Hayati Baba wa Taifa Mwl, Julius Nyerere |
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emanuel Humba. |
KATIKA
kuhakikisha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anaenziwa kipekee, Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya (NHIF) unaendesha zoezi la upimaji afya za wanachama na wananchi
kwa ujumla mkoani Shinyanga ambako kilele cha maadhimisho hayo yatafanyika
Oktoba 14, mwaka huu.
Akizungumzia
zoezi hilo, Mkurugenzi wa Uendeshaji Eugen Mikongoti alisema kuwa, Mfuko
umefikia uamuzi huo kwa lengo la kuenzi mazuri yote yaliyofanywa na Baba wa
Taifa enzi za uhai wake.
“Baba
wa Taifa aliapa kupigana na maadui watatu ambao ni Umasikini, Ujinga na Maradhi
na katika hayo sisi ni wadau wakubwa katika kupambana na adui maradhi na ndio
maana tumeona tumuenzi kwa njia hii ambapo wananchi watapima afya zao bila
malipo na kupata ushauri wa kitaalam ili kuepukana na maradhi yasiyoambukiza,”
alisema Mikongoti.
Mbali
na upimaji wa afya kwa wananchi, alisema kuwa Mfuko unatumia fursa hiyo kujibu
kero mbalimbali za wanachama wake ambao watafika katika viwanja vya Sabasaba ambako
Mfuko umeweka banda kwa ajili ya kuendesha zoezi la upimaji na utoaji wa elimu
juu ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii, kwa muda wa
siku tano, kuanzia jana.
Alisema
kuwa lengo kubwa la NHIF ni kuhakikisha wanachama wake na wananchi kwa ujumla
wanapata huduma bora za matibabu na Vituo vya kutolea huduma hizo vinaboreshwa
kwa kuwa na vifaa vya kisasa vya uchunguzi kupitia fursa inayotolewa na Mfuko
huo ya mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo.
“Mfuko
umekuwa na jitihada mbalimbali za kuhakikisha huduma za afya vituoni zinakuwa
bora na unafanya hivyo kwa kutambua kuwa mhimili mkubwa wa Mtanzania katika
kufanya kazi na kujiondolea umasikini ni afya yake kwanza…nawaomba wananchi wa
Shinyanga na wa maeneo mengine mfike katika banda letu ambalo linatoa huduma za
upimaji na elimu ya afya kwa ujumla,” alisema.
Mikongoti
alisema kuwa Mfuko utaendelea kumuenzi Baba wa Taifa katika kupambana na adui
maradhi kwa kuhakikisha Watanzania wanakuwa na uhakika wa matibabu kupitia
utaratibu wa kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya
Jamii.
Wakati
huo huo, Mfuko umeendelea na jitihada zake
za kuhakikisha makundi maalum yanapata huduma bora baada ya kuchangia jumla ya
shilingi milioni 1.5, shuka 80 na fulana 80 kwa Kituo cha Mihuji Chesire Home
kilichopo mjini Dodoma ambacho kinalea watoto wenye matatizo ya mtindio wa
ubongo.
Mchango huo wa NHIF ulitolewa
mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Dodoma katika harambee ya kuchangia kituo
hicho na Meneja wa Kanda ya Kati Dkt. Daudi Bunyinyiga ambaye alimwakilisha
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Emanuel Humba.
Akiwasilisha
mchango huo, Dokta Bunyinyiga alisema kuwa Mfuko kama Taasisi inayofanya kazi
na Jamii inawajibu wa kuhakikisha jamii inayoizunguka hususani watu wenye
mahitaji maalum wanafaidika na huduma zake.