Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza akisisitiza jambo kwa uongozi wa NHIF kwenye uzinduzi wa ofisi mpya ya Mfuko huo iliyoko Kibaha. |
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF akitoa maelezo ya awali kabla ya uzinduzi wa Ofisi hiyo. |
Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Kibaha Dk. Mpemba akitoa neno la shukrani kwa uongozi wa Mfuko katika uboreshaji wa huduma za matibabu. |
Baadhi ya Maofisa wa Mfuko na wageni waalikwa wakisikiliza kwa makini |
Wakibadilishana mawazo namna ya uboreshaji wa huduma za matibabu mkoani Pwani |
Baadhi ya Wakurugenzi wa NHIF wakibadilishana mawazo kabla ya kuanza kwa hafla ya uzinduzi wa Ofisi hiyo. |
Maofisa waliokuwa wakiandaa shughuli hiyo. |
RC Mahiza aziundua ofisi mpya za NHIF
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Bi. Mwantumu Mahiza ameutaka Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya kuisaidia kwa hali na mali Hospitali ya Tumbi kutokana
na umuhimu wake katika kuhudumia wagonjwa mbalimbali wakiwemo majeruhi wengi wa
ajali zinazotokea katika maeneo ya mkoa huo.
Alisema kuwa kutokana na changamoto nyingi zinazoikabili
Hospitali hiyo ikiwemo ya kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa kwa siku, ukosefu wa
Vifaa vya kisasa vya uchunguzi, kuna haja kubwa kwa NHIF kuingilia kati ili
kuinusuru hospitali hiyo na maisha ya Watanzania kwa ujumla.
Bi. Mahiza aliyasema hayo jana katika uzinduzi wa Ofisi
mpya ya NHIF iliyopo mkoani Pwani ambayo iliwakilisha Ofisi zingine mpya nane
zilizopo katika Mikoa ya Mara, Kigoma, Ruvuma, Rukwa, Singida, Lindi,
Shinyanga, Kagera na Manyara ambazo zimefunguliwa na NHIF kwa lengo la kusogeza
huduma kwa wanachama wake na kuboresha huduma kwa ujumla.
“Nimefarijika sana kwa kutupa heshima kubwa Mkoa wa
Pwani, mngeeamua kwenda Mkoa mwingine kuzindua ili kuziwakilisha ofisi zingine,
Niwaombe sana wenzangu NHIF, mtupe umuhimu wa kipekee katika kutusaidia vifaa
tiba na hasa kifaa cha kutunzia damu salama, inashangaza na haieleweki kwa
wasomi kama sisi kuona ajali na wagonjwa wakiwa Pwani na damu ikitunzwa Dar es
Salaam...nakuagiza Mganga Mkuu wasilisha ombi hilo NHIF haraka iwezekanavyo,”
alisema Mahiza.
Alisema kuwa suala la vifaa vya uchunguzi katika hospitali
hiyo linamnyima usingizi kutokana na mazingira yanayoikabili hospitali hiyo
ambayo kwa wastani inapokea wagonjwa 500 kwa siku.
Akijibu ombi hilo la Mkuu wa Mkoa, Mjumbe wa Bodi ya
NHIF, Bi. Mwanaidi Mtanda alisema kuwa Bodi itahakikisha inatoa kipaumbele
katika suala hilo kwa lengo la kuwezesha hospitali hiyo kuwa na vifaa vya
kisasa ili huduma bora kwa wanachama na wananchi kwa ujumla zipatikane.
“Kwa niaba ya Bodi niseme kuwa Mfuko una nia ya dhati ya
kusaidia Hospitali ya Tumbi na Mkoa wa Pwani kwa ujumla kwa lengo la kuboresha
huduma na pale tutakapopokea maombi kutoka kwenu yatafanyiwa kazi haraka sana,”
alisema Bi. Mtanda.
Bi. Mtanda hakusita kusema kuwa hamasa ya utumiaji wa
fursa inayotolewa na NHIF ya utoaji wa mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa
majengo kwa vituo hasa vya serikali bado ni mdogo hivyo akatumia fursa hiyo
kuwaomba viongozi na wamiliki wa vituo vyote vya matibabu vilivyosajiliwa na
Mfuko kuomba mikopo hiyo ili kuviwezesha vituo vyao kutoa huduma bora za
matibabu.
Hata hivyo, Bi. Mwantumu alieleza wazi kuwa NHIF imekuwa
chachu kubwa katika maendeleo ya sekta ya afya kutokana na ukweli kwamba vituo
vingi vinaendesha shughuli zake kwa kutumia fedha zinazolipwa na Mfuko huo.
“Mtu yeyote anayefuatilia mwenendo wa Sekta ya Afya
nchini atakubaliana nami nikisema Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, umekuwa
chachu kubwa katika maendeleo ya sekta ya afya kwani kwa kiwango kikubwa vituo
vingi vinaendesha shughuli zake kwa fedha zinazolipwa na Mfuko huo hivyo
nawapongeza na kuwataka muendelee kusaidia,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa NHIF, Bw. Emanuel Humba alisema
kuwa lengo la uzinduzi wa ofisi hizo ni kutaka kuwajulisha wadau kuwa Mfuko
umesogeza huduma zake karibu na wanachama ikiwa ni njia mojawapo ya uboreshaji
wa huduma.
Alisema pamoja na Mfuko huo kukua kwa kasi na kuwa na
mafanikio makubwa lakini bado unakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za
ukosefu wa dawa, vifaa tiba, upungufu wa wahudumu changamoto ambazo Mfuko
unazifanyia kazi kupitia mipango mbalimbali ikiwemo ya kusajili maduka ya dawa
muhimu na ukopeshaji wa vifaa tiba.
NHIF kwa sasa ina mtandao wa ofisi zake katika Mikoa yote
Tanzania Bara na Zanzibar isipokuwa mikoa mipya.
No comments:
Post a Comment