiwa na fursa nyingi za kiuchumi na pato la mwananchi wa Mwanza likikidhi mahitaji ya kujiunga na Mfuko huo ili kuwa na uhakika wa matibabu.
"Hapa tuna fursa nyingi zikiwemo za uvuvi, ufagaji, kilimo, madini, utalii na zingine na ili hizi fursa zitumike ni lazima wananchi hawa wawe na afya njema hivyo ni lazima tuhakikishe sisi viongozi tunawahamasisha wananchi wetu kwa kuwaeleza umuhimu wa kuwa na bima ya afya...sitakubali mkoa huu kubaki na asilimia 1.1 ya kaya zilizoko kwenye Mfuko wa CHF," alisema.
Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa Uongozi wa Mkoa wa Mwanza utatoa ushirikiano kwa NHIF ili lengo la kuwafikia Watanzania asilimia 30 ifikapo 2015 lifanikiwe.
Aliongeza kuwa hata Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010 katika ibara ya 85 inasema wazi kuwa "Mandeleo ya Taifa letu yataletwa na wananchi wenye afya bora inayowezesha kuzalisha mali na kutoa huduma mbalimbali".
Mbigiro akitoa mwito kwa wanachama wa Mfuko huo, aliwataka kuwa walinzi wa huduma za Mfuko hasa wanapokutana na dawa zinazotolewa na Serikali zikiuzwa kwenye maduka binafsi.
Ili kutimiza lengo la kupanua wigo wa wanachama wa Mfuko huo, Mbigiro alizitaka Halmashauri kutunga sheria ndogo itakayowalazimu wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emanuel Humba akitoa maelezo ya Mfuko huo kwa wadau, aliwataka watoa huduma kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Mfuko huo ili kuboresha huduma za matibabu.
Aliahidi kuwa Mfuko utaendelea na juhudi za kutoa elimu kuanzia ngazi ya Taifa hadi ngazi ya kaya ili kuhakikisha lengo la afya bora kwa kila Mtanzania linafikiwa.
No comments:
Post a Comment