Wednesday, June 15, 2011

Wadau wasema rushwa kubwa bado tatizo

Na Grace Michael

WADAU wa kupambana na rushwa nchini wameitaka serikali kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) kuweka jitihada za dhati katika kupambana na watoa rushwa na wapokea rushwa wakubwa ambao ndio wana athari kubwa katika maendeleo.

Wamesema kuwa hawajarishwa na jitihada za kupambana na rushwa hasa kwa watoa rushwa wakubwa ambao ndio wanasababisha athari kubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi hii.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na wadau wa sekta mbalimbali wa kupambana na rushwa katika kongamano la mwaka la wadau wa kupambana na kuzuia rushwa nchini.

Akizungumzia hilo, Mwenyekiti wa Kampuni ya IPP, Bw. Reginald Mengi alisema kuwa eneo la watoa rushwa wakubwa halijashughulikiwa na nguvu kubwa imeelekezwa kwa wapokeaji.

Alisema kuwa nchi haitashinda vita dhidi ya rushwa bila ya kuwashughulikia watoa rushwa wakubwa hivyo kuna haja ya kuchukua maamuzi au hatua kali dhidi yao ili kukata mzungunguko huo haramu.

"Hawa watoa rushwa wakubwa wana nguvu kubwa ya kifedha na wana uwezo wa kuhakikisha wanakwamisha jitihada mbalimbali lakini ni lazima tufike mahali hatua kali zichukuliwe hata kama hazitawafurahisha baadhi ya watu," alisema Bw. Mengi.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Bw. Julius Mtatiro alisema kuwa mapambanao ya rushwa nchini yamekwama kwa kuwa nguvu kubwa imeelekezwa kwenye rushwa ndogo ndogo huku rushwa kubwa zikiachwa.

"Vigogo wanahusika na rushwa na hawachukuliwi hatua zozote na ndio maana hata huko mahakamani wanaofikishwa na waliohusika na rushwa ndogo ndogo tu na hatua zinashindikana kuchukuliwa kutokana na kuendekeza mambo ya kujuana na urafiki, hivyo hata nguvu ya kupambana ipasavyo inakwama," alisema Bw. Mtatiro.

Alisema kuwa bila ya viongozi wenyewe serikalini kujiweka katika mazingira safi hawataweza kupambana na vita hiyo, hivyo akasema kuwa kutokana na kutokuwa makini kwa serikali kunakwamisha upambanaji wa vita hiyo.

Alisema kuwa wao kama upinzani, watatimiza wajibu wao wa kuhamasisha wananchi kuichukia rushwa lakini pia wao wenyewe ndani ya chama kuhakikisha wanakuwa safi ili wawe mfano kwa jamii na waweze kusikilizwa na jamii.

"Kama wananchi wanakujua uchafu wako hawawezi kusikiliza unachokikemea hivyo kama huko wizarani ni kuchafu, mamilioni ya fedha kwenye halmashauri yanaibwa bila hatua kamwe jamii haiwezi kusikiliza suala hilo, hivyo ni vyema serikali ingeweka umakini katika kushughulikia suala hilo," alisema Bw. Mtatiro.

Akizungumzia madhara ya rushwa yanavyoathiri ukuaji wa uchumi na ufanyaji wa biashara, Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara Taifa (TNBC), Bw. Dan Mrutu alisema kuwa rushwa inachangia kwa kiasi kikubwa kupandisha gharama za kufanya biashara kwa kuwa mchakato wote uhitaji rushwa ili kufanikisha biashara.

"Mfano unataka kufanya biashara ambayo mtaji wake umepanga uwe milioni moja, unaweza ukatumia milioni tatu kwa kuwa kila mtumishi katika mnyororo huo anataka rushwa, kila utakapofika utakwamishwa, hivyo hadi unafanikiwa unakuwa umeingia gharama kubwa bila sababu ya msingi hivyo rushwa ni adui katika ukuaji wa uchumi," alisema.

Alisema kuwa endapo rushwa haitashughulikiwa ipasavyo itaathiri hata mpango wa kilimo kwanza kwa kuwa hata upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya kilimo nako itahitajika rushwa kwa ajili ya maofisa wanaoshughulikia ardhi, hivyo kuna kila haja ya kupambana na rushwa katika maeneo yote.

Akizungumzia tathimi ya kupambana na vita ya rushwa nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa TAKUKURU, Dkt. Edward Hosea alisema kuwa jitihada za serikali na wananchi zinazaa matunda kwa kuwa hata wadau wametambua kuwa kazi hiyo si ya TAKUKURU peke yake bali ni ya wadau wote.

Alisema kuwa wananchi kwa sasa wametambua madhara ya rushwa hatua inayowafanya hata kutoa ushirikiano katika mamlaka husika lakini pia hakusita kuvipongeza vyombo vya habari kwa kazi kubwa iliyofanyika katika kuibua mambo mbalimbali ya rushwa na kufanikisha kuchukuliwa hatua.

Alisema kuwa kama kuna malalamiko yoyote ya kutokuchukuliwa kwa hatua kwa baadhi ya watoa au wala rushwa ni vyema wenye ushahidi wakajitokeza ili TAKUKURU iweze kufanyia kazi kwa kuwa nchi inaongozwa kwa Utawala wa Sheria na si hisia.

Bw. Hosea alipobanwa na vyombo vya habari kuhusiana na wamiliki wa Kampuni ya Kagoda kutoshughulikiwa, alisema kuwa wao kama TAKUKURU hawaiogopi Kagoda wala mla rushwa yoyote na kutokana na hali hiyo akasisitiza kuwa mwananchi yoyote mwenye ushahidi auwasilishe.

"Unajua sisi tunachunguza na tunapomaliza kazi yetu tunapeleka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ambaye naye hutoa uamuzi kama mhusika apelekwe mahakamani au la, na hiyo inatokana na ushahidi uliopo na ndio maana alishawahi kuwaomba wenye ushahidi wauwasilishe hatuwezi kuwakamata watu bila kuwa na ushahidi," alisema Bw. Hosea.

Akifungua Kongamano hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, Bw. Mathias Chikawe, aliwataka viongozi katika maeneo yao ya kazi kusimamia utawala bora kwa kuhakikisha maadili ya kazi yanafuatwa lakini viongozi wa jamii wakiwemo wa dini na wanasiasa, aliwataka kukemea rushwa na vitendo vya ufisadi kila wanapopata nafasi ya kuzungumza na wananchi kwa maana ya wafuasi au wanachama wao.

No comments:

Post a Comment