Thursday, August 2, 2012

NHIF, TAMISEMI, WAUJ WAJADILI UBORESHAJI HUDUMA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma 

UBORESHAJI wa huduma za matibabu kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya hususan upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma ni moja ya mambo yaliyojadiliwa mwishoni mwa wiki katika kikao kazi kilichojumuisha wataalam kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na TAMISEMI. 

Katika kikao kazi hicho ambacho kilihudhuriwa na maofisa wa ngazi za juu katika taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na TAMISEMI wakiwemo mawaziri wa pande zote mbili, walijadili kwa kina namna ya kupunguza ama kuondoa kabisa tatizo la dawa ambalo wanachama na wananchi kwa ujumla wanakutana nalo wakati wa kupata huduma za matibabu.

Kwa upande wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, kupitia Mkurugenzi wake Mkuu, Emanuel Humba alisema kuwa Mfuko utaendelea na uboreshaji wa huduma za matibabu kupitia mpango wa Mfuko huo wa mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo kwa vituo vilivyosajiliwa na Mfuko huo lakini pia kuendelea kusajili maduka ya dawa muhimu ili wanachama wapate huduma inayotakiwa na wananchi waone umuhimu wa kujiunga na Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF). 

Aidha kwa upande wa Bohari ya Dawa (MSD) ambao ndio wana jukumu la usambazaji dawa, kupitia Mkurugenzi wake Mkuu Joseph Mgaya, alisema kuwa wanaendelea kushughulikia changamoto zilizopo kama kutokuwepo kwa maoteo sahihi ya dawa ili hatimaye idara hiyo iweze kuondokana na malalamiko yanayoelekezwa kwake. 

Wakihitimisha kikao kazi hicho, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) Hawa Ghasia, walizitaka pande zote mbili kuhakikisha zinatekeleza maafikiano yaliyofikiwa katika kikao hicho ili kipa upande uweze kutoa huduma nzuri kwa wananchi wa Tanzania.

Aidha walisema kuwa njia pekee ya kuwakomboa wananchi au kuwafanya wawe na uhakika wa kupata matibabu ni kuwahamasisha kujiunga na Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF) hivyo wakaitaka NHIF kuhakikisha inaongeza kasi ya uelimishaji huku Serikali ikiendelea na uboreshaji wa huduma za matibabu kwa kushirikiana na wadau wote wa sekta ya afya.

1. Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Emanuel Humba akitoa maelezo ya utangulizi katika mkutano huo, kulia ni Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, Jumanne Sagini

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hussein Mwinyi akitoa maelekezo kwa watendaji, kulia ni Waziri wa TAMISEMI, Hawa Ghasia.

Mawaziri wakiteta jambo katika mkutano huo.

Dk. Mwinyi akiendelea kusisitiza jambo



Ofisa kutoka NHIF anayeshughulikia CHF, Rehani Athumani akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Mfuko huo katika kikao kazi hicho

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Regina Kikuli akitoa mwongozo wa majadiliano.

Mkurugenzi NHIF akijibu hoja za wajumbe.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Joseph Mgaya na Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo wakifuatilia mjadala

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Hamis Mdee akifuatilia mjadala

Dk. Mwinyi akifunga kikao





No comments:

Post a Comment