Friday, September 16, 2011

Mama Maria atoa pole kwa maafa Zanzibar

 Na Grace Michael, Butiama
MAMA Maria Nyererea ambaye ni Mjane wa Baba wa Taifa, ametoa pole kwa Taifa na kuonesha masikitiko yake juu ya maafa yaliyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita yaliyosababishwa na ajali za kuzama kwa Meli ya Mv Spice Islanders katika Mkondo wa Nungwi.
 
Mbali na maafa hayo makubwa, pia Mama Maria ametoa pole kwa waliofikwa na maafa yaliyotokana na kupasuka kwa bomba la mafuta jijini Nairobi Kenya ambapo mamia ya watu walipoteza maisha.
Mama Maria aliyasema hayo juzi nyumbani kwake Butiama wakati akizungumza na baadhi ya waandishi waliomtembelea kwa lengo la kumjulia hali na kuzulu kaburi la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
“Kwa kweli natoa pole kwa Taifa zima kutokana na msiba mzito uliotokea huko Zanzibar lakini na kwa Afrika Mashariki nzima...ni msiba mzito sana,” alisema Mama Maria.
 
Akizungumzia afya yake, alisema ni njema na anafarijika kuona watu wakizulu makazi ya baba wa Taifa na kwa lengo la kumjulia hali yeye mwenyewe.
“Mimi afya yangu ni nzuri sijui wengine...lakini kwa upande wangu ni mzima kabisa, nimefarijika sana kunitembelea kwani nikiona hivi nafurahi sana,” alisema.
Alieleza kufurahishwa na kufarijika kutokana na hatua Watanzania kumtembelea mara kwa mara ili kumjulia hali nyumbani kwake.
“Wakati mwingine si jambo rahisi kwa watu kukutembelea kila mara wakati si mtumishi wa serikalini, ni mstaafu.Wapo watumishi wa serikali ambao baada ya kustaafu hawapati bahati ya kutembelewa na wananchi, hii ni bahati na inanifariji sana,” alisema Mama Maria
Meli ya Mv Spice Islanders ilizama katika Mkondo wa Nungwi, alfajiri ya kuamkia Septemba 10, mwaka huu ilipokuwa safarini kutoka Kisiwa cha Unguja kwenda kisiwani Pemba
Katika tukio la kupasuka kwa bomba la mafuta katika Jiji la Nairobi, watu zaidi ya 100 wameripotiwa kufa na wengine kujeruhiwa vibaya kutokana na bomba hilo kulipuka moto na kuwateketeza watu walikuwa wakichota mafuta yaliyokuwa yakitiririka.
Mama Maria alisema Watanzania na watu wa Afrika Mashariki wapo katika masikitiko makubwa kutokana na vifo vya ndugu, jamaa na marafiki zao vilivyosababishwa na matukio ya ajali hizo mbili.
 

Thursday, September 8, 2011

Wahandisi wataka kujitosa kumaliza tatizo la umeme


Na Grace Michael

BODI ya Usajili ya Wahandisi (ERB), imesema tatizo la umeme linaloikabili nchi kwa sasa lisingefika hapo lilipo endapo serikali ingewashirikisha wataalam hao katika hatua mbalimbali.

Kutokana na hali hiyo, wameiomba serikali kuhakikisha inatoa ushirikiano wa kutosha katika mambo mbalimbali yanayohusu fani hiyo, ili kuepukana na matatizo kama tatizo la umeme kwa sasa.

Akitoa salamu za bodi hiyo wakati wa kufunga wa mkutano uliokutanisha bodi tatu za sekta ya ujenzi, Bw. Gema Modu, alisema kuwa; “Kungekuwa na ushirikishwaji wa uhakika katika suala la umeme, suluhu ingekuwa imepatikana, hata tatizo hili lisingefikia hapo lilipo,”

Aliongeza kuwa; “Tatizo hili la umeme kwa upande wetu tunalichukulia kwa sura mbili moja ikiwa ni tatizo na nyingine ni fursa kwetu ya kuingia kufanya kazi hiyo na katika hili tumejipanga na tutaingia huko kwa lengo la kusaidia.”

Bodi nyingine zilizoshiriki mkutano huo ni pamoja na Bodi ya Wakandarasi (CRB), Bodi ya Wasanifu na Wakadiria majengo ambao kwa pamoja walijadili masuala mbalimbali ya sekta ya ujenzi na hatimaye kutoka na maamuzi ambayo yatawasilishwa serikalini kwa lengo la kuboresha sekta hiyo.

Mkutano huo ambao ulifungwa na Waziri wa Miundombinu Dkt. John Magufuli kwa niaba ya Makamu wa Rais Dkt. Mohamed Gharib Bilali, aliwataka wataalam hao kuwa wawazi katika mambo wanayotaka serikali iyafanyie kazi hata kama ni makali.

Andikeni mahitaji yenu kwa uwazi, msiwe wanasiasa katika kazi zenu...hata kama ni maneno makali andikeni na wenyeviti wa bodi waweke saini zao nami nitayapeleka kwa rais bila kuchakachua kitu chochote,” alisema Dkt. Magufuli.

Aidha aliwataka wote kwa pamoja kushirikiana katika kazi na kuachana na utamaduni wa kupigana vijembe na rushwa katika kazi na badala yake watangulize uzalendo katika shughuli zao kwa kuwa fani za ujenzi ndizo zenye mwelekeo wa maendeleo ya nchi, lakini pia ndizo zimeshikilia uchumi wa nchi.

Kwa mujibu wa hotuba ya Makamu wa Rais, serikali itazidi kuwashirikisha katika kazi za umma na kutoa upendeleo kwa wazalendo katika kazi hizo, lakini akaonya kuwa wasifanye kazi ambazo ziko chini ya kiwango.

Tunatambua kuwa kuna tatizo la mitaji na katika hili tunatoa mwito kwa mabenki kuwatazama kwa jicho la pekee wakati mnapojitokeza kuomba mikopo...suala la msingi ni kufanya kazi zenye viwango kwa kuwa serikali tunachefuliwa sana na majengo mabovu na kazi zote ambazo ziko chini ya kiwango,” alisema hotuba hiyo.

Alisema kuwa serikali inatambua madeni inayodaiwa na wataalam hao na ikaahidi kuwa sehemu kubwa ya madeni hayo italipwa hivi karibuni.



Hata hivyo washiriki wa mkutano huo wamekubaliana kupambana na tatizo la rushwa na wakashauri kuwepo mjadala wa wazi ambao utajadili suala hilo kwa uwazi na bila kuoneana aibu kwa kuwa rushwa ni ugonjwa unaoweza kuliua taifa.

Wednesday, August 31, 2011

Bunge lalalia hoja za msingi


Tumaini Makene na Grace Michael

PAMOJA na mkutano wa nne wa Bunge la 10 kumalizika kwa kutimiza moja ya majukumu yake ya kikatiba ya kuisimamia serikali ambapo imeunda kamati teule kufuatilia tuhuma za ufisadi katika sakata la Bw. David Jairo, bado Bunge hilo limeendelea 'kukalia' hoja mbalimbali, zinazoonekana kuibua masuala mazito nchini, hasa zile ambazo baadhi ya wabunge wamekuwa wakiwabana viongozi wa serikali.

Mbali ya kukalia hoja hizo binafsi za wabunge, mkutano wa nne pia umeendelea kuliweka kiporo suala nyeti la mjadala wa uandikwaji wa katiba mpya nchini, ambapo suala hilo lilikuwa katika ratiba ya vikao vya mkutano huo uliomalizika mwishoni mwa juma lililopita, lakini muswada uliopaswa kuwasilishwa, uliondolewa baadaye na kamati ya uongozi, inayohusika katika kupanga ratiba za vikao vya Bunge na masuala ya kujadiliwa katika mkutano husika.

Imeelezwa na Kaimu Katibu wa Bunge, Bw. John Joel kuwa kamati hiyo iliona kuwa suala hilo ni nyeti na hivyo halikupaswa kujadiliwa katika muda mfupi wa mkutano huo wa nne ambao ulikuwa na masuala mengi ya kibajeti, hivyo wabunge waingepata muda wa kutosha kuujadili muswada huo kwa kina, ikaonekana ni vyema urudishwe kwenye kamati husika ya bunge, ili wadau mbalimbali nchini waendelee kutoa maoni yao.

Zitto na Baraza la Mawaziri

Bw. Zitto Kabwe ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini ambaye aliibua tuhuma nzito bungeni dhidi ya Baraza la Mawaziri ambalo alisema limekuwa likifikia maamuzi kutokana na kurubuniwa.

Bw. Zitto alitoa tuhuma hiyo kwa kujiamini na akaenda mbali zaidi kwa kusema kuwa hawezi kutafuna maneno kwa kuwa anaamini anachokisema kuwa baraza hilo ndivyo linavyofanya kazi.

Tuhuma hiyo aliziibua wakati akichangia Azimio la Serikali linalohusu kuongeza muda wa uhai wa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC), ambapo alipingana moja kwa moja na azimio hilo ambalo lilitaka kuongezwa muda wa miaka mitatu kwa CHC.

"Jamani tulikubaliana vingine kabisa katika Kamati na leo kilicholetwa hapa ni kitu kingine, Kamati ya Fedha na Uchumi ilijadili na kutaka shirika hili lipewe muda zaidi kutokana na majukumu yaliyo mbele yake lakini hiki kilicholetwa hapa ni kitu kingine...wabunge kataeni haya maamuzi ya baraza la mawaziri kwa kuwa yametokana na kurubuniwa na watu wenye lengo la kuua CHC kwa ajili ya maslahi yao," alisema Bw. Zitto.

Kutokana na tuhuma hizo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI),George Mkuchika aliomba mwongozo kwa spika akitaka Bw. Zitto athibitishe kauli yake hatua iliyomfanya Bi. Makinda kumpa muda wa siku saba kuthibitisha tuhuma hizo.Pamoja na Bw. Zitto kuwasilisha ushahidi wake kama alivyotakiwa, lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika juu ya tuhuma hizo.

 
Chadema na Spika Makinda

SAKATA la Chama cha Demokrasia (CHADEMA) na Spika wa Bunge Bi. Anne Makinda nalo limewekwa kiporo mpaka sasa.

CHADEMA walimshtaki Bi. Makinda katika Kamati ya Kanuni ya Bunge ambapo walilalamikia kitendo cha kuendesha Bunge kwa upendeleo hasa katika mijadala mbalimbali ambapo walidai anaipendelea serikali.

Hata hivyo Bi. Makinda alikaririwa na vyombo vya habari likiwemo Majira akisema: "Niko tayari kuhojiwa, kwa kuwa nafahamu kuwa kila jambo linalofanyika ndani ya bunge linafuata kanuni na huo ndio utaratibu hivyo mambo ya bungeni lazima yamalizikie bungeni," alisema Spika Makinda.
 
Katika hilo, Bi. Makinda alisema kuwa asingeruhusu kujadiliwa kwa mambo waliyohoji  kwa kuwa jambo likiwa mahakamani haliwezi kujadiliwa bungeni na ikifanyika hivyo itakuwa ni kuingilia mhimili mwingine.

Hoja nyingine ambayo mtoaji wake aliambiwa na kiti awasilishe ushahidi kuthibitisha kauli yake ni ya Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, ambaye alitoa tuhuma nzito juu ya ufisadi wa matumizi mabaya kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, akimtuhumu kuwa hawezi kutekeleza kwa vitendo yale ambayo amekuwa akiyasema, hasa katika kupunguza gharama za matumizi kwa serikali.

Akichangia hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka 2011/2012, Mchungaji Msigwa alimtuhumu Bw. Pinda kuwa alitumia ndege mbili za serikali kwenda Iringa kufungua barabara, ambapo pia msafara wake uliokuwa na magari yapatayo 50 alifunga barabara za Dar es Salaam-Morogoro na Iringa kwa takriban masaa matano, hivyo kuzuia shughuli za kiuchumi na kijamii.

Pia mbunge huyo alitoa tuhuma kwa serikali kuwa imekuwa ikiua watu na kuwajeruhi kwa kipigo katika maeneo mbalimbali nchini, akitolea mifano ya mauaji ya wananchi katika Mgodi wa North Mara huko Nyamongo (Tarime), mauaji ya watu watatu huko Arusha, wakati wa maandamano ya amani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kipigo walichopewa baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu Dodoma, hadi wengine wakalazwa hospitalini kwa kujeruhiwa.

Hoja hizo ya Mchungaji Msigwa ambayo ni kati ya hoja zilizoibua 'utaratibu, mwongozo, taarifa' katika mkutano ulioisha, iliilazimisha serikali kuingilia kati kupitia kwa Waziri William Lukuvi, ambaye kwa kutumia kanuni ya 64:(1) (b )ya Kanuni za Kudumu za Bunge, inayosema mbunge yeyote hatazungumzia jambo ambalo haliko kwenye mjadala, akimtaka mbunge huyo kuthibitisha kauli yake.

Hoja nyingine ya Mchungaji Msigwa ilihusiana na ukiukwaji wa sheria ya mafao ya wanasiasa wastaafu, ambapo alituhumu kuwa Spika wa Bunge la 9, Bw. Samuel Sitta anaendelea kukaa katika nyumba ya spika akidai imekodishwa kwa dola 8,000 za Marekani takriban milioni 12 kwa mwezi, akisema kitu hicho si stahili yake, suala ambalo hata hivyo lilizimwa na Spika Anna Makinda, akimzuia Waziri Mkuu Pinda asilijibu swali hilo katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo.

Mchungaji Msigwa akizungumza na Majira jana, alishikilia msimamo wake kuwa anao ushahidi wa hoja zake hizo na kuwa yuko tayari kuutoa wakati wowote akihitajiwa, akiongeza kusema kuwa sheria ya mafao ya viongozi wastaafu wa kisiasa haizungumzi juu ya spika mstaafu kupewa nyumba na serikali, isipokuwa gari moja na dereva ambavyo bunge litalazimika kuvihudumia kwa matengenezo, lita 70 za mafuta. 

Kitu kingine kinachoibua mkanganyo mkubwa katika suala hilo na pengine kulazimisha taifa kuangalia mfumo mzima wa mafao ya wastaafu na stahili za watumishi wa serikali, watendaji na wanasiasa, ni kuwa sasa Bw. Sitta 'analazimika' kupata mafao hayo ya bunge, lakini pia stahili zake kama waziri, kwa maana ya gari la serikali, nyumba na kama anaishi katika nyumba yake binafsi, serikali inatakiwa kumlipa fedha za fidia ya gharama za nyumba.

Hoja nyingine ambayo nayo imeonekana kulaliwa na haijulikani itatolewa maelezo lini ni juu ya tuhuma alizotoa Mbunge wa Singida Mashariki, Bw. Tundu Lissu Mbunge wa Singida, akisema kuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu), Bw. Kassim Majaliwa alisema uongo bungeni, kulidanganya bunge juu ya michango wanayochangishwa wananchi.

Akijibu swali Namba 313, Bw. Majaliwa alisema kuwa michango mbalimbali wanayochangishwa wananchi nchini wamekuwa hawalazimishwi kwa serikali kutumia nguvu, bali wanashirikishwa kuiibua, kupanga na kuendesha miradi wao wenyewe, lakini Bw. Lissu aliliambia bunge kuwa kwa majibu hayo, waziri huyo alilidanganya bunge na kuwa angeweza kuthibitisha uongo huo siku hiyo hiyo kwa maandishi.

Pamoja na kupewa muda wa takribani masaa mawili awe tayari amewasilisha usahidi wake, mpaka mkutano wa bunge unamalizika hakukuwa na kauli yoyote kuonesha kuwa ushahidi ulipokelewa na kuwa tayari unafanyiwa kazi, pengine kwa uharaka ule ule wa kuombwa kuthibitisha.

Akizungumza na Majira jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Bunge, Bw. John Joel alisema kuwa hoja za Bw. Zitto, Bw. Lema na Bw. Lissu zimeshawasilishwa kwa spika, ambapo kanuni zinamwelekeza kuzisoma na kujiridhisha nazo kwanza kabla hajaamua kuziweka wazi bungeni, ambapo iwapo mbunge husika atashindwa kuthibitisha kauli yake aliyotoa bungeni katika hoja yake hiyo, atakabiliwa na adhabu.

Lakini katika hali ambayo inaibua changamoto kwa kanuni za bunge, Bw. Joel alisema kuwa kanuni hizo 'ziko kimya' pale ambapo mbunge atafanikiwa kuthibitisha katika hoja yake 'ukweli' wa kile alichokisema bungeni, hatua zipi zitachukuliwa dhidi ya mtu huyo. Mjadala unaweza kuwa mkubwa mathalani katika hoja ya Bw. Zitto, ambaye alilituhumu Baraza la Mawaziri kuwa lilishawishiwa katika uamuzi wake, hivyo akiweza kuthibitisha bunge litaliwajibishaje baraza hilo.

"Spika hana limit (ukomo wa muda) katika kuzipitia na kuziwasilisha hoja hizo bungeni, lakini ni lazima ajiridhishe kuwa kilichowasilishwa kiko katika mfumo fulani...kama ikibainika kuwa mbunge alidanganya basi atapewa adhabu, ziko adhabu kadhaa...ndiyo maana si vizuri kukimbilia kuzipeleka bungeni kwa suala ambalo spika anakuwa hana uhakika nalo, lazima spika ajitosheleze. 

Alipoulizwa juu ya hatua gani zitachukuliwa kwa upande wa pili, iwapo mbunge mto hoja ataweza kuthibitisha kauli yake, Bw. Joel alisema: "kanuni ziko kimya katika suala hilo...lakini kwa mfano kama aliyetuhumiwa ni waziri kuwa alilidanganya bunge, spika anaweza kumwambia afute kauli yake hiyo. Lakini ndiyo maana hata juzi umemsikia spika akisema tumemaliza mzunguko wa kanuni zetu, hivyo zinapaswa kuangaliwa upya."

Akizungumzia juu ya 'kesi' iliyofunguliwa na CHADEMA kwa Kamati ya Kanuni, ikihoji uadilifu wa Spika Makinda katika kusimamia masuala ya msingi ya kitaifa, hasa pale serikali inapobanwa bungeni kutoa majibu, ambapo amedaiwa kuwa amekuwa akitumia madaraka yake vibaya kuiokoa serikali, hivyo kuwakwaza wabunge kutimiza wajibu wao wa kikatiba, Bw. Joel alisema kuwa tayari imeshawasilishwa kwa kamati hiyo, ambayo itakaa wakati wowote, kupitia hoja za chama hicho.

"Spika na Naibu Spika si kwamba wanajiuzulu nafasi zao katika kamati hiyo, kinachotokea ni spika kutokuwa mwenyekiti, yaani hatakalia kiti chake cha uenyekiti wakati wa kusikiliza hoja hiyo, kwa kuwa anaweza kuhitajika kuleta maelezo ya kujitetea, hivyo spika na naibu wake wote hawatakuwemo wakati wa kikao," alisema Bw. Joel.  

  

Wednesday, August 24, 2011

Wabunge wachachamaa sakata la Jairo

Siku moja baada ya Katibu Mkuu Kiongozi kumwamuru Katibu Mkuu wa Nishati na Madini Bw. David Jairo kurejea kazini kutokana na tuhuma zilizokuwa zikimkabili kushindwa kuthibitika, wabunge wamekuja juu wakitaka uthibitisho huo usitishwe kwa kuwa hawakushirikishwa.

Wamekwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa Bw. Luhanjo ameridharau Bunge hoja ambayo iliwasilishwa na Mbunge Kigoma Kaskazini Bw. Zitto Kabwe na kuungwa mkono na wabunge wote.

Wakati hayo yakiendelea, Bw. Jairo ameanza kazi rasmi na kusema kuwa yeye binafsi hawezi kumchukia mtu ila anaamini kilichofanywa na CAG ndicho sahihi.

Jairo hana hatia-CAG

*Luhanjo aamuru aanze kazi leo
*Asema hakupatina na kosa lolote

Na Grace Michael

KATIBU Mkuu Kiongozi Bw. Phillemon Luhanjo ameamuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Bw. David Jairo kurejea mara moja kazini kwa kuwa uchunguzi uliofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) haujamkuta na hatia yoyote.

Bw. Jairo, ambaye alisimamishwa kazi Julai 21, mwaka huu ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizotolewa bungeni wakati wa kuwasilisha wa hotuba ya bajeti ya Wizara yake ambapo alidaiwa kuchangisha jumla ya sh. bilioni moja  kuwahonga wabunge wapitishe bajeti ya wizara hiyo.

Akitoa uamuzi juu ya uchunguzi uliofanywa na CAG dhidi ya tuhuma hizo, Bw. Luhanjo alisema:

“Kutokana na matokeo haya ya uchunguzi wa awali ambao umefanywa kwa umakini mkubwa na kushindwa kuthibitisha tuhuma hizo, mimi kama Mamlaka ya nidhamu ya Katibu Mkuu wa Nishati na Madini David Jairo, sitaweza kuendelea na hatua ya pili ya kumpa taarifa ya tuhuma na hati ya mashtaka kwa kuwa Jairo hajapatikana na kosa lolote la kinidhamu,” alisema Bw. Luhanjo.

Kutokana na hatua hiyo, alisema kwa mujibu wa sheria namba 8 ya Utumishi wa Umma na kanuni zake anamwamuru Bw. Jairo kurejea kazini mara moja ambapo atatakiwa kuingia ofisini kwake leo.

Akifafanua matokeo ya uchunguzi wa tuhuma hizo, CAG Ludovick Otouh alianza kwa kueleza chimbuko la uchunguzi huo ambapo alisema ulitokana na wabunge waliohoji uhalali wa wizara kuomba michango kutoka kwenye taasisi kwa lengo la kushawishi baadhi ya wabunge kupitisha bajeti kirahisi.

Alisema kuwa ukaguzi huo ulifanyika kulingana na hadidu rejea zilizokuwa na lengo la kutafuta ukweli kuhusu tuhuma za michango na matumizi ya fedha zilizochangwa na wizara.

“Kazi hii ilihusisha kufanya mapitio ya nyaraka mbalimbali, vitabu vya risiti, hati
za malipo na taarifa za benki kwa kipindi cha mwezi Mei hadi Julai mwaka huu na timu ya wakaguzi iliwahoji watu kutoka taasisi zilizochangishwa, wizara, wabunge na wakala wa Jeolojia Tanzania," alisema CAG.

Alisema ukaguzi ulibaini kuwa idadi ya taasisi zilizopewa barua za kuchangia gharama za kuwasilisha bungeni bajeti ya wizara zilikuwa ni nne na sio 20 kama ilivyokuwa ikidaiwa na wabunge na utafiti huo ulibaini kuwa jumla ya fedha zilizochangwa ni sh. milioni 149.7.

Mbali na fedha hizo zilizochangwa na taasisi lakini pia ukaguzi huo ulibaini kuwa idara ya uhasibu ya wizara ilitoa sh. milioni 150.7 kwa ajili ya posho za vikao vya kazi katika uandaaji wa uwasilishwaji wa bajeti hiyo lakini pia Idara ya Mipango ya wizara nayo ilichanga sh. milioni 278 kwa ajili ya kazi hiyo.

Aidha CAG alifafanua kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) iligharamia chakula cha mchana cha sh. milioni 3.6 na tafrija iliyofanyika Julai 18, mwaka huu ambayo iligharimu sh. milioni 6.1.

“Jumla ya michango iliyochangwa ni sh. milioni 578.5 na sio bilioni moja kama ilivyotajwa kwenye tuhuma na taasisi zilizodaiwa kuhusika sio 20 kwa kuwa wizara hiyo ina taasisi zisizo zidi saba,” alisema Bw. Otouh.

Ukaguzi huo pia haukupata ushahidi wowote wa fedha zilizochangwa kutumika kuwalipa wabunge malipo yoyote kwa madhumuni ya kuwahonga bali malipo yaliyofanyika yalihusu posho za kujikimu, takrima na posho za vikao kwa maofisa walioshiriki katika kazi nzima ya uwasilishwaji wa bajeti.

Kwa mujibu wa taarifa za benki iliyotumika kukusanya fedha hizo hadi kufikia Julai 29, mwaka huu kiasi cha sh. milioni 20 kilikuwa ni fedha za matumizi ya fedha zilizochangwa na kupokelewa kwenye akaunti ya GST kabla ya kufanyika marejesho ya sh. milioni 99.4 na sh. milioni 14.8.

Kutokana na hali hiyo, CAG alisema kuwa jumla ya kiasi cha fedha kilichosalia kwenye akaunti hiyo kulingana na nyaraka za benki ni sh. milioni 195.2.

“Kwa kuwa ukaguzi maalum haukupata uthibitisho wa kuwepo taasisi 20 zilizotakiwa kuchanga bilioni moja kama ilivyodaiwa na wabunge, ukaguzi haukuthibitisha kuwepo kwa usahihi wa tuhuma zilizotolewa dhidi ya Bw. Jairo,” alihitimisha CAG.

Hata Hivyo waandishi wa habari walipohoji ni kwa nini vyombo vingine vya dola ikiwamo TAKUKURU na polisi havikuhusishwa kwenye uchunguzi huo, Bw. Luhanjo alisema kuwa suala hilo lilikuwa ni tatizo la kiutawala wa kifedha na sio rushwa wala kosa la jinai.

Alitumia mwanya huo, kuwaonya watumishi wa umma wanaojihusisha na uvujishaji wa siri na nyaraka za serikali kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria na kanuni za utumishi wa umma.

“Hata huyu aliyefanya hivi tukimpata naye atapata haki yake...ni kosa kubwa kuvujisha siri za serikali kwani usalama wa serikali ni wa mtumishi mwenyewe hivyo natoa onyo na iwe fundisho kwa watumishi wengine wenye tabia za kutoa siri za serikali,” alisema Bw. Luhanjo.

Hatua ya kusimamishwa kwa Bw. Jairo ili kupisha uchunguzi ilitokana na tuhuma zilizotolewa na wabunge wakati wa bajeti ya awali ya Wizara ya Nishati na Madini ambapo walidai kuwa Bw. Jairo amechangisha jumla ya sh. bilioni moja kutoka kwenye taasisi 20 zilizo chini ya wizara hiyo kwa lengo la kuwahonga wabunge kupitisha
bajeti hiyo.

Wednesday, August 17, 2011

EWURA sasa yakubali yaishe kanuni ya mafuta

Na Grace Michael
MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) imekubali kukaa na wadau kwa lengo la kukubaliana kurekebisha kanuni ili iweze kuelekeza namna ya kutathmini akiba ya mafuta yaliyoagizwa kabla ya kubadilisha bei katika kipindi husika.
Hatua hiyo ya EWURA inakuja siku chache baada ya kutangaza mabadiliko ya bei ya mafuta ambayo ilipanda ikilinganishwa na bei iliyokuwepo hatua iliyozua malalamiko miongoni mwa watumiaji ambao walifikia hatua ya kuhoji mchakato unaofanywa kufikia hatua ya kupandisha au kushusha bei ya mafuta.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Ofisa Uhusiano wa mamlaka hiyo, Bw. Titus Kaguo, alisema kuwa mbali na hatua ya kukaa na wadau kuona mchakato huo, lakini EWURA inafuatilia kwa karibu uanzishwaji wa mfumo wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja.
“Pamoja na maelezo tuliyoyatoa kama EWURA kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta, imeonekana wadau mbalimbali na umma kwa ujumla wangependa kuona mamlaka ikipitia upya utaratibu wake wa kutangaza bei za mafuta kila baada ya wiki mbili, kwa kuwa taasisi hii imekuwa sikivu na yenye kujali maoni ya wadau wetu tumeamua kuchukua hatua hizo,” alisema Bw. Kaguo.
Alisema kuwa mfumo wa uagizaji mafuta kwa pamoja utawezesha kupata kiasi halisi cha mafuta yatakayokuwa yakiagizwa na kujua bei zake kwa usahihi na bei hizo ndizo zitatumika katika kukokotoa bei kwenye kila kipindi husika.
Aidha mamlaka hiyo, imesema itaendeleza uhamasishaji wa ushindani wa haki katika soko ili kuendelea kuboresha huduma na bei kwa walaji lakini pia itaendelea kuzingatia maoni yanayotolewa na wananchi pamoja na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kanuni zinazotumika katika usimamizi na udhibiti wa biashara hiyo unaboreshwa.
“Ikumbukwe kuwa EWURA ilipoanza kupanga bei mwaka 2009, bei za mafuta katika soko la dunia zilikuwa chini sana lakini soko la ndani ilikuwa ni sh. 2,200 kwa lita, tuliingilia bei hiyo ikashuka hadi1,147 kwa lita hivyo ni dhahiri kuwa mfumo wetu unamnufaisha mlaji na ndio maana tunakubali kukua na wadau kujadili masuala haya,” alisema.
Akizungumzia mafuta ya taa ambayo yanaonekana kuadimika sokoni, Bw. Kaguo alisema kuwa takwimu walizonazo zinaonesha kuwa mafuta yananunuliwa kwa wingi kutoka kwenye maghala ya mafuta hivyo kama kuna tatizo hilo, mamlaka hiyo inalifuatilia kwa karibu ili kubaini ukweli wake.

Kazi ya EWURA isibezwe, tuwapeni nafasi

Na Grace Michael
JUNI 22, mwaka huu, Serikali kupitia Waziri wa Fedha na Uchumi wakati akihitimisha hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka 2011/12 ilitoa maagizo kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kuchukua hatua mbalimbali zitakazoshusha bei ya mafuta.
Kutokana na agizo hilo, EWURA ilianza kazi hiyo Julai 4,2011 ambapo ilipitia hatua mbalimbali kama kutoa matangazo kwenye vyombo vya habari kuhusu mchakato huo lakini pia ilishirikisha wadau ambao baadhi yao walichangia kwa maandishi na hatimaye mchakato wa utengenezaji wa kanuni mpya ukahitimishwa.
Mchakato huo wa kanuni mpya ndio uliofanikisha kushuka kwa bei ya mafuta ambayo ilitangazwa na mamlaka hiyo, Agosti 2, mwaka huu.
Kitendo cha kushuka kwa bei ya mafuta kilizua tafrani katika maeneo mbalimbali kwa kuwa huduma za mafuta zilikosekana baada ya wafanyabiashara wa mafuta kuamua kufunga vituo vyao wakitaka kushinikiza bei iliyokuwepo awali kubaki kama ilivyo
Sakata hilo ambalo lilidumu takiribani kwa muda wa wiki nzima, hatua iliyosababisha sakata hilo kuibuka bungeni na kujadiliwa kama suala la dharura, hatimaye serikali ikatoa maagizo kwa makampuni manne ikiyataka kuanza huduma mara moja.
Mbali na agizo hilo, pia ilikuja na mikakati kadhaa ya kuhakikisha suala hilo halijirudii tena.
Pamoja na hayo, EWURA haikuishia hapo, ilichukua hatua kwa Kampuni ya BP (T)Ltd kwa kuifungia leseni yake kwa muda wa miezi mitatu kwa kuwa ilikiuka amri halali ya mamlaka hiyo ambayo ilitaka warejeshe huduma kama kawaida.
Kwa kuwa sakata hilo lilichukua muda takribani wiki nzima na baadae huduma kurejea, tayari muda wa wiki mbili kwa EWURA kutangaza bei mpya uliwadia  ambapo Agosti 14, mwaka huu ilitangaza bei mpya  ambayo ilikuwa juu ikilinganishwa na iliyoleta mgomo.
EWURA walieleza sababu za kupanda kwa bei ya mafuta ambazo ni kushuka kwa thamani ya shilingi yetu ikilinganishwa na thamani ya dola ya Kimarekani ambayo ndiyo inatumika kununulia mafuta lakini pia sababu nyingine ilikuwa ni kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
Pamoja na mamlaka hiyo kueleza sababu hizo, bado ilizidi kulaumiwa huku wengine wakidai kuwa EWURA imezidiwa nguvu na wafanyabiashara na wengine kusema haina msimamo wa dhati.
Kwa hili napingana nalo kwa kuwa EWURA imekuwa ikitangaza bei hizi kila baada ya wiki mbili na bei zimekuwa zikipanda na kushuka takribani kwa muda wa miaka mitatu sasa.
Nionavyo mimi si muda muafaka wa kuibeza EWURA bali tuna jukumu kubwa la kuiunga mkono ili iweze kutekeleza majukumu iliyopewa kwa mujibu wa sheria.
Mtakubaliana na mimi kuwa bei zinaposhushwa na EWURA watumiaji huchekelea na bei inapopanda wafanyabiashara nao hufurahia huku watumiaji ikiwa ni kinyume chake hivyo hatuna sababu ya kuilaumu mamlaka hii kwa kazi inayofanya kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ilizojiwekea.
Jambo la msingi ni kila mmoja wetu kutoa ushirikiano kwa mamlaka hii wakati anapokutana na vituo vinavyouza mafuta bei ya juu tofauti na bei elekezi ili mamlaka hii iweze kufanya kazi yake.
Nimesema hivyo kwa kuwa EWURA ina watendaji ambao nao ni binadamu hawawezi kuota kila kinachofanyika katika maeneo yote ya nchi, ila sisi wananchi ambao ndio watumiaji wa huduma hizi tunatakiwa kutoa ushirikiano wa kutosha na si kulaumu kwa kila jambo.
Mbali na wananchi wa kawaida wanasiasa nao wanatakiwa kuipa ushirikiano mamlaka hii na si kujenga hoja za kuiboa kwa kuwa yapo mambo ambayo ni ya kiutendaji zaidi hivyo kama tutaingiza siasa katika suala hili itasababisha matatizo makubwa.
Ombi langu kwa EWURA ni kuendelea kukaza buti kwa kuvishikisha adabu vituo ambavyo vitaonekana vinakwenda kinyume na maagizo mnayoyatoa.

Mungu ibari Tanzania
0755-23-42-57