Na Grace Michael
SIKU moja baada ya viongozi wa dini kumpa saa 48 Rais Jakaya Kikwete kuwataja kwa majina ya baadhi yao wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, Ikulu imeshindwa kutaja majina hayo, badala yake ikasema kauli hiyo haikutarajiwa kutoka kwa viongozi hao kwa kuwa nao si malaika ama watakatifu hapa duniani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu jana na kusainiwa na Mwandishi Msaidizi wa Rais, Bi. Premy Kibanga, kauli ya viongozi hao wa dini ni ya kusikitisha na haikutarajiwa kutoka kwao.
“Viongozi wa dini ni watu wa kutumainiwa sana katika jamii yeyote, lakini ikizingatiwa kuwa wao sio malaika ama watakatifu hapa duniani, nao wanatumbukia katika majaribu na kujikuta katika vitendo au hali isiyo tegemewa kabisa,” ilisema taarifa hiyo.
Badala ya kutaja majina ya wauza 'unga', taarifa hiyo ilieleza kuwa hivi karibuni wapo viongozi wa dini waliokamatwa kwa rushwa, ngono na kutuhumiwa kujihusisha na vitendo mbalimbali ambavyo ni kinyume na maadili ya jamii na wapo ambao wamekamatwa na watafikishwa kwenye vyombo vya sheria, lakini wapo wanaochunguzwa hivyo kutokana na hayo viongozi hao hawakutakiwa kujitetea kwa kauli nyepesi kwa kumpa Rais saa 48."
Ilisisitiza kuwa kiongozi anayejishuku ajisalimishe mwenyewe na anayeshukiwa na jamii afichuliwe ili afanyiwe uchunguzi na hatimaye sheria ichukue mkondo wake, lakini si kusubiri Rais awataje hadharani ndiyo viongozi hao waanze kuchukua hatua.
Vyombo vya habari jana viliwakariri baadhi ya viongozi wa dini wakimpa Rais Kikwete muda wa saa 48 kuwataja viongozi aliowatuhumu kwa ujumla kuwa wanajihusisha na biashara hiyo haramu.
Taarifa hiyo ilifafanua mambo aliyoyazungumza Rais Kikwete kwenye sherehe ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu John Ndimbo wa Jimbo la Mbinga ambapo Rais Kikwete alitoa ombi la kuwataka viongozi hao kujihusisha kikamilifu katika mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya.
“Ni tatizo linalozidi kukua pamoja na jitihada za Serikali kupitia vyombo vya usalama kuwabana, kuwawajibisha watumiaji na wafanyabiashara ya dawa za kulevya. Athari zake kwa jamii zinaeleweka, hivyo sihitaji kuzirudia...
“Kila siku kuna watu wanaokamatwa kwa kujihusisha na dawa za kulevya na hiyo inaashiria kuimarika kwa vyombo vyetu vya usalama, lakini inasikitisha sana kuona kuwa biashara hiyo sasa inawavutia hata watumishi wa Mungu.
"Huku sasa tunakoelekea kwa kweli ni kubaya sana. Nawaomba mtoe uzito unaostahili kwa tatizo hili. Viongozi wa dini mnasikilizwa, Nawaomba kemeeni, onyeni na elimisheni jamii juu ya madhara ya dawa za kulevya, waelimisheni vijana ambao ndiyo walengwa wakuu, waepuke na waache kujihusisha na biashara na matumizi ya dawa za kulevya,” alisema.
Taarifa hiyo iliongeza: “Mtu akikuonya kuwa nyumbani kwako kumeonekana nyoka, huanzi kwa kuuliza kama kweli, ni wa rangi gani? Unatakiwa kushtuka na kujiandaa kumsaka kwa nia ya kumwondoa nyumbani kwako hata ikibidi umuue ili asije akaleta madhara makubwa kwako na kwa familia yako, hivyo Rais alikuwa na nia njema katika kulielezea jambo hili, na mwenye nia njema haumbuki,” ilisema taarifa hiyo.
Pia viongozi hao walitakiwa kuweka mikakati na vipaumbele vya kufanyia kazi changamoto hiyo na sio kuahirisha tatizo hili ambalo linazidi kuwa kubwa na kazi ya kupambana na dawa za kulevya haimhusu Rais peke yake bali inamhusu kila Mtanzania.
No comments:
Post a Comment