*Luhanjo aamuru aanze kazi leo
*Asema hakupatina na kosa lolote
Na Grace Michael
KATIBU Mkuu Kiongozi Bw. Phillemon Luhanjo ameamuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Bw. David Jairo kurejea mara moja kazini kwa kuwa uchunguzi uliofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) haujamkuta na hatia yoyote.
Bw. Jairo, ambaye alisimamishwa kazi Julai 21, mwaka huu ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizotolewa bungeni wakati wa kuwasilisha wa hotuba ya bajeti ya Wizara yake ambapo alidaiwa kuchangisha jumla ya sh. bilioni moja kuwahonga wabunge wapitishe bajeti ya wizara hiyo.
Akitoa uamuzi juu ya uchunguzi uliofanywa na CAG dhidi ya tuhuma hizo, Bw. Luhanjo alisema:
“Kutokana na matokeo haya ya uchunguzi wa awali ambao umefanywa kwa umakini mkubwa na kushindwa kuthibitisha tuhuma hizo, mimi kama Mamlaka ya nidhamu ya Katibu Mkuu wa Nishati na Madini David Jairo, sitaweza kuendelea na hatua ya pili ya kumpa taarifa ya tuhuma na hati ya mashtaka kwa kuwa Jairo hajapatikana na kosa lolote la kinidhamu,” alisema Bw. Luhanjo.
Kutokana na hatua hiyo, alisema kwa mujibu wa sheria namba 8 ya Utumishi wa Umma na kanuni zake anamwamuru Bw. Jairo kurejea kazini mara moja ambapo atatakiwa kuingia ofisini kwake leo.
Akifafanua matokeo ya uchunguzi wa tuhuma hizo, CAG Ludovick Otouh alianza kwa kueleza chimbuko la uchunguzi huo ambapo alisema ulitokana na wabunge waliohoji uhalali wa wizara kuomba michango kutoka kwenye taasisi kwa lengo la kushawishi baadhi ya wabunge kupitisha bajeti kirahisi.
Alisema kuwa ukaguzi huo ulifanyika kulingana na hadidu rejea zilizokuwa na lengo la kutafuta ukweli kuhusu tuhuma za michango na matumizi ya fedha zilizochangwa na wizara.
“Kazi hii ilihusisha kufanya mapitio ya nyaraka mbalimbali, vitabu vya risiti, hati
za malipo na taarifa za benki kwa kipindi cha mwezi Mei hadi Julai mwaka huu na timu ya wakaguzi iliwahoji watu kutoka taasisi zilizochangishwa, wizara, wabunge na wakala wa Jeolojia Tanzania," alisema CAG.
Alisema ukaguzi ulibaini kuwa idadi ya taasisi zilizopewa barua za kuchangia gharama za kuwasilisha bungeni bajeti ya wizara zilikuwa ni nne na sio 20 kama ilivyokuwa ikidaiwa na wabunge na utafiti huo ulibaini kuwa jumla ya fedha zilizochangwa ni sh. milioni 149.7.
Mbali na fedha hizo zilizochangwa na taasisi lakini pia ukaguzi huo ulibaini kuwa idara ya uhasibu ya wizara ilitoa sh. milioni 150.7 kwa ajili ya posho za vikao vya kazi katika uandaaji wa uwasilishwaji wa bajeti hiyo lakini pia Idara ya Mipango ya wizara nayo ilichanga sh. milioni 278 kwa ajili ya kazi hiyo.
Aidha CAG alifafanua kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) iligharamia chakula cha mchana cha sh. milioni 3.6 na tafrija iliyofanyika Julai 18, mwaka huu ambayo iligharimu sh. milioni 6.1.
“Jumla ya michango iliyochangwa ni sh. milioni 578.5 na sio bilioni moja kama ilivyotajwa kwenye tuhuma na taasisi zilizodaiwa kuhusika sio 20 kwa kuwa wizara hiyo ina taasisi zisizo zidi saba,” alisema Bw. Otouh.
Ukaguzi huo pia haukupata ushahidi wowote wa fedha zilizochangwa kutumika kuwalipa wabunge malipo yoyote kwa madhumuni ya kuwahonga bali malipo yaliyofanyika yalihusu posho za kujikimu, takrima na posho za vikao kwa maofisa walioshiriki katika kazi nzima ya uwasilishwaji wa bajeti.
Kwa mujibu wa taarifa za benki iliyotumika kukusanya fedha hizo hadi kufikia Julai 29, mwaka huu kiasi cha sh. milioni 20 kilikuwa ni fedha za matumizi ya fedha zilizochangwa na kupokelewa kwenye akaunti ya GST kabla ya kufanyika marejesho ya sh. milioni 99.4 na sh. milioni 14.8.
Kutokana na hali hiyo, CAG alisema kuwa jumla ya kiasi cha fedha kilichosalia kwenye akaunti hiyo kulingana na nyaraka za benki ni sh. milioni 195.2.
“Kwa kuwa ukaguzi maalum haukupata uthibitisho wa kuwepo taasisi 20 zilizotakiwa kuchanga bilioni moja kama ilivyodaiwa na wabunge, ukaguzi haukuthibitisha kuwepo kwa usahihi wa tuhuma zilizotolewa dhidi ya Bw. Jairo,” alihitimisha CAG.
Hata Hivyo waandishi wa habari walipohoji ni kwa nini vyombo vingine vya dola ikiwamo TAKUKURU na polisi havikuhusishwa kwenye uchunguzi huo, Bw. Luhanjo alisema kuwa suala hilo lilikuwa ni tatizo la kiutawala wa kifedha na sio rushwa wala kosa la jinai.
Alitumia mwanya huo, kuwaonya watumishi wa umma wanaojihusisha na uvujishaji wa siri na nyaraka za serikali kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria na kanuni za utumishi wa umma.
“Hata huyu aliyefanya hivi tukimpata naye atapata haki yake...ni kosa kubwa kuvujisha siri za serikali kwani usalama wa serikali ni wa mtumishi mwenyewe hivyo natoa onyo na iwe fundisho kwa watumishi wengine wenye tabia za kutoa siri za serikali,” alisema Bw. Luhanjo.
Hatua ya kusimamishwa kwa Bw. Jairo ili kupisha uchunguzi ilitokana na tuhuma zilizotolewa na wabunge wakati wa bajeti ya awali ya Wizara ya Nishati na Madini ambapo walidai kuwa Bw. Jairo amechangisha jumla ya sh. bilioni moja kutoka kwenye taasisi 20 zilizo chini ya wizara hiyo kwa lengo la kuwahonga wabunge kupitisha
bajeti hiyo.
No comments:
Post a Comment