Wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wakifurahia. |
WATUMISHI wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wametakiwa kufanya kazi huku wakilinda maslahi ya Mfuko huo na kuweka malengo ya muda mrefu ili uendelee kutoa huduma bora kwa wanachama wake.
Mwito huo ulitolewa Dar es Salaam juzi na Mjumbe wa Bodi Bi. Mariam Wilmore wakati akitoa nasaha zake kwa watumishi wa Mfuko huo wakati wa sherehe ya kukaribisha mwaka iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Alisema kuwa pamoja na sifa mbalimbali za kitaifa na Kimataifa zinazotolewa kwa Mfuko huo lakini ipo haja kwa wafanyakazi wote kujenga mshikamano na kujivunia ubima kwa lengo la kuuendeleza zaidi Mfuko na kuufanya uzidi kuwa imara.
Mbali na hayo, wajumbe wengine wa bodi walitumia fursa hiyo, kuupongeza uongozi wa Mfuko kwa kuufikisha hapo ulipo licha ya kwamba ulianza kwa kukabiliwa na changamoto nyingi ambazo zilihitaji viongozi imara na wavumilivu.
Kutokana na hali hiyo, wameutaka kuendekea kuwa imara na kutoyumbishwa kwa namna yoyote ili wanachama wake waendelee kunufaika na huduma bora zinazotolewa mpaka sasa.
"Yawezekana uimara huu umewezeshwa na aliyekikamata chombo hiki ambaye kwa kweli tuna kila sababu ya kumpongeza, uimara wake ndo unaowezesha hata haya mafanikio yaliyopo sasa," alisema Mjumbe wa Bodi, Gratian Mukoba.
Pamoja na kupongezwa kwa mafanikio yaliyofikiwa na Mfuko huo, mjumbe mwingine Prof. Joseph Shija hakusita kuwaelezwa watumishi wa Mfuko huo matumaini makubwa waliyonayo Watanzania katika Mfuko huo, hivyo akawataka kutobweteka na mafanikio yaliyofikiwa mpaka sasa na badala yake akawataka kuongeza bidii ya kazi kwa lengo la kuboresha zaidi.
"Siwezi nikashangaa kusikia mafanikio mengi ambayo mnayo mpaka sasa likiwemo la kupata Tuzo ya Kimataifa kutokana na ubora wa huduma zenu...najua kazi mliyoifanya katika kipindi hiki cha miaka 10 ni kubwa, msilewe sifa hizi ongezeni bidii katika kazi ili hatimaye mfikie lengo la afya bora kwa kila Mtanzania," alisema Prof. Shija.
Aidha aliwataka watumishi kufanya kazi kwa uadilifu na kuachana na utamaduni wa unung'unikaji lakini pia kuhakikisha wanajenga dhana ya kujiendeleza kitaaluma kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
"Kamwe msiridhike na mlichonacho, ongezeni bidii na kujiendeleza ili utendaji uzidi kuwa bora zaidi na suala hili ili litekelezwe kwa ari, Mfuko unatakiwa kuwa na mpango wa kuwatunuku na kuwapa motisha watumishi bora kwa kila mwaka ili wengine waweze kuiga," alisema Prof. Shija.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Emanuel Humba, aliwataka watumishi kutojiona wanyonge katika hatua ambayo Mfuko iko nayo kwani ni kubwa ikilinganishwa na mifuko mingine iliyoanza kabla ya Mfuko huo.
"Mtakumbuka tulianza na changamoto nyingi sana lakini sasa tuko pazuri...watu walidiriki kutuita 'njiti' lakini hilo hatukulijali kwani kuzaliwa njiti haina maana hata akili huna na ndio maana mpaka sasa tunafanya vizuri," alisema Humba.
Kutokana na hayo, alisema kuwa Mfuko umejipanga kuhakikisha unatoa elimu ya kutosha kwa umma ili huduma zinazotolewa na Mfuko zielewe na wananchi wote lakini pia wanachama wa Mfuko huo waweze kupata huduma za matibabu kwa heshima inayotakiwa.
No comments:
Post a Comment