Na Grace Michael
HATIMAYE Kamati ya Bunge ya Miundombinu imepitisha bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia huku ikiendelea na msimamo wake wa kutopitisha bajeti ya Wizara ya Uchukuzi endapo Serikali haitatenga fedha za reli,Shirika la Ndege Tanzania (ATC) na Wakala wa Meli.
Hatua hiyo iliwekwa rasmi Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw. Peter Serukamba ambaye alisema kuwa kamati yake haitakuwa tayari kupitisha bajeti hiyo bila kuwepo kwa fedha hizo.
"Tuna sababu zetu, tunataka fedha za reli, ATC na wakala wa meli, wapo watu wanasema kuwa fedha za reli zipo lakini kwenye vitabu hazipo, hakuna mpango wa serikali ambao fedha zake ziko mdomoni hivyo hatutakubali mpaka tuone fedha hizo ndani ya vitabu," alisema Bw. Serukamba.
Alisema kuwa Serikali inaweza ikapunguza matumizi ambayo si ya lazima katika wizara mbalimbali ili fedha hizo zikatumike katika masuala hayo ambayo ni ya muhimu kwa nchi na wananchi wa Tanzania.
Alitolea mfano wa Wizara ya fedha ambayo imetengewa mabilioni ya fedha katika matumizi ya kawaida huku mambo ya msingi kama reli inayotegemewa na wananchi wengi ikiachwa bila fedha zozote.
"Hatuwezi kuendelea huku tukiendekeza starehe na hata nyumbani kwako ukitaka kuendelea ni lazima upunguze starehe hivyo watu wa kawaida hawatatuelewa kutoweka fedha za kukarabati reli usafiri ambao ni tegemeo kubwa kwa wananchi wengi wa Tanzania.
Alisema kuwa nia ya Kamati ni njema kwa kuwa hata gharama za bidhaa zinapanda kutokana na gharama kubwa ya usafirishaji gharama ambayo ingepungua endapo kungekuwa na usafiri wa uhakika wa reli.
"ATC inahitaji bilioni 23 zikiwemo bilioni mbili za kulipia gharama za ndege zilizokwenda kwenye matengenezo...kama serikali imeshindwa kufanya hivyo basi itangaze imefunga shirika hilo ili wafanyakazi wake warejee majumbani kwani huwezi ukatenga fedha za kulipa wafanyakazi huku hakuna kazi wanayoifanya," alisema Bw. Serukamba.
Alisema kuwa hawatakubali ndege mbili za ATC zifie Afrika Kusini zilikokwenda kwa ajili ya matengenezo hivyo akasisitiza kutengwa kwa fedha hizo kwa ajili ya kulikwamua shirika hilo. Alisema kuwa yapo maeneo kwenye bajeti za wizara ambayo yametengewa fedha za matumizi ya kawaida maeneo ambayo yanaweza zikapunguzwa na fedha kwa ajili reli, ATC na wakala wa meli zitapatikana.
Akizungumzia bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Bw. Serukamba alisema kuwa Kamati imemwagiza Waziri mwenye dhamana Bw. John Magufuli kuhakikisha anasimamia sheria za nchi ili sekta hiyo iweze kufanikiwa hasa katika ujenzi wa barabara ambao umewekewa mkazo mkubwa katika bajeti hiyo.
Alisema kuwa wizara hiyo imeweka mipango mizuri ambayo imekubalika na kamati hiyo ikiwemo mipango ya ujenzi wa nyumba za Serikali, ujenzi wa barababa madaraja yakiwemo ya Kigamboni, Malagarasi na Kilombero. Alisema kuwa jambo linalotakiwa kufanywa na wizara hiyo ni kuhakikisha inasimamia sheria ili utekelezaji wa waliyoyapanga yaweze kufanyika.
No comments:
Post a Comment