Wednesday, June 1, 2011

Bajeti mbadala Chadema, kufuta posho za vikao

Yataja vipaumbele sita ikiwamo miundombinu, umeme

Na Grace Michael

KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni imetangaza mwelekeo wa bajeti mbadala ya 2011/2012 huku ikisisitiza kufuta posho za vikao kwenye mfumo wa serikali kwa lengo la kupunguza mzigo wa matumizi yake.
Masuala mengine yaliyosisitizwa kwenye mwelekeo huo ni kupunguza misamaha ya kodi kutoka asilimia 4.5 hadi asilimia moja na kuanzisha kitengo cha kushughulikia mafisadi wakubwa ambao wanalalamikiwa na wananchi.

Kambi hiyo imetaja vipaumbele sita katika bajeti hiyo ambavyo ni miundombinu, umeme, kuwezesha ukuaji wa sekta za uzalishaji na ukuaji wa uchumi vijijini, maendeleo ya rasilimali watu, utawala bora pamoja na kuimarisha usimamizi wa mashirika ya umma.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Waziri Kivuli wa Uchumi na Fedha, Bi. Christina Lissu, alisema kuwa bajeti hiyo mbadala inalenga kutoa unafuu wa kikodi kwa wananchi maskini na kuhakikisha 'kila anayetakiwa kulipa kodi analipa'.

Akifafanua vipaumbele hivyo, alisema kuwa, katika miundombinu bajeti hiyo itasisitiza barabara zote muhimu ambazo hazijaanza kujengwa zianze mwaka huu wa fedha, upanuzi wa bandari uzingatiwe sambamba na uboreshaji wa reli ya kati, ili iweze kufanya kazi ya kusafirisha mizigo na abiria kwa kiwango cha kuridhisha, pamoja na kuongeza mtaji katika Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) ili liweze kujiendesha kibiashara.

Alisema kuwa suala la umeme imependekezwa fedha zielekezwe kwenye miradi mitatu ya makaa ya mawe ya megawati 1,500 katika migodi ya Mchuchuma, Ngaka na Kiwira, umeme wa gesi wenye megawati 300 kutoka Mtwara, Dar es Salaam hadi Mwanza na mradi wa kusambaza umeme mijini na vijijini.

Katika kipaumbele cha kuwezesha ukuaji wa sekta za uzalishaji na hasa ukuaji wa uchumi vijijini, alisema kuwa kutaboreshwa miundombinu, upatikanaji wa maji safi na salama, kuongeza ubora wa bidhaa za kilimo, kupeleka umeme vijijini na kuelekeza rasilimali za kutosha kwenye kukuza uchumi vijijini.

Akielezea maendeleo ya rasilimali watu, Bi. Lissu alisema bajeti hiyo inasisitiza watoto wanaomaliza kidato cha nne wanapata mafunzo ya ufundi ili waweze kujiajiri wanaporejea vijijini, huku lengo kubwa katika bajeti hiyo ikiwa ni upatikanaji wa elimu bora na si wingi wa majengo ya shule au wanafunzi wanaomaliza shule.

Suala jingine la elimu linalowekewa umuhimu ni kuhakikisha bodi ya mikopo ya elimu ya juu inapata fedha za kutosha kutoka kwenye kodi ya uendelezaji ujuzi ambayo theruthi mbili yake hupelekwa hazina, lakini kambi ya upinzani inataka fedha hizo zibaki kwa bodi hiyo ili kukidhi mahitaji ya mikopo.

Jambo jingine katika kipaumbele hicho ni kuanzisha bima ya afya kwa wananchi wote ambayo itakuwa ni ya lazima kwa wafanyakazi na wasio wafanyakazi ambayo itachangiwa na wananchi pamoja na serikali.

Katika kuimarisha utawala bora, Bi. Lissu alisema kuwa wanaitaka serikali kutenga fedha zitakazowezesha kuwashirikisha vyema wananchi katika mchakato wa uandikwaji wa katiba mpya pia kuimarisha TAKUKURU kwa kuanzisha kitengo maalumu kitakachoshughulikia ufisadi mkubwa.

Mbali na hilo Serikali ya Chadema kama ingekuwa na ridhaa ya kuongoza, ingeweka mfumo mpya wa kudhibiti mgongano wa maslahi hasa katika biashara na siasa, ambapo alisema kuwa suala hilo litawezekana kwa kuweka mkazo katika utangazaji wa mali za viongozi.

"Kuna mkazo pia katika kuanzisha Ofisi ya Bajeti ya Bunge ili kuweka uwazi kwenye Bajeti ya Serikali kwani kwa sasa wabunge hawahusishwi katika kupanga bajeti ya serikali...tunapendekeza itungwe sheria ya bajeti itakayowezesha kuanzishwa kwa ofisi hiyo," alisema.

Alisema kuwa bajeti hiyo pia itaainisha vyanzo vipya vya mapato na kuboresha vilivyopo kwa kupunguza bei ya mafuta kwa asilimia 40 kutoka bei ya sasa, kupanua wigo wa kodi kwa kuweka lengo la kukusanya mapato ya ndani sawa na asilimia 20 ya Pato la Taifa, kuongeza wigo wa walipa kodi, kuangalia mfumo mpya wa utawala wa kodi na kufuta matumizi mengine na kupunguza matumizi yasiyo na maana kwenye maofisi.

"Hakuna haja ya kuwepo kwa posho za vikao na wakati mtu huyo anatekeleza majukumu yake...kuwe na sheria kali za kuzuia ukwepaji kodi kwa mashirika makubwa ya nje na hasa kampuni za madini na mafuta," alisema Bi. Lissu.

Alisema kuwa mambo mengi yatafafanuliwa wakati wa uwasilishwaji wa bajeti mbadala ya kambi ya upinzani itakayowasilishwa na Bw. Zitto Kabwe ambaye ni Waziri Kivuli wa Uchumi na Fedha.

No comments:

Post a Comment