Tuesday, June 21, 2011

Makinda: Niko tayari kuhojiwa na Kamati


Na Grace Michael, Dodoma

SPIKA wa Bunge, Bi. Anne Makinda amesema yuko tayari kuhojiwa na Kamati ya Kanuni za Kudumu za Bunge pindi atakapoitwa kutokana na malalamiko ya
Chama cha Demokrasia (CHADEMA) ya kutoridhishwa na uendeshaji wa mijadala ambao unalenga kuipendelea serikali.

Spika aliweka msimamo wake huo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa bunge, walipotaka kujua msimamo wake kuhusiana na uamuzi wa wabunge hao.

Alisema kuwa Bunge ni chombo kinachoendeshwa kwa mujibu wa kanuni hivyo kila jambo linalofanyika ndani ya bunge ni lazima lijikite kwenye kanuzi zilizopo.

“Niko tayari kuhojiwa, kwa kuwa nafahamu kuwa kila jambo linalofanyika ndani ya bunge linafuata kanuni na huo ndio utaratibu, hivyo mambo ya bungeni lazima yamalizikie bungeni,” alisema Spika Makinda.

Alisema kuwa endapo wabunge wa CHADEMA hawakuridhishwa na maamuzi aliyoyafanya wakati wa mjadala, walipaswa kuandika malalamiko na kuyafikishwa kwa Katibu wa Bunge kwa ajili ya hatua zingine zaidi za kuitisha Kamati za Bunge kwa ajili ya kujadili malalamiko hayo.

Alisema kuwa pamoja na yeye kuwa ndiye mwenyekiti wa kamati hiyo, lakini inapofika wakati wa kujadili malalamiko dhidi yake anapaswa kujiondoa na wajumbe watalazimika kuchagua mwenyekiti mwingine ambaye kwa mujibu wa kanuni atatakiwa kushinda kwa kura zaidi ya asilimia 50.

Kutokana na hali hiyo, Bi. Makindi alisema kuwa kinachofanywa na CHADEMA si sahihi kwa kuwa mambo ya bungeni hujadiliwa bungeni na si kwenye vyombo vya habari kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha kanuni za bunge.

Hata hivyo, Spika alisema kuwa hajaona barua yoyote iliyowasilishwa kwa Katibu wa Bunge lakini akasema yuko tayari kuhojiwa kwa hilo.

Akijibu madai ya CHADEMA yaliyotolewa na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Bw. Tundu Lissu kuwa Spika amekuwa akiibeba serikali na kuonea wapinzani, alikanusha na kusema kuwa hana hana tabia hiyo kwa kuwa akifanya hivyo atakuwa kinyume na anachotakiwa kufanya katika nafasi yake.

“Unapopewa mamlaka ya kuliongoza bunge ni lazima uwe na woga kwa Mungu kwa kuwa ukipendelea mtu mmoja na kumnyima haki mwingine utakuwa hutendi haki, hivyo madai ya upendeleo mimi siyakubali hata kidogo,” alisema Bi. Makinda.

Wabunge wa CHADEMA walilalamikia kitendo cha Spika kumzuia Waziri Mkuu kujibu maswali yao kwa madai kuwa wana kesi mahakamani.

Katika hilo, Bi. Makinda alisema kuwa asingeruhusu kujadiliwa kwa mambo waliyohoji kwa kuwa jambo likiwa mahakamani haliwezi kujadiliwa bungeni na ikifanyika hivyo itakuwa ni kuingilia mhimili mwingine.

Wiki iliyopita, wabunge wa CHADEMA Bw. Lissu (Singida Mashariki) na Ester Matiko (Viti Maalumu), walitaka ufafanuzi kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati wa maswali ya papo kwa papo kuhusu mauaji ya wananchi katika Mgodi wa Nort Mara yaliyofanyika hivi karibuni.

Kutokana na hali hiyo, Bw. Lissu aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kusema kambi yake imeamua kumshtaki Spika katika Kamati ya Kanuni za Kudumu za Bunge baada ya kutoridhishwa na utendaji wake, huku akifafanua kesi iliyopo mahakamani haina uhusiano na matukio ya mauaji ya raia katika mgodi wa North Mara.

Wakati Spika Makinda akisema hayo, Bi. Matiko amekanusha bungeni kuwa yeye hakabiliwi na kesi yoyote, hivyo akasema kuwa taarifa iliyotolewa na Spika wa Bunge pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Bw. William Lukuvi
ilipotosha umma.

Wabunge walia faini makosa ya barabarani

Na Grace Michael, Dodoma

MJADALA wa Bajeti ya Serikali jana uliendelea bungeni huku wabunge wakijikita kujadili vipaumbele vilivyoainishwa kwenye bajeti hiyo huku wakipinga baadhi ya
vyanzo vya mapato kama kuongezeka kwa faini za makosa barabara.

Suala la kuongezwa kwa faini za makosa barabarani lilionekana kuwagusa wabunge wengi ambao walisema kuwa serikali inatakiwa kuliangalia kwa makini kwa kuwa linalenga kuumiza wananchi badala ya kuwasaidia huku likiibia tatizo jingine la rushwa.

Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Njombe Kaskazini, Bw. Deo Sanga (CCM), alisema kuwa kupandisha faini hizo si njia sahihi ya kutatua tatizo la usalama barabarani bali itasababisha matatizo kwa wananchi na kuongeza mianya ya rushwa.

“Ni lazima hapa serikali iangalie kwa makini na ikibidi hata kujifunza nchi zingine kwani haiwezekani makosa yaanzie sh. 50,000 hadi 300,000 hapa tutawaumiza wananchi wetu na si kuwasaidia,” alisema Bw. Sanga.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Bi. Rose Kamili (CHADEMA) alipingana na hoja hiyo akisema kuwa endapo faini hiyo haitapunguzwa kutoka hapo ilipokadiriwa basi, serikali itakuwa imezalisha tatizo jingine la rushwa kwa kuwa hata hicho kiwango cha awali cha sh. 20,000 kilikuwa kikiwasumbua wananchi.

Kutokana na hali hiyo, wabunge walishauri kuondolewa kwa kiwango hicho kilichopendekezwa ili kibaki cha awali na kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinafuatwa.

Akichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Mtera, Bw. Livingstone Lusinde (CCM), alisema kuwa tatizo kubwa lililopo ni utekelezaji wa vipaumbele ambavyo vimekuwa vikiwekwa kwenye bajeti.

Alisema kutokana na kutosimamia vyema vipaumbele maeneo mengi hasa ya vijijini yamejikuta yakikosa huduma muhimu za kijamii kama maji, umeme, miundombinu, afya na zingine.

Akichambua vipaumbele hivyo kwa kuanza na miundombinu alisema kuwa kutokana na kushindwa kuweka vipaumbele katika maeneo mengine, Dar es Salaam imejikuta ikiwa na tatizo kubwa la msongamano wa magari barabarani kwa kuwa miundombinu iliyopo
sasa inashindwa kukidhi mahitaji.

“Nadhani kwa kutozingatia masuala mengi au kusahaulika kwa baadhi ya maeneo ndiko kunachangia hata serikali yetu kukwama kuhamia hapa Dodoma na ingekuwa vyema sasa Spika angeanza kuhamia hapa kwa kuwa hakuna kinachomfanya abaki Dar es Salaam wakati bunge liko Dodoma,” alisema Bw. Lusinde.

 “Viongozi kukaa Dar es Salaam kunawafanya washindwe hata kutekeleza majumu yao kwa kuwa muda mwingi wanautumia barabarani na wakifika ofisini tayari wanakuwa wamechoka na wanachokifanya ni kunywa chai na kusoma magazeti, na ndio maana kazi ya kutekeleza mipango ya serikali haifanikiwi,” alisema Bw. Lusinde.

Alisema kutokana na hali iliyopo, mambo mengi yamekuwa yakifanywa bila kuangalia athari zake ambapo alitolea mfano wa matangazo ya biashara ya pombe kwenye vyombo vya habari ambayo alisema yamekuwa yakilitesa taifa hivyo akataka matangazo ya aina kama hiyo yakataliwe.

“Mfano umekaa kwenye TV na uko na masheikh, maaskofu unaona linapita tangazo la Safari Lager urithi wetu. Hivi kama urithi wa nchi utakuwa pombe, hali ya nchi yenyewe itakuwaje na ndio maana wakati mwingine hata mijadala yetu inaendeshwa kama tumelewa,” alisema

Kwa upande wa Mbunge wa Ilemela, Bw. Highness Kiwia (CHADEMA), alisema kuwa pamoja na baba wa taifa kupambana na ukoloni lakini ukoloni huo kwa sasa umerejea kwa sura mpya ya ufisadi ambao Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere alisema ni adui mkuu wa maendeleo kuliko hata vita.

Akizungumzia umeme, alisema kuwa wananchi wa Ilemela wamechoshwa na nyimbo za Waziri wa Nishati na Madini ambazo kila ziku zinaelezea utekelezaji wa miradi yenye megawati kadhaa katika maeneo mbalimbali kupata umeme wenyewe

Wednesday, June 15, 2011

Wadau wasema rushwa kubwa bado tatizo

Na Grace Michael

WADAU wa kupambana na rushwa nchini wameitaka serikali kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) kuweka jitihada za dhati katika kupambana na watoa rushwa na wapokea rushwa wakubwa ambao ndio wana athari kubwa katika maendeleo.

Wamesema kuwa hawajarishwa na jitihada za kupambana na rushwa hasa kwa watoa rushwa wakubwa ambao ndio wanasababisha athari kubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi hii.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na wadau wa sekta mbalimbali wa kupambana na rushwa katika kongamano la mwaka la wadau wa kupambana na kuzuia rushwa nchini.

Akizungumzia hilo, Mwenyekiti wa Kampuni ya IPP, Bw. Reginald Mengi alisema kuwa eneo la watoa rushwa wakubwa halijashughulikiwa na nguvu kubwa imeelekezwa kwa wapokeaji.

Alisema kuwa nchi haitashinda vita dhidi ya rushwa bila ya kuwashughulikia watoa rushwa wakubwa hivyo kuna haja ya kuchukua maamuzi au hatua kali dhidi yao ili kukata mzungunguko huo haramu.

"Hawa watoa rushwa wakubwa wana nguvu kubwa ya kifedha na wana uwezo wa kuhakikisha wanakwamisha jitihada mbalimbali lakini ni lazima tufike mahali hatua kali zichukuliwe hata kama hazitawafurahisha baadhi ya watu," alisema Bw. Mengi.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Bw. Julius Mtatiro alisema kuwa mapambanao ya rushwa nchini yamekwama kwa kuwa nguvu kubwa imeelekezwa kwenye rushwa ndogo ndogo huku rushwa kubwa zikiachwa.

"Vigogo wanahusika na rushwa na hawachukuliwi hatua zozote na ndio maana hata huko mahakamani wanaofikishwa na waliohusika na rushwa ndogo ndogo tu na hatua zinashindikana kuchukuliwa kutokana na kuendekeza mambo ya kujuana na urafiki, hivyo hata nguvu ya kupambana ipasavyo inakwama," alisema Bw. Mtatiro.

Alisema kuwa bila ya viongozi wenyewe serikalini kujiweka katika mazingira safi hawataweza kupambana na vita hiyo, hivyo akasema kuwa kutokana na kutokuwa makini kwa serikali kunakwamisha upambanaji wa vita hiyo.

Alisema kuwa wao kama upinzani, watatimiza wajibu wao wa kuhamasisha wananchi kuichukia rushwa lakini pia wao wenyewe ndani ya chama kuhakikisha wanakuwa safi ili wawe mfano kwa jamii na waweze kusikilizwa na jamii.

"Kama wananchi wanakujua uchafu wako hawawezi kusikiliza unachokikemea hivyo kama huko wizarani ni kuchafu, mamilioni ya fedha kwenye halmashauri yanaibwa bila hatua kamwe jamii haiwezi kusikiliza suala hilo, hivyo ni vyema serikali ingeweka umakini katika kushughulikia suala hilo," alisema Bw. Mtatiro.

Akizungumzia madhara ya rushwa yanavyoathiri ukuaji wa uchumi na ufanyaji wa biashara, Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara Taifa (TNBC), Bw. Dan Mrutu alisema kuwa rushwa inachangia kwa kiasi kikubwa kupandisha gharama za kufanya biashara kwa kuwa mchakato wote uhitaji rushwa ili kufanikisha biashara.

"Mfano unataka kufanya biashara ambayo mtaji wake umepanga uwe milioni moja, unaweza ukatumia milioni tatu kwa kuwa kila mtumishi katika mnyororo huo anataka rushwa, kila utakapofika utakwamishwa, hivyo hadi unafanikiwa unakuwa umeingia gharama kubwa bila sababu ya msingi hivyo rushwa ni adui katika ukuaji wa uchumi," alisema.

Alisema kuwa endapo rushwa haitashughulikiwa ipasavyo itaathiri hata mpango wa kilimo kwanza kwa kuwa hata upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya kilimo nako itahitajika rushwa kwa ajili ya maofisa wanaoshughulikia ardhi, hivyo kuna kila haja ya kupambana na rushwa katika maeneo yote.

Akizungumzia tathimi ya kupambana na vita ya rushwa nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa TAKUKURU, Dkt. Edward Hosea alisema kuwa jitihada za serikali na wananchi zinazaa matunda kwa kuwa hata wadau wametambua kuwa kazi hiyo si ya TAKUKURU peke yake bali ni ya wadau wote.

Alisema kuwa wananchi kwa sasa wametambua madhara ya rushwa hatua inayowafanya hata kutoa ushirikiano katika mamlaka husika lakini pia hakusita kuvipongeza vyombo vya habari kwa kazi kubwa iliyofanyika katika kuibua mambo mbalimbali ya rushwa na kufanikisha kuchukuliwa hatua.

Alisema kuwa kama kuna malalamiko yoyote ya kutokuchukuliwa kwa hatua kwa baadhi ya watoa au wala rushwa ni vyema wenye ushahidi wakajitokeza ili TAKUKURU iweze kufanyia kazi kwa kuwa nchi inaongozwa kwa Utawala wa Sheria na si hisia.

Bw. Hosea alipobanwa na vyombo vya habari kuhusiana na wamiliki wa Kampuni ya Kagoda kutoshughulikiwa, alisema kuwa wao kama TAKUKURU hawaiogopi Kagoda wala mla rushwa yoyote na kutokana na hali hiyo akasisitiza kuwa mwananchi yoyote mwenye ushahidi auwasilishe.

"Unajua sisi tunachunguza na tunapomaliza kazi yetu tunapeleka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ambaye naye hutoa uamuzi kama mhusika apelekwe mahakamani au la, na hiyo inatokana na ushahidi uliopo na ndio maana alishawahi kuwaomba wenye ushahidi wauwasilishe hatuwezi kuwakamata watu bila kuwa na ushahidi," alisema Bw. Hosea.

Akifungua Kongamano hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, Bw. Mathias Chikawe, aliwataka viongozi katika maeneo yao ya kazi kusimamia utawala bora kwa kuhakikisha maadili ya kazi yanafuatwa lakini viongozi wa jamii wakiwemo wa dini na wanasiasa, aliwataka kukemea rushwa na vitendo vya ufisadi kila wanapopata nafasi ya kuzungumza na wananchi kwa maana ya wafuasi au wanachama wao.

Ahadi za JK kwenye kampeni za kusaka urais

1. Kujenga reli mpya kutoka Dar es Salaam mpaka mikoa ya Kanda ya ziwa-Nzega, Tabora
2. Mkoa wa Tanga kuwa Jiji la Viwanda- Tanga mjini
3. Tabora kutumia maji ya Ziwa Victoria-Igunga
4. Kulipa madeni ya chama cha Ushirika mkoa wa Shinyanga (SHIRECU)- Shinyanga
4. Kumaliza migogoro ya Ardhi nchini- Dodoma
5. Wakulima kuacha kutumia jembe la mkono-Dodoma mjini
6. Kuwapatia trekta wakulima -Kata ya Mrijo, Dodoma
7. Wananchi kutoondolewa kwenye Ranchi ya Misenyi-Kagera
8. Kujenga Uwanja wa Ndege Misenyi-Kagera
9. Kupanua Uwanja wa Ndege Bukoba-Bukoba Mjini
10. Kujenga uwanja wa ndege mkubwa Kigoma - Kigoma Mjini
11. Mtukula kupatiwa umeme kutoka Uganda- Kagera
12. Mikoa ya Kagera, Kigoma, Lindi, Rukwa na Ruvuma kuunganishwa katika gridi ya taifa ya umeme- Kagera
13. Kuimarisha Takukuru kwa miaka mitatu-Kagera
14. Hukumu kwa waliopatikana na hati ya kuua albino- Mbeya
15. Kununua meli kubwa kuliko MV Bukoba-Kagera
16. Kuanzisha benki ndogondogo kwa ajili ya wajasiriamali
17. Serikali kuvisaidia vyama vya ushirika-Mwanza
18. Kuimarisha usalama Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika kwa kupeleka kikosi maalum chenye vifaa kupambana na wahalifu-Mwanza
19. Wilaya ya Geita kuwa hadhi ya mkoa Januari mwakani- Geita
20. Kulinda muungano kwa nguvu zote-Pemba
21. Kuwajengea nyumba waathirika wa mafuriko Kilosa-Morogoro
22. Kununua meli mpya kubwa Ziwa Nyasa-Mbeya mjini
23. Kujenga bandari Kasanga –Rukwa
24. Kumaliza tatizo la walimu miaka mitano ijayo - Songea
25. Kufufua mgodi wa makaa ya mawe Kiwira -Mbeya
26. Kuzuia hatari ya kisiwa cha Pangani kuzama- Tanga
27. Kununua bajaji 400 kwa ajili ya kubeba wajawazito hasa vijijini- Iringa
28. Kujenga barabara yenye kiwango cha lami kutoka Same mpaka Kisiwani –Kihurio na kuiunganisha na barabara kuu ya Moshi -Dar es salaam- Same mkoani Kilimanjaro
29. Kumaliza tatizo la maji katika wilaya ya Same-Same Mjini
30. Kuboresha barabara za Igunga -Tabora
31. Kusambaza walimu 16,000 katika shule za sekondari zenye upungufu makubwa wa walimu- Kisesa Magu
32. Kununua vyandarua viwili kwa kila kaya- Mbeya Mjini
33. Kuzipandisha hadhi hospitali maalumu saba nchini kuwa za rufaa ili kuipunguzia mzigo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN)-Hydom Manyara
34. Kulinda amani nchini kwa kuzuia chokochoko za kidini, kikabila na kisiasa- Musoma
35. Kulinda haki za walemavu- Makete
36. Kujenga baabara ya Njombe- Makete kwa kiwango cha lami,urefu wa kilomita 109- Iringa mjini
37. Kujenga barabara Musoma–Mto wa Mbu Arusha-Arusha
38. Kuanzisha jimbo la Ulyankulu- Shinyanga Mjini
39. Kujenga barabara ya lami Manyoni-Kigoma– Kaliua,Tabora
40. Kukarabati barabara ya Arusha Moshi-Arusha Mjini
41. Kuboresha barabara ya Handeni, Kondoa,mpaka Singida-Dodoma
42. Kuwafidia wanakijiji ng’ombe waliopotea wakati wa ukame mwaka 2009- Longido 45.Vijiji vyote vilivyoko kilomita 15 kutoka kwenye bomba kuu la mradi mkuu wa maji wa Ziwa Victoria-Shinyanga-Kahama kuunganishiwa maji - Shinyanga
43. Tatizo la umeme kufikia kikomo Novemba mwaka huu mkoani Arusha –Arusha mjini
44. Kukopesha wavuvi zana za kilimo-Busekera, Wilaya ya Musoma, .
45. Kuwapatia maji wakazi wa Wilaya ya Longido- Longido
46. Kujenga barabara ya lami kupitia pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Seregenti – Ngorongoro
47. Utekelezaji wa mpango wa maendeleo ya kilimo kuwasaidia wafugaji kuweza kupata na kutunza mifugo yao vizuri- Mbulu mkoani Manyara
48. Kusambaza maji nchi nzima-Babati vijijini
49. Kusambaza umeme, utoaji wa huduma za afya, na uboreshaji wa kilimo cha umwagiliaji na utoaji ruzuku kwa wakulima. mwaka 2010-2015-Babati vijijini Kuongeza mara tatu idadi ya wananchi wanaonufaika na ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa mfumo wa vocha.-Iringa
50. Kuhakikisha Isimani inapata maji ya uhakika- Iringa
51. Kuiwekea lami barabara inayokwenda katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ambayo ndiyo hifadhi kubwa kuliko zote Tanzania-Iringa
52. Kulinda usalama wa wananchi kwa ujumla ili kudumisha amani na sifa ya nchi-Ifunda
53. kutokomeza malaria 2015-Bunda,mkoa wa Mara
54. kuwapa wanawake nafasi zaidi-Kilolo ,Iringa
55. ahadi kuisadia Zanzibar kuendeleza miradi mbalimbali ya kijamii-Kibandamaiti Mjini Zanzibar
56. Kuipandisha hadhi hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar kuwa ya rufaa-Kabandamaiti mjini Zanzibar
57. Kuisaidia Zanzibar kila panapohitajika msaada-Kibandamaiti
58. Serikali kujenga upya bandari ya Mbambabay-Ruvuma
59. Ununuzi wa Meli mpya yenye uwezo wa kubeba tani 400-Mbambabay Ruvuma
60. kufufua chama kikuu cha ushirika cha wakulima wa Mbinga(MBICU) –Ruvuma
61. Ahadi Rais wa Marekani Barack Obama kuimwagia misaada Tanzania –Ruvuma
62. Ahadi hakutakuwa na umwagaji wa damu baada ya uchaguzi-Dar es Salaam
63. Mtwara kuwa mji wa Viwanda –Mtwara
64. Ahadi ujenzi wa kwanda cha dawa ya kuua viluilui vya mbu-Kibaha
65. Hospitali ya Tumbi kuwa ya mkoa-Kibaha
66. Halmashauri ya manispaa ya Kibaha kutenga eneo maalumu la viwanda -Kibaha

Tuesday, June 14, 2011

Simba, Yanga 'zajazwa manoti'

 
Na Grace Michael

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) jana ilitekeleza moja ya masharti yake katika mkataba wa udhamini katika Klabu za Simba na Yanga kwa kuzipa jumla ya sh. milioni 40.

Klabu hizo zimejipatia fedha hizo, baada ya kupata ushindi ambapo Yanga ilitwaa ubingwa wakati Simba ilishika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Tanzania Bara iliyomalizika hivi karibuni.

Akikabidhi hundi hizo, Mkurugenzi wa Masoko wa TBL, David Minja alisema baada ya kumalizika kwa msimu wa 2010/2011 wa Ligi Kuu, TBL imeona itimize ahadi yake ya kutoa zawadi kwa mshindi wa kwanza na wa pili wa ligi wa hiyo.

"Yanga ambao ndiyo waliibuka mabingwa wanapata sh. milioni 25 na Simba waliochukua nafasi ya pili wanapata sh. milioni 15, ambazo ndizo zilikuwa ndani ya makubaliano yetu kwenye mkataba wa udhamini," alisema Minja.

Aidha TBL ilizishukuru timu zote zilizoshiriki michuano hiyo, viongozi na wanachama lakini pia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kuonesha ushirikiano wa hali na mali, tangu kuanza kwa ligi hiyo hadi mwisho.

"TBL inathamini kwa namna ya kipekee mchezo huu, unaopendwa na mamilioni ya Watanzania ambao si tu mchezo, bali pia ni ajira hivyo tutaendelea tena na tena kuwa wadhamini wa klabu hizi kongwe vyenye mashabiki wengi, ili waendelee kuipa heshima nchi yetu," alisema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa aliishukuru TBL kwa udhamini wake kupitia bia ya Kilimanjaro na akaweka wazi kuwa huo ndiyo udhamini wa maana katika ligi.

"Naomba niwe wazi kwa kusema kuwa muendelee kuwa wadhamini katika ligi zingine, ili klabu zingine nazo ziweze kufaidika na tunaahidi kuendelea kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ili hata udhamini wenu uwe na matunda," alisema.

Naye Katibu Mkuu wa klabu ya Simba Godfrey Nyange alisema kuwa wao kama Simba wanashukuru TBL kwa kutimiza matakwa ya mkataba hatua iliyowafanya wamevuna walichopanda, hivyo akaahidi kutumia fedha hizo kwa maendeleo ya klabu hiyo ili udhamini huo uwe na tija.

Wabunge tangulizeni maslahi ya waliowapa kazi




Na Grace Michael

WAKATI nchi ikikabiliwa na matatizo lukuki, wabunge wetu wapo mjini Dodoma kuhudhuria mkutano wa nne wa Bunge ambao kubwa zaidi utajadili na kupitisha bajeti ya 2011/2012 suala ambalo ni la msingi kwa nchi yetu.

Pamoja na kukabiliwa na jukumu hilo kubwa, lakini baadhi yao wametekwa na hoja ya kukatwa posho za vikao ambayo ilibuliwa na Waziri Kivuli wa Wizara ya Fedha na Uchumi Bw. Zitto Kabwe kwenye hotuba ya mwelekeo wa bajeti ya mwaka 2011/12.

Hoja hiyo imeibua malumbano makubwa kati ya abunge wanaotetea na wanaopinga hoja hiyo.

Kundi kubwa la wabunge hasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamekuwa mwiba katika hoja hiyo wakipinga kwa nguvu zote kuondolewa kwa posho hizo.

Wapo baadhi ya wabunge hasa wanaotoka kambi ya upinzani wao kwa pamoja wanaunga hoja hiyo kwa kutaka fedha hizo ziondolewe kwa kuwa hazina msingi wowote wa kulipwa.

Wabunge hao wa upinzani walikwenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa endapo posho hizo zitaondolewa, Serikali inaweza ikaokoa kiasi cha sh. bilioni 900 ambazo zikiwekewa mpango mzuri zinaweza zikasaidia katika kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.

Kila mpenda maendeleo atakubaliana na mimi kuwa asilimia kubwa ya wananchi hasa wanaoishi vijijini wanakabiliwa na kero nyingi hasa za ukosefu wa maji safi na salama, wanapoteza maisha kutokana na kutokuwepo kwa huduma za afya zilizoimarika lakini bado mama mjamzito anajifungulia njiani kutokana na ubovu wa miundombinu.

Watoto katika shule mbalimbali za serikali wanaketi chini kwa kukosa madawati, hawana vitabu na vyumba vya madarasa vilivyopo haviwatoshi lakini yote haya wabunge wetu hawayaoni.

Wamefikia mahali wabunge wetu wamejifanya hawana macho wala masikio, nasema hivyo kwa kuwa kero hizi zipo majimboni mwao na walizitumia kama daraja wakati wa kampeni, waliwaomba wananchi wawachague ili wasaidie katika kupigania maendeleo lakini la kuunguza posho zao limekuwa chungu.

Hoja hii itatusaidia kubaini viongozi ambao tuliwaweka madarakani bila kujua dhamira yao, kwa kupinga hoja hiyo ni ushahidi moja kwa moja kuwa wapo katika madaraka hayo kwa maslahi yao na si ya wananchi kama walivyotuongopea wakiwa majukwaani na wengine wakidiriki hata kutupigia magoti.

Posho za vikao ambazo zinaombwa zikatwe ni zile ambazo mhusika hulipwa huku akiwa tayari na posho ya kujikimu katika eneo husika hivyo kwa kupokea posho nyingine ya kikao ni sawa na kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu kwa kuwa kazi unayoifanya hapo ipo ndani ya majukumu yako ya kikazi.

Suala hili linaonekana kubezwa na wengi lakini yawezekana  wanafanya hivyo kwa kuwa nao ni sehemu ya watu walioingia bungeni kwa ajili ya kuvuna kilichopo na kisha kuwaacha wananchi wakiwa watupu.

Hoja zijadiliwe kwa hoja na sio kubeza hoja iliyotolewa na hasa hoja ambazo zina lengo la kupunguza mzigo wa matumizi kwa serikali hivyo isifike mahala hoja hii ikabezwa na kuchukuliwa kama ni ya kisiasa ili iondolewe kwenye mstari.

Ni lazima kila mmoja wetu atambue namna nchi ilivyo na mzigo mkubwa, imeshindwa hata kuimarisha huduma za kijamii kutokana na ufinyu wa bajeti, maisha bora kwa kila mtanzania yamekwama kutokana na mizigo ya matumizi kama hiyo ya posho hivyo kuna kila haja ya wabunge sasa kuketi na kuliangalia suala hili kwa kina ili kuona namna linavyoweza kushughulikiwa.

Ipo hoja iliyoelezwa kuwa posho hizo haziwezi kuondolewa kwa kuwa zipo kwa mujibu wa sheria, inashangaza kusikia maneno hayo huku watunga sheria wakiwa hao hao hivyo ni vyema wangesema kuwa wako tayari kuangalia uwezekano wa kutengua kifungu hicho cha posho ili fedha hizo sasa zielekezwe katika matumizi mengine.

Wabunge wetu wamekuwa wakali kweli kweli kwenye maslahi yao kuliko hata wanavyoweza kutetea hoja zingine ambazo zinawagusa moja kwa moja wananchi hivyo ni vyema ukali huo mkautumia katika kutetea maslahi ya wananchi zaidi ili hatimaye tuondokane na kero zilizopo kwa sasa.

Mungu inariki Tanzania

0755-23-42-57





Sunday, June 12, 2011

DC Mafia aipiga jeki CHF


Mkuu wa Wilaya ya Mafia Manzie Mangochie amezindua kampeni ya uchangiaji wa mfuko wa afya ya jamii CHF kisiwani hapo  kwa kuchangia kaya 100 zisizo na uwezo mapema wiki hii.

Harambee hiyo ilifanyika katika Bwalo la Magereza iliambatana na  uzinduzi wa Bodi ya Afya ya Halmashauri pamoja na azimio la kusitisha huduma za matibabu kisiwani humo kesho kutwa Juni 15, 2011. Jumla ya shilingi milioni moja zilichangwa na wadau mbalimbali waliohudhuria.

Akizungumza kwa njia ya simu na Majira Meneja Kiongozi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) tawi la Pwani Bibi .Rose Ongara amesema uzinduzi wa Bodi ya Afya unaifanya Halmashauri ya Mafia kuungana na Halmashauri nyingine 100 katika huduma za CHF ambazo sasa zinasimamiwa na Ofisi yake.

"Uhamasishaji uliofanywa na mkuu wa wilaya hiyo yenye wakazi takribani 48,000 na Kaya zipatazo 9,875 umefungua milango kwa wananchi kupata matibabu kwa mwaka mzima kwa Kaya kwa kuchangia shilingi 5,000 tu kwa mwaka," Alisema Bi. Ongara.

Mambo mengine yaliyojadiliwa na kuazimiwa katika kikao hicho ni pamoja na kufuta huduma za matibabu ya bure ambayo yalikuwa yakitolewa katika kisiwa hapo na kubainisha viwango vitakavyoanza kutozwa kuwa ni  shilingi 500 kwa zahanati na shilingi 800 kwa Hospitali kila mara mgonjwa atakapokuwa anataka huduma hizo. Hata hivyo utaratibu huu hautawahusu wanachama wa CHF ambao wao watakuwa wanachangia mara moja tu mwaka.

Katika Hafla hiyo iliyohudhuriwa na Wawakilishi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Kanda ya Pwani Bodi ya Afya ya Halmashauri ya Mafaia ilimchagua Bw Abdul Rajab Manda kuwa mwenyekiti wake kwa kipindi cha miaka 3 kuanzia Mei, 2011
.
Naye Msimamizi wa huduma za CHF kitaifa Bw Rehani Athumani amewashukuru wadau wote wanaojitokeza kuhamasisha huduma za CHF hasa Wakuu wa Wilaya na mashirika mbalimbali ya Umma ambao katika siku za karibuni wameongeza kasi ya kuunga mkono CHF.Hadi kufikia tarehe 31 Mei, 2011 Rehani amesema Mfuko wa Afya ya Jamii ulikuwa na wanachama wachangiaji katika Kaya zaidi ya 457,000 na wanufaika milioni 2.7 nchi nzima.

Thursday, June 9, 2011

Serikali yaongeza kipaumbele cha ajira kwa vijana

Na Grace Michael

KATIKA kuhakikisha serikali inagusa kila kero iliyopo nchini, bajeti ya mwaka wa fedha wa 2011/2012 imeibuka na kipaumbele kipya cha kukuza ajira ambacho hakikuwemo katika vipaumbele vya miaka mitatu iliyopita.

Vipaumbele ambavyo serikali imekuwa ikivipa kipaumbele kwa kuvitengea mabilioni ya shilingi ni pamoja na elimu, miundombinu, afya, kilimo, nishati na maji.

Akiwasilisha bungeni jana mjini Dodoma bajeti ya serikali ya 2011/12, Waziri wa Fedha, Bw. Mustapha Mkulo alivitaja vipaumbele vilivyomo kwenye bajeti hiyo kuwa ni pamoja na Umeme, Maji, kilimo, kupanua ajira na miundombinu kwa maana ya  reli, barabara, bandari, viwanja vya ndege na vingine.

Bw. Mkulo akizungumzia kipaumbele cha ajira alikiri kuwa imekuwa ni changamoto kubwa kwa serikali lakini akaanisha mipango mbalimbali iliyowekwa na serikali kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hilo.

Alisema kuwa Mpango wa Ukanda wa Kilimo ni moja ya mpango ambao utasaidia katika kupunguza umasikini wa wananchi lakini pia utasaidia katika kuongeza ajira.

“Kuimarishwa kwa kilimo cha mazao, viwanda vya kusindika, kuwezesha wajasiliamali wadogo na wa kati, kuweka mazingira mazuri hasa ya upatikanaji wa mikopo pamoja na mafunzo kwa wajasiliamali vitasaidia katika kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira nchini,” alisema Bw. Mkulo.

Bw. Mkulo, alisema  Miundombinu serikali imetenga sh. Trilioni 3.7 kwa ajili ya  barabara, bandari, reli, mkongo wa Taifa na viwanja vya ndege.

Alisema sekta ya nishati imetengewa sh. bilioni 539.3, maji sh. bilioni 621.6, kilimo sh. bilioni 926, elimu ikitengewa sh. trilioni 2.2 huku afya ikiwa na sh. trilioni 1.2.

Vipaumbele ambavyo vimekuwa katika bajeti za miaka mitatu iliyopita kwa maana ya 2008/09, 2009/010, 2010/011 ni pamoja na Elimu, Miundombinu, Afya, Kilimo, maji na Nishati na Madini.

Pamoja na kutoa vipaumbele vingi namna hiyo, serikali bado imeshindwa kuleta mabadiliko ya dhati hata katika baadhi ya vipaumbele hivyo hatua inayowafanya wananchi kuishauri kutoa vipaumbele vichache ambavyo itavisimamia kwa dhati na hatimaye kuonesha mabadiliko.

Kwa mujibu wa bajeti ya mwaka 2008/2009 elimu ilitengewa sh. trilioni 1.2 sawa na asilimia 17 ya bajeti yote, 

Alisema kuwa 2009/2010 elimu ilitengewa sh. bilioni 1743.9 huku 2010/2011 ikitengewa sh. trilioni 2.

Kipaumbele cha mindombinu ambayo ndio imekuwa ni kero kubwa katika maeneo mbalimbali ya nchi mwaka 2008/09 ilikuwa na sh. bilioni 971.9, 2009/10 sh. bilioni 1,096.6 huku mwaka 2010/11 ikipewa sh. bilioni 1,505.1.

Alisema kuwa kilimo kilitengewa sh bilioni 481, 2008/09 na 2009/10, sh. bilioni 666.9, 2010/11 imetengewa sh. bilioni 903.8.

Alisema kuwa Sekta ya Afya kwa 2008/09 ilitengewa sh. bilioni 784.5, 2009/10 sh. bilioni 963 na 2010/11 sh. bilioni 1,205.9.

Sekta ya Nishati, 2008/09 ilitengewa sh. bilioni 382,na 2009/2010 sh. bilioni 285.5.

Alisema kuwa 2010/2011 imetengewa sh. bilioni 327.2  huku sekta ya maji ikipewa sh. bilioni 217 2008/09, sh. bilioni 347.3 2009/10 na sh. bilioni 397.6 kwa 2010/2011.

Tuesday, June 7, 2011

Askari wamejipanga kudhibiti wafuasi wa CHADEMA

Askari wakiwa kazini siku aliyokamatwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa ajili ya kudhibiti ghasia.

Vijana CHADEMA wakionesha alama ya vidole viwili

Vijana wakishinikiza kuachiwa kwa Kiongozi wa Kambi  ya Upinzani Bungeni Freeman Mbowe mwishoni mwa wiki iliyopita.

Ikulu: Viongozi wa dini si malaika

Na Grace Michael

SIKU moja baada ya viongozi wa dini kumpa saa 48 Rais Jakaya Kikwete kuwataja kwa majina ya baadhi yao wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, Ikulu imeshindwa kutaja majina hayo, badala yake ikasema kauli hiyo haikutarajiwa kutoka kwa viongozi hao kwa kuwa nao si malaika ama watakatifu hapa duniani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu jana na kusainiwa na Mwandishi Msaidizi wa Rais, Bi. Premy Kibanga, kauli ya viongozi hao wa dini ni ya kusikitisha na haikutarajiwa kutoka kwao.

“Viongozi wa dini ni watu wa kutumainiwa sana katika jamii yeyote, lakini ikizingatiwa kuwa wao sio malaika ama watakatifu hapa duniani, nao wanatumbukia katika majaribu na kujikuta katika vitendo au hali isiyo tegemewa kabisa,” ilisema taarifa hiyo.

Badala ya kutaja majina ya wauza 'unga', taarifa hiyo ilieleza kuwa hivi karibuni wapo viongozi wa dini waliokamatwa kwa rushwa, ngono na kutuhumiwa kujihusisha na vitendo mbalimbali ambavyo ni kinyume na maadili ya jamii na wapo ambao wamekamatwa na watafikishwa kwenye vyombo vya sheria, lakini wapo wanaochunguzwa hivyo kutokana na hayo viongozi hao hawakutakiwa kujitetea kwa kauli nyepesi kwa kumpa Rais saa 48."

Ilisisitiza kuwa kiongozi anayejishuku ajisalimishe mwenyewe na anayeshukiwa na jamii afichuliwe ili afanyiwe uchunguzi na hatimaye sheria ichukue mkondo wake, lakini si kusubiri Rais awataje hadharani ndiyo viongozi hao waanze kuchukua hatua.

Vyombo vya habari jana viliwakariri baadhi ya viongozi wa dini wakimpa Rais Kikwete muda wa saa 48 kuwataja viongozi aliowatuhumu kwa ujumla kuwa wanajihusisha na biashara hiyo haramu.

Taarifa hiyo ilifafanua mambo aliyoyazungumza Rais Kikwete kwenye sherehe ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu John Ndimbo wa Jimbo la Mbinga ambapo Rais Kikwete alitoa ombi la kuwataka viongozi hao kujihusisha kikamilifu katika mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya.

“Ni tatizo linalozidi kukua pamoja na jitihada za Serikali kupitia vyombo vya usalama kuwabana, kuwawajibisha watumiaji na wafanyabiashara ya dawa za kulevya. Athari zake kwa jamii zinaeleweka, hivyo sihitaji kuzirudia...

“Kila siku kuna watu wanaokamatwa kwa kujihusisha na dawa za kulevya na hiyo inaashiria kuimarika kwa vyombo vyetu vya usalama, lakini inasikitisha sana kuona kuwa biashara hiyo sasa inawavutia hata watumishi wa Mungu.

"Huku sasa tunakoelekea kwa kweli ni kubaya sana.  Nawaomba mtoe uzito unaostahili kwa tatizo hili. Viongozi wa dini mnasikilizwa, Nawaomba kemeeni, onyeni na elimisheni jamii juu ya madhara ya dawa za kulevya, waelimisheni vijana ambao ndiyo walengwa wakuu, waepuke na waache kujihusisha na biashara na matumizi ya dawa za kulevya,” alisema.

Taarifa hiyo iliongeza: “Mtu akikuonya kuwa nyumbani kwako kumeonekana nyoka, huanzi kwa kuuliza kama kweli,  ni wa rangi gani?  Unatakiwa kushtuka na kujiandaa kumsaka kwa nia ya kumwondoa nyumbani kwako hata ikibidi umuue ili asije akaleta madhara makubwa kwako na kwa familia yako, hivyo Rais alikuwa na nia njema katika kulielezea jambo hili, na mwenye nia njema haumbuki,” ilisema taarifa hiyo.

Pia viongozi hao walitakiwa kuweka mikakati na vipaumbele vya kufanyia kazi changamoto hiyo na sio kuahirisha tatizo hili ambalo linazidi kuwa kubwa na kazi ya kupambana na dawa za kulevya haimhusu Rais peke yake bali inamhusu kila Mtanzania.

Sunday, June 5, 2011

Kamati Miundombinu yasisitiza kukwamisha bajeti ya Uchukuzi

Na Grace Michael

HATIMAYE Kamati ya Bunge ya Miundombinu imepitisha bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia huku ikiendelea na msimamo wake wa kutopitisha bajeti ya Wizara ya Uchukuzi endapo Serikali haitatenga fedha za reli,Shirika la Ndege Tanzania (ATC) na Wakala wa Meli.

Hatua hiyo iliwekwa rasmi Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw. Peter Serukamba ambaye alisema kuwa kamati yake haitakuwa tayari kupitisha bajeti hiyo bila kuwepo kwa fedha hizo.

"Tuna sababu zetu, tunataka fedha za reli, ATC na wakala wa meli, wapo watu wanasema kuwa fedha za reli zipo lakini kwenye vitabu hazipo, hakuna mpango wa serikali ambao fedha zake ziko mdomoni hivyo hatutakubali mpaka tuone fedha hizo ndani ya vitabu," alisema Bw. Serukamba.

Alisema kuwa Serikali inaweza ikapunguza matumizi ambayo si ya lazima katika wizara mbalimbali ili fedha hizo zikatumike katika masuala hayo ambayo ni ya muhimu kwa nchi na wananchi wa Tanzania.

Alitolea mfano wa Wizara ya fedha ambayo imetengewa mabilioni ya fedha katika matumizi ya kawaida huku mambo ya msingi kama reli inayotegemewa na wananchi wengi ikiachwa bila fedha zozote.
"Hatuwezi kuendelea huku tukiendekeza starehe na hata nyumbani kwako ukitaka kuendelea ni lazima upunguze starehe hivyo watu wa kawaida hawatatuelewa kutoweka fedha za kukarabati reli usafiri ambao ni tegemeo kubwa kwa wananchi wengi wa Tanzania.

Alisema kuwa nia ya Kamati ni njema kwa kuwa hata gharama za bidhaa zinapanda kutokana na gharama kubwa ya usafirishaji gharama ambayo ingepungua endapo kungekuwa na usafiri wa uhakika wa reli.

"ATC inahitaji bilioni 23 zikiwemo bilioni mbili za kulipia gharama za ndege zilizokwenda kwenye matengenezo...kama serikali imeshindwa kufanya hivyo basi itangaze imefunga shirika hilo ili wafanyakazi wake warejee majumbani kwani huwezi ukatenga fedha za kulipa wafanyakazi huku hakuna kazi wanayoifanya," alisema Bw. Serukamba.

Alisema kuwa hawatakubali ndege mbili za ATC zifie Afrika Kusini zilikokwenda kwa ajili ya matengenezo hivyo akasisitiza kutengwa kwa fedha hizo kwa ajili ya kulikwamua shirika hilo. Alisema kuwa yapo maeneo kwenye bajeti za wizara ambayo yametengewa fedha za matumizi ya kawaida  maeneo ambayo yanaweza zikapunguzwa na fedha kwa ajili reli, ATC na wakala wa meli zitapatikana.

Akizungumzia bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Bw. Serukamba alisema kuwa Kamati imemwagiza Waziri mwenye dhamana Bw. John Magufuli kuhakikisha anasimamia sheria za nchi ili sekta hiyo iweze kufanikiwa hasa katika ujenzi wa barabara ambao umewekewa mkazo mkubwa katika bajeti hiyo.

Alisema kuwa wizara hiyo imeweka mipango mizuri ambayo imekubalika na kamati hiyo ikiwemo mipango ya ujenzi wa nyumba za Serikali, ujenzi wa barababa madaraja yakiwemo ya Kigamboni, Malagarasi na Kilombero. Alisema kuwa jambo linalotakiwa kufanywa na wizara hiyo ni kuhakikisha inasimamia sheria ili utekelezaji wa waliyoyapanga yaweze kufanyika.

Chadema wapinga kumkamata Mbowe

*Wasema amri hiyo inakiuka sheria
*Wadai Jeshi la polisi lina ubaguzi


Na Grace Michael

KAMBI rasmi ya Upinzani Bungeni imeshtushwa na amri iliyotolewa na Mahakama ya Arusha ya kumkamata kiongozi wa kambi hiyo, Bw. Freeman Mbowe kwa kuwa inakiuka sheria, mila na desturi zinazohusu kinga, haki na mamlaka ya Bunge na ambazo ndio msingi mkuu wa demokrasia ya kibunge.

Mbali na kushtushwa lakini pia imedai kuwa imeshangazwa na unafiki pamoja na ubaguzi wa wazi unaooneshwa na Jeshi la Polisi juu ya Wabunge wa vyama vya upinzani kwa kuwakamata bila ya kuomba kibali kwa Spika wa Bunge kama inavyofanyika kwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi.

Kutokana na hatua hiyo, Bw. Mbowe ameweka wazi msimamo wake kwa kusema kuwa yuko tayari kusimamia haki za kambi hiyo kwa gharama yoyote huku akitumia msemo usemao "Bora kufa umesimama kuliko kuishi umepiga magoti'.

Hatua hiyo ilifikiwa Dar es Salaam jana ambapo Bw. Mbowe kwa kushirikiana na viongozi wengine wa kambi ya upinzani kueleza kilichotokea mahakamani na namna walivyokubaliana na mahakama huku wakieleza haki na kinga walizonazo.

Bw. Mbowe alisema kuwa kitendo kinachofanywa na Mahakama hiyo anaweza akakihusisha na njama ya kuwatoa wabunge hao kwenye kupigania agenda za muhimu kwa Watanzania hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Bunge la Bajeti, kipindi kinachotaka utulivu na amani ili wabunge wapate fursa ya kufikiri kwa kina na kwa umakini.

"Nadhani mambo haya yanafanyika kwa makusudi kabisa ili watuondoe kwenye hoja za msingi...mahakamani tulikubaliana kimsingi kuwa hatutahudhuria siku ya kesi kwa kuwa tunaanza vikao vya kamati na vikao vya bunge...nikiwa kama kiongozi wa upinzani nina serikali yangu kivuli ambayo inahitaji uongozi wangu hivyo isingekuwa rahisi kwenda Arusha," alisema Bw. Mbowe.

Pamoja na kusema hayo, alisema kuwa kambi hiyo haijawahi kudharau mamlaka ya Mahakama na wala haitegemei kufanya hivyo lakini akasisitiza kuzingatiwa kwa haki za msingi zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.

Akizunguzma amri iliyotolewa na mahakama, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bw. Tundu Lissu, alisema kuwa ibara ya 100 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatambua na kulinda “uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge na uhuru huo hauwezi kuvunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katika Mahakama au mahali penginepo nje ya Bunge.

Bw. Lissu alikwenda mbali zaidi kwa kueleza maeneo ambayo mbunge ana kinga nayo ni ukumbi ambao hutumiwa kwa vikao vya Bunge, pamoja na ofisi, vyumba, vibambaza, maeneo ya wageni, bustani na maeneo mengine yaliyowekwa kwa ajili ya matumizi au malazi ya wajumbe, maofisa au wageni wa Bunge pamoja na njia zinazounganisha maeneo hayo na maeneo yanayoweza kutangazwa na Spika hivyo akasema kuwa hata akiwa ndani ya gari la Kambi ya upinzani anakuwa na kinga.


Alisema kuwa wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Arusha inatoa amri dhidi ya Bw. Mbowe alikuwa analindwa na kinga ya Bunge na kinga hiyo itaendelea kwa kipindi chote cha Mkutano wa Nne wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Akizungumzia unafiki na ubaguzi wa Jeshi la Polisi, Bw. Lissu alisema kuwa wabunge wa vyama vya upinzani wamekuwa wakikamatwa bila ya kuwepo kwa kibali chochote cha Spika kama inavyotakiwa na Sheria ya Kinga, Mamlaka na Haki za Bunge.

Aliwataja wabunge ambao wamekamatwa na polisi bila kibali ni Bw. Mbowe, Bw. Godbless Lema (Arusha Mjini), Bw. Phillemon Ndesamburo (Moshi Mjini), Bw. Joseph Selasini (Rombo), Bw. Meshack Opulukwa (Meatu), Bw. Tundu Lissu (Singida Mashariki), Bi. Esther Matiko (Viti Maalum, CHADEMA) na Bi. Magdalena Sakaya (Viti Maalum, CUF).

Alisema kuwa wabunge wa CCM na ambao wanakabiliwa na tuhuma za makosa makubwa zaidi wamekuwa wakiombewa kibali cha Spika kabla ya kukamatwa na katika hilo walisema wanao ushahidi wa barua ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Mwanza SP B.M. Wakulyamba kwa Katibu wa Bunge ya kumwomba Bw.Titus Mlengeya Kamani (Busega, CCM) kwa ajili kuhojiwa na Jeshi la Polisi kuhusu madai ya kuhusika kwake na njama za kutaka kumwuua aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Busega Dkt. Raphael Chegeni.

Alisema kuwa hatua hiyo inadhirihisha upendeleo wa wazi wa Jeshi la Polisi kwa Wabunge wa CCM na kwa sababu hizo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haitarajii, na itapinga kwa nguvu zote kitendo chochote cha kumtishia au kumkamata Kiongozi wa kambi hiyo kwa kipindi chote ambacho ana kinga ya Bunge kama inavyotambuliwa na Katiba na sheria.

Kambi hiyo imesema inatarajia kuwasilisha barua ya malalamiko katika Ofisi ya Katibu wa Bunge ili haki iweze kutendeka kwa wabunge wote na kuondoa ubaguzi uliopo.

Thursday, June 2, 2011

Kamati yawatimua Kariakoo, NARCO kwa ubabaishaji

Na Grace Michael

KAMATI ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) jana ililazimika kuyatimua mbele yake Shirika la Masoko Kariakoo na Ranchi ya Taifa (NARCO) baada ya kubaini ubabaishaji katika uendeshaji wake.

Shirika la Masoko Kariakoo ndilo lilikuwa la kwanza kutimuliwa kutokana na bodi iliyofika mbele ya kamati hiyo kuwepo kwenye nafasi hizo za uongozi kinyume cha sheria.

Baada ya uongozi huo kujitambulisha mbele ya kamati, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Zitto Kabwe alianza kumhoji Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo, Bw. Bakari Kingobi kama yupo kihalali au kwa mujibu wa sheria katika nafasi hiyo.

Bw. Kingobi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji, aliyeonekana kutambua wazi kuwa yupo isivyo halali, alikiri kuwa mpaka sasa anashika nafasi hiyo kinyume na sheria na akaweka wazi kuwa tayari ameandika Barua TAMISEMI akikumbusha umuhimu wa kuteuliwa kwa bodi mpya baada ya bodi hiyo kumaliza muda wake.

Suala jingine ambalo liliibuliwa ni namna Mwenyekiti huyo alivyoteuliwa kinyume cha sheria ambapo aliteuliwa na TAMISEMI badala ya kuteuliwa na Rais kama sheria inavyotaka.

Pamoja na wajumbe wa kamati hiyo kuhoji mambo mbalimbali yanayohusiana na upotevu wa mali za shirika hilo zikiwemo nyumba, viwanja na mali zingine lakini Bw. Zitto alilazimika kusitisha maswali na hayo na kuamua kuwatimua viongozi hao kwa kuwa hawakuwa halali mbele ya kamati hiyo.

"Nimepata ushauri wa kikanuni hapa, tumebaini kuwa watu tulionao mbele yetu si ambao tunawahitaji na tukiendelea kuwahoji na sisi tutavunja sheria, hivyo waondoke na kamati itawasiliana na TAMISEMI ili mchakato wa uteuzi wa bodi mpya ufanyike haraka," alisema Bw. Zitto na kuongeza;

"Kuna madudu mengi kwa kuwa uongozi wa shirika umezidiwa nguvu na wafanyabiashara, imefika mahali nyumba na hata viwanja vinachukuliwa tu na watu na kupotea bila sababu ya msingi, hivyo tutahakikisha tunalifanyia kazi suala hili," alisema.

Mbali na hilo, Bw. Zitto pia alisema kuwa kamati itaomba ripoti ya ukaguzi iliyofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) baada ya kuagizwa na Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda ili kujadiliwa.

Kwa upande wa NARCO walijikuta wakifukuzwa baada ya kushindwa kuieleza kamati idadi ya ng'ombe waliopotea na waliokufa.

Wajumbe wa Kamati walihoji kuongezeka kwa takwimu za ng'ombe wanaokufa na kupotea katika ranchi mbalimbali, hatua iliyowafanya waombe ufafanuzi zaidi kutoka kwa viongozi hao.

Akijibu hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya NARCO, Bw. Salum Shamte, alisema kuwa kwa wakati huo hawakuwa na idadi sahihi lakini akatoa idadi ya ng'ombe 55 walioibwa katika ranchi ya Kongwa.

Alisema kuwa wizi uliofanyika Kongwa walibaini kuhusika kwa meneja wa ranchi hiyo ambapo walimchulia hatua ya kumwachisha kazi.

Akihoji hatua hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Bi. Ester Bulaya, alishangazwa na hatua ya kumwachisha kazi peke yake bila ya kumfikisha mbele ya vyombo vya sheria ili hatua zaidi zichuliwe.

"Kwa nini huyu mtu aishie kufukuzwa kazi tu...? Haiwezekani, ni lazima hatua zaidi zichukuliwe kwani suala hilo mmelifuatilia kwa muda gani ili kujua polisi wamefikia wapi? alihoji Bi. Bulaya.

Hata hivyo Bw. Zitto aliagiza uongozi huo kuandika barua polisi ili kujua uchunguzi wa suala hilo umefikia wapi na majibu hayo yafikishwe mbele ya kamati kwa ufuatiliaji zaidi.

Bw. Zitto alisema kuwa anapata mashaka na idadi kubwa ya upotevu na vifo vya ng'ombe hivyo akautaka uongozi huo kuondoka ili ujiandae na takwimu zitakazoonesha idadi halisi ya ngombe waliokufa na kupotea.

"Haiwezekani idadi hiyo itoke asilimia 10 na kufikia asilimia 30, hii inaonesha kuna njama fulani hatutakubali...maeneo mengine mmefanya vizuri lakini hili hapana, kajipangeni upya," alisema Bw. Zitto.

Wednesday, June 1, 2011

POAC yaamuru TICTS kufikishwa Kamati ya Maadili

Na Grace Michael

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) imeagiza Kitengo kinachohudumia Makontena Bandarini (TICTS), kufikishwa mbele ya Kamati ya maadili kutokana na kudharau mamlaka ya Rais Jakaya Kikwete na kamati hiyo.

Agizo hilo lilitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Zitto Kabwe baada ya kupata maelezo kutoka TPA ya namna kitengo hicho kilivyogoma kulipa deni linalodaiwa na TPA.

"Tumemwagiza Katibu wa Katibu wa Kamati yetu aandae mchakato wa kuifikisha TICS mbele ya kamati ya maadili ili ikajieleze ni kwa nini inadharau mamlaka ya Rais...TPA wamelalamikia kitendo cha kutolipwa fedha zao ambazo zilikuwa ni gaharama za kupunguza msongamano wa makontena bandarini baada ya kitengo hicho kuzidiwa nguvu," alisema Bw. Zitto.

Alisema kuwa hatua hiyo wameifikia baada ya TICS kuandika barua TPA ikigoma kulipa deni la Dola za Marekani laki 261 ambazo zilikuwa ni gharama za uhamishaji makontena hayo.

Katika taarifa iliyotolewa mbele ya kamati hiyo, ilieleza kuwa Oktoba 18, mwaka jana, TPA iliandika barua kwa TICS ikikumbusha deni hilo lakini katika majibu ya TICS hawakuwa tayari kulipa fedha hizo kwa madai kuwa hawakuwa na mkataba wa kufanya hivyo.

Kutokana na hali hiyo, kamati hiyo iliagiza kufanyika hivyo kwa kuwa TICS wameonesha dharau kwa Rais ambaye aliagiza fedha hizo zilipwe lakini pia wameidharau kamati hiyo.

Hata hivyo kamati hiyo ilishindwa kupitisha hesabu za TPA kutokana na kuwepo kwa mapungufu ya hapa na pale hasa utata wa kiasi cha fedha kinachotakiwa kulipwa na TICS kwa TPA katika shughuli zake mbalimbali ikiwemo pango.

Suala jingine ambalo liliagizwa na kamati hiyo ni kuhakikisha Bodi ya TPA inapitisha mfumo wa matumizi ya sheria ya manunuzi ili manunuzi yote yanayofanyika yafanywe kupitia sheria hiyo.

Bw. Zitto alisema kuwa kamati hiyo imebaini kuwa yapo manunuzi yaliyofanywa na TPA kinyume cha sheria hiyo ya manunuzi na mengine hayakuidhinishwa na Bodi hivyo wakaagizwa kuyafanyia kazi masuala hayo.

"Kamati pia imeagiza TPA wafanye mkutano na uongozi wa Mkoa wa Mtwara kwa lengo la kuwaelezea namna walivyozipangisha kampuni tatu katika eneo la bandari na kuondoa uvumi wa kuwa bandari hiyo imeuzwa lakini pia kamati itatembelea bandari zote kwa lengo la kukagua na kujirisha na maelezo wanayoelezwa," alisema Bw. Zitto.

Bw. Zitto pia alitumia mwanya huo kusisitiza umuhimu wa TPA kuhakikisha wanajipanga vyema ili kuongeza mapato yao.

Bajeti mbadala Chadema, kufuta posho za vikao

Yataja vipaumbele sita ikiwamo miundombinu, umeme

Na Grace Michael

KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni imetangaza mwelekeo wa bajeti mbadala ya 2011/2012 huku ikisisitiza kufuta posho za vikao kwenye mfumo wa serikali kwa lengo la kupunguza mzigo wa matumizi yake.
Masuala mengine yaliyosisitizwa kwenye mwelekeo huo ni kupunguza misamaha ya kodi kutoka asilimia 4.5 hadi asilimia moja na kuanzisha kitengo cha kushughulikia mafisadi wakubwa ambao wanalalamikiwa na wananchi.

Kambi hiyo imetaja vipaumbele sita katika bajeti hiyo ambavyo ni miundombinu, umeme, kuwezesha ukuaji wa sekta za uzalishaji na ukuaji wa uchumi vijijini, maendeleo ya rasilimali watu, utawala bora pamoja na kuimarisha usimamizi wa mashirika ya umma.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Waziri Kivuli wa Uchumi na Fedha, Bi. Christina Lissu, alisema kuwa bajeti hiyo mbadala inalenga kutoa unafuu wa kikodi kwa wananchi maskini na kuhakikisha 'kila anayetakiwa kulipa kodi analipa'.

Akifafanua vipaumbele hivyo, alisema kuwa, katika miundombinu bajeti hiyo itasisitiza barabara zote muhimu ambazo hazijaanza kujengwa zianze mwaka huu wa fedha, upanuzi wa bandari uzingatiwe sambamba na uboreshaji wa reli ya kati, ili iweze kufanya kazi ya kusafirisha mizigo na abiria kwa kiwango cha kuridhisha, pamoja na kuongeza mtaji katika Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) ili liweze kujiendesha kibiashara.

Alisema kuwa suala la umeme imependekezwa fedha zielekezwe kwenye miradi mitatu ya makaa ya mawe ya megawati 1,500 katika migodi ya Mchuchuma, Ngaka na Kiwira, umeme wa gesi wenye megawati 300 kutoka Mtwara, Dar es Salaam hadi Mwanza na mradi wa kusambaza umeme mijini na vijijini.

Katika kipaumbele cha kuwezesha ukuaji wa sekta za uzalishaji na hasa ukuaji wa uchumi vijijini, alisema kuwa kutaboreshwa miundombinu, upatikanaji wa maji safi na salama, kuongeza ubora wa bidhaa za kilimo, kupeleka umeme vijijini na kuelekeza rasilimali za kutosha kwenye kukuza uchumi vijijini.

Akielezea maendeleo ya rasilimali watu, Bi. Lissu alisema bajeti hiyo inasisitiza watoto wanaomaliza kidato cha nne wanapata mafunzo ya ufundi ili waweze kujiajiri wanaporejea vijijini, huku lengo kubwa katika bajeti hiyo ikiwa ni upatikanaji wa elimu bora na si wingi wa majengo ya shule au wanafunzi wanaomaliza shule.

Suala jingine la elimu linalowekewa umuhimu ni kuhakikisha bodi ya mikopo ya elimu ya juu inapata fedha za kutosha kutoka kwenye kodi ya uendelezaji ujuzi ambayo theruthi mbili yake hupelekwa hazina, lakini kambi ya upinzani inataka fedha hizo zibaki kwa bodi hiyo ili kukidhi mahitaji ya mikopo.

Jambo jingine katika kipaumbele hicho ni kuanzisha bima ya afya kwa wananchi wote ambayo itakuwa ni ya lazima kwa wafanyakazi na wasio wafanyakazi ambayo itachangiwa na wananchi pamoja na serikali.

Katika kuimarisha utawala bora, Bi. Lissu alisema kuwa wanaitaka serikali kutenga fedha zitakazowezesha kuwashirikisha vyema wananchi katika mchakato wa uandikwaji wa katiba mpya pia kuimarisha TAKUKURU kwa kuanzisha kitengo maalumu kitakachoshughulikia ufisadi mkubwa.

Mbali na hilo Serikali ya Chadema kama ingekuwa na ridhaa ya kuongoza, ingeweka mfumo mpya wa kudhibiti mgongano wa maslahi hasa katika biashara na siasa, ambapo alisema kuwa suala hilo litawezekana kwa kuweka mkazo katika utangazaji wa mali za viongozi.

"Kuna mkazo pia katika kuanzisha Ofisi ya Bajeti ya Bunge ili kuweka uwazi kwenye Bajeti ya Serikali kwani kwa sasa wabunge hawahusishwi katika kupanga bajeti ya serikali...tunapendekeza itungwe sheria ya bajeti itakayowezesha kuanzishwa kwa ofisi hiyo," alisema.

Alisema kuwa bajeti hiyo pia itaainisha vyanzo vipya vya mapato na kuboresha vilivyopo kwa kupunguza bei ya mafuta kwa asilimia 40 kutoka bei ya sasa, kupanua wigo wa kodi kwa kuweka lengo la kukusanya mapato ya ndani sawa na asilimia 20 ya Pato la Taifa, kuongeza wigo wa walipa kodi, kuangalia mfumo mpya wa utawala wa kodi na kufuta matumizi mengine na kupunguza matumizi yasiyo na maana kwenye maofisi.

"Hakuna haja ya kuwepo kwa posho za vikao na wakati mtu huyo anatekeleza majukumu yake...kuwe na sheria kali za kuzuia ukwepaji kodi kwa mashirika makubwa ya nje na hasa kampuni za madini na mafuta," alisema Bi. Lissu.

Alisema kuwa mambo mengi yatafafanuliwa wakati wa uwasilishwaji wa bajeti mbadala ya kambi ya upinzani itakayowasilishwa na Bw. Zitto Kabwe ambaye ni Waziri Kivuli wa Uchumi na Fedha.