MKUU wa Mkoa Tanga Chiku Galawa amewataka viongozi mkoani humo kuhakikisha wanafanya uhamasishaji juu ya mradi wa Mama Mjamzito na Mtoto Mchanga unaofadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya Ujerumani (KfW) kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bimaya Afya ili mradi huo uweze kuwa tija.
Amesema ni lazima viongozi waamke na kuongeza mapambano ya kunusuru afya za akina mama wajawazito na watoto.
Galawa aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Mradi huo ambao ulifanyika mkoani humo na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wafadhili wa Mradi huo, wakuu wa Wilaya, Uongozi kutoka Mkoa wa Mbeya, wanufaika wa mradi huo ambao ni akina mama wajawazito na wadau wengine.
“Uendelevu wa Mradi huu utatokana na juhudi za uelimishaji wa wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii na Mfuko wa Taifa wa Bila ya Afya…natoa mwito kwa viongozi wenzangu wa Mkoa wa Tanga na Mbeya tuone fahari juu ya mradi huu muhimu na tujione wenye bahati miongoni mwa Watanzania,” alisema Galawa.
Alisema kuwa pamoja na juhudi mbalimbali ambazo zinafanywa na Serikali katika kukabiliana na changamoto za Sekta ya Afya lakini bado zimeendelea kuibuka zingine kutokana pia na kuongezeka kwa idadi watu hivyo Serikali peke yake ina mzigo mkubwa unaotakiwa kuungwa mkono na wadau wengine wa maendeleo.
“Kutokana na hali hiyo inayoikabili Serikali, daima tunaendelea kujivunia kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kuwahudumia wananchi katika maeneo tofauti ya nchi yetu kulingana na makundi yao,” alisema na kuongeza.
“Ni kazi hiyo nzuri inayofanywa na Mfuko huu ambayo imewezesha Wafadhili kutoka Serikali ya Ujerumani (KfW) kukubali kuunga mkono juhudi hizo na sasa kwa ajili ya wanawake wajawazito na watoto wachanga katika mikoa ya Tanga na Mbeya,” alisema Galawa.
Alisema mradi huo unaolenga kuboresha huduma za afya hasa kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga utasaidia akina mama kujifungua katika mazingira ya uangalizi zaidi na kuepukana na madhara ambayo wangeweza kuyapata kutokana na kujifungulia majumbani.
Galawa pia alieleza kuwa moja ya faida za mradi huo ni pamoja na kutoa vifaa tiba kama vile vitanda vya kujifungulia na vingine hivyo hatua hiyo itasaidia kutokana na ukweli kwamba vituo vingi vinakabiliwa na upungufu wa vifaa tiba.
“Ni matumaini yangu kuwa watoa huduma wa mikoa hii mtazingatia matumizi bora ya vifaa hivyo ili view endelevu na hasa kwa malengo yaliyokusudiwa,” alisema Galawa.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka viongozi wa Halmashauri wakiongozwa na Madiwani watatekeleza wajibu wao wa kuhakikisha kwamba mradi huo unakuwa na tija na utambuzi wa akina mama hao unafanywa kwa uwazi bila upendeleo ili lengo la kuhakikisha uzazi salama kwa wanawake linatimia.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Emanuel Humba alisema kuwa lengo kubwa la mradi huo ni kuwawezesha akina mama wasio na uwezo kupata huduma za matibabu kupitia utaratibu wa NHIF katika kipindi chote cha ujauzito na miezi mitatu baada ya kujifungua.
Aidha mradi huo utasaidia kuzilipia kaya za akina mama hao mchango wa Mfuko wa Afya ya Jamii kwa kipindi cha mwaka mmoja, kuwajengea uwezo wa kifedha watoa huduma zitokanazo na Bima ya Afya.
Humba alisema kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa katika Wilaya ya Korogwe, Pangani, Ileje na Rungwe kwa kuwaandikisha wajawazito na kuwapatia vitambulisho vya Bima ya Afya, usambazaji wa fomu 12,700 za kuandikisha walengwa ambapo mpaka hivi sasa jumla ya akina mama 600 wameshajitokeza na kuanza kufaidika.
Kutokana na hayo, Humba aliwaomba viiongozi wote wakiwemo wabunge kuhakikisha wanasaidia suala la uhamasishaji ili akina mama wengi zaidi na wasio na uwezo waweze kunufaika na Mradi huo.
Naye Mwakilishi wa KfW, Dk Kai Gesing alisema kuwa suala la afya ni suala nyeti sana hasa katika kuwasaidia akina mama wajawazito na watoto hivyo kwa kulitambua hilo, wakaona umuhimu wa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya katika kutekeleza Mradi huo.
"Suala la akina mama ni suala nyeti sana na ndio maana tumeamua kuja na Mradi huu ili hatimaye tupunguze idadi ya vifo vya akina mama hawa lakini pia kuhakikisha wengi wanajifungulia katika vituo vya afya na kwenye mazingira mazuri," alisema Dk Gesing.
Kwa upande wa wanufaika wa mradi huo ambao ni akina mama wajawazito, waliupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya pamoja na wafadhili wa mradi huo kwa kuleta mradi huo ambao wao wanauona ni mkombozi wa afya zao pamoja na familia zao ambazo zitanufaika kwa matibabu kupitia CHF.
No comments:
Post a Comment