Na Mwandishi Wetu, Dodoma
UBORESHAJI wa huduma za
matibabu kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya hususan upatikanaji wa
dawa katika vituo vya kutolea huduma ni moja ya mambo yaliyojadiliwa mwishoni
mwa wiki katika kikao kazi kilichojumuisha wataalam kutoka Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na TAMISEMI.
Katika kikao kazi hicho
ambacho kilihudhuriwa na maofisa wa ngazi za juu katika taasisi zilizoko chini
ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na TAMISEMI wakiwemo mawaziri wa
pande zote mbili, walijadili kwa kina namna ya kupunguza ama kuondoa kabisa
tatizo la dawa ambalo wanachama na wananchi kwa ujumla wanakutana nalo wakati
wa kupata huduma za matibabu.
Kwa upande wa Mfuko wa Taifa
wa Bima ya Afya, kupitia Mkurugenzi wake Mkuu, Emanuel Humba alisema kuwa Mfuko
utaendelea na uboreshaji wa huduma za matibabu kupitia mpango wa Mfuko huo wa
mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo kwa vituo vilivyosajiliwa na Mfuko
huo lakini pia kuendelea kusajili maduka ya dawa muhimu ili wanachama wapate
huduma inayotakiwa na wananchi waone umuhimu wa kujiunga na Mfuko wa Afya wa
Jamii (CHF).
Aidha kwa upande wa Bohari ya
Dawa (MSD) ambao ndio wana jukumu la usambazaji dawa, kupitia Mkurugenzi wake
Mkuu Joseph Mgaya, alisema kuwa wanaendelea kushughulikia changamoto zilizopo kama kutokuwepo kwa maoteo sahihi ya dawa ili hatimaye
idara hiyo iweze kuondokana na malalamiko yanayoelekezwa kwake.
Wakihitimisha kikao kazi
hicho, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Waziri wa Ofisi ya Waziri
Mkuu (TAMISEMI) Hawa Ghasia, walizitaka pande zote mbili kuhakikisha
zinatekeleza maafikiano yaliyofikiwa katika kikao hicho ili kipa upande uweze
kutoa huduma nzuri kwa wananchi wa Tanzania.
Aidha walisema kuwa njia
pekee ya kuwakomboa wananchi au kuwafanya wawe na uhakika wa kupata matibabu ni
kuwahamasisha kujiunga na Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF) hivyo wakaitaka NHIF
kuhakikisha inaongeza kasi ya uelimishaji huku Serikali ikiendelea na
uboreshaji wa huduma za matibabu kwa kushirikiana na wadau wote wa sekta ya
afya.
|
1. Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Emanuel Humba akitoa maelezo ya utangulizi katika mkutano huo, kulia ni Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, Jumanne Sagini |
|
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hussein Mwinyi akitoa maelekezo kwa watendaji, kulia ni Waziri wa TAMISEMI, Hawa Ghasia. |
|
Mawaziri wakiteta jambo katika mkutano huo. |
|
Dk. Mwinyi akiendelea kusisitiza jambo |
|
Ofisa kutoka NHIF anayeshughulikia CHF, Rehani Athumani akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Mfuko huo katika kikao kazi hicho |
|
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Regina Kikuli akitoa mwongozo wa majadiliano. |
|
Mkurugenzi NHIF akijibu hoja za wajumbe. |
|
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Joseph Mgaya na Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo wakifuatilia mjadala |
|
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Hamis Mdee akifuatilia mjadala |
|
Dk. Mwinyi akifunga kikao
|