*Wasema amri hiyo inakiuka sheria
*Wadai Jeshi la polisi lina ubaguzi
Na Grace Michael
KAMBI rasmi ya Upinzani Bungeni imeshtushwa na amri iliyotolewa na Mahakama ya Arusha ya kumkamata kiongozi wa kambi hiyo, Bw. Freeman Mbowe kwa kuwa inakiuka sheria, mila na desturi zinazohusu kinga, haki na mamlaka ya Bunge na ambazo ndio msingi mkuu wa demokrasia ya kibunge.
Mbali na kushtushwa lakini pia imedai kuwa imeshangazwa na unafiki pamoja na ubaguzi wa wazi unaooneshwa na Jeshi la Polisi juu ya Wabunge wa vyama vya upinzani kwa kuwakamata bila ya kuomba kibali kwa Spika wa Bunge kama inavyofanyika kwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi.
Kutokana na hatua hiyo, Bw. Mbowe ameweka wazi msimamo wake kwa kusema kuwa yuko tayari kusimamia haki za kambi hiyo kwa gharama yoyote huku akitumia msemo usemao "Bora kufa umesimama kuliko kuishi umepiga magoti'.
Hatua hiyo ilifikiwa Dar es Salaam jana ambapo Bw. Mbowe kwa kushirikiana na viongozi wengine wa kambi ya upinzani kueleza kilichotokea mahakamani na namna walivyokubaliana na mahakama huku wakieleza haki na kinga walizonazo.
Bw. Mbowe alisema kuwa kitendo kinachofanywa na Mahakama hiyo anaweza akakihusisha na njama ya kuwatoa wabunge hao kwenye kupigania agenda za muhimu kwa Watanzania hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Bunge la Bajeti, kipindi kinachotaka utulivu na amani ili wabunge wapate fursa ya kufikiri kwa kina na kwa umakini.
"Nadhani mambo haya yanafanyika kwa makusudi kabisa ili watuondoe kwenye hoja za msingi...mahakamani tulikubaliana kimsingi kuwa hatutahudhuria siku ya kesi kwa kuwa tunaanza vikao vya kamati na vikao vya bunge...nikiwa kama kiongozi wa upinzani nina serikali yangu kivuli ambayo inahitaji uongozi wangu hivyo isingekuwa rahisi kwenda Arusha," alisema Bw. Mbowe.
Pamoja na kusema hayo, alisema kuwa kambi hiyo haijawahi kudharau mamlaka ya Mahakama na wala haitegemei kufanya hivyo lakini akasisitiza kuzingatiwa kwa haki za msingi zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.
Akizunguzma amri iliyotolewa na mahakama, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bw. Tundu Lissu, alisema kuwa ibara ya 100 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatambua na kulinda “uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge na uhuru huo hauwezi kuvunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katika Mahakama au mahali penginepo nje ya Bunge.
Bw. Lissu alikwenda mbali zaidi kwa kueleza maeneo ambayo mbunge ana kinga nayo ni ukumbi ambao hutumiwa kwa vikao vya Bunge, pamoja na ofisi, vyumba, vibambaza, maeneo ya wageni, bustani na maeneo mengine yaliyowekwa kwa ajili ya matumizi au malazi ya wajumbe, maofisa au wageni wa Bunge pamoja na njia zinazounganisha maeneo hayo na maeneo yanayoweza kutangazwa na Spika hivyo akasema kuwa hata akiwa ndani ya gari la Kambi ya upinzani anakuwa na kinga.
Alisema kuwa wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Arusha inatoa amri dhidi ya Bw. Mbowe alikuwa analindwa na kinga ya Bunge na kinga hiyo itaendelea kwa kipindi chote cha Mkutano wa Nne wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Akizungumzia unafiki na ubaguzi wa Jeshi la Polisi, Bw. Lissu alisema kuwa wabunge wa vyama vya upinzani wamekuwa wakikamatwa bila ya kuwepo kwa kibali chochote cha Spika kama inavyotakiwa na Sheria ya Kinga, Mamlaka na Haki za Bunge.
Aliwataja wabunge ambao wamekamatwa na polisi bila kibali ni Bw. Mbowe, Bw. Godbless Lema (Arusha Mjini), Bw. Phillemon Ndesamburo (Moshi Mjini), Bw. Joseph Selasini (Rombo), Bw. Meshack Opulukwa (Meatu), Bw. Tundu Lissu (Singida Mashariki), Bi. Esther Matiko (Viti Maalum, CHADEMA) na Bi. Magdalena Sakaya (Viti Maalum, CUF).
Alisema kuwa wabunge wa CCM na ambao wanakabiliwa na tuhuma za makosa makubwa zaidi wamekuwa wakiombewa kibali cha Spika kabla ya kukamatwa na katika hilo walisema wanao ushahidi wa barua ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Mwanza SP B.M. Wakulyamba kwa Katibu wa Bunge ya kumwomba Bw.Titus Mlengeya Kamani (Busega, CCM) kwa ajili kuhojiwa na Jeshi la Polisi kuhusu madai ya kuhusika kwake na njama za kutaka kumwuua aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Busega Dkt. Raphael Chegeni.
Alisema kuwa hatua hiyo inadhirihisha upendeleo wa wazi wa Jeshi la Polisi kwa Wabunge wa CCM na kwa sababu hizo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haitarajii, na itapinga kwa nguvu zote kitendo chochote cha kumtishia au kumkamata Kiongozi wa kambi hiyo kwa kipindi chote ambacho ana kinga ya Bunge kama inavyotambuliwa na Katiba na sheria.
Kambi hiyo imesema inatarajia kuwasilisha barua ya malalamiko katika Ofisi ya Katibu wa Bunge ili haki iweze kutendeka kwa wabunge wote na kuondoa ubaguzi uliopo.
No comments:
Post a Comment