Monday, February 13, 2012

NHIF toeni motisha kwa watumishi bora-Prof. Shija


Mjumbe wa Bodi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Prof. Shija
 Na Mwandishi Wetu

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umetakiwa kuanzisha mpango wa kutoa tuzo na motisha kwa watumishi bora ili kutoa changamoto kwa watumishi wengine.

Hatua hiyo itawezesha kufanya kazi kwa ushindani lakini pia kuongeza ufanisi na hatimaye Mfuko kuendelea kufanya vizuri katika utoaji wa huduma zake kwa wanachama.

Mwito huo ulitolewa Dar es Salaam juzi na Mjumbe wa Bodi ya Mfuko huo, Prof. Joseph Shija katika sherehe ya kukaribisha mwaka 2012 ya watumishi wa Mfuko huo.

Prof. Shija alisema kuwa Watanzania wana matumaini makubwa na Mfuko huo katika kuboresha na kuhakikisha afya bora kwa kila Mtanzania na uhakika kwa kupata matibabu kwa kadi unapatikana hivyo kuna kila sababu ya watumishi wake kufanya kazi kwa ushindani mkubwa ili kukabiliana na changamoto hiyo.

"Ili hili liweze kufanikiwa ni lazima watumishi mfanye kazi kwa uadilifu na si kwa mtindo wa unung'unikaji lakini pia hakikisheni mnajenga utamaduni wa kutoridhika na kiwango cha elimu mlichonacho, jiendelezeni kila mnapopata nafasi hiyo ili kuongeza zaidi ufanisi wa kazi zenu ndani ya shirika," alisema Prof. Shija.

Aidha aliwataka watumishi kutoridhika na viwango vya elimu walivyonavyo hivyo wajenge utamaduni wa kujiendeleza wakati wanapopata fursa hiyo ili kuufanya Mfuko huo kuwa na watumishi wenye ubora na wanaoweza kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.

Alisema kuwa Mfuko katika kipindi hiki cha miaka 10 tangu uanzishwe, umevuka mawimbi ya kila namna na kufanya mambo makubwa katika utoaji wa huduma zake ambayo yanazivuta hata nchi zingine kuja kujifunza jambo ambalo ni kuupongeza uongozi wa Mfuko huu.

Akizungumza katika sherehe hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Emanuel Humba alisema kuwa pamoja na mafanikio makubwa na ya kujivunia yaliyofikiwa na Mfuko huo, lakini bado kuna changamoto ikiwemo ya elimu kwa wananchi hasa katika kipindi hiki ambacho Mfuko unasimamia pia Mifuko ya Afya ya Jamii (CHF).

Humba alisema kuwa changamoto nyingine ni huduma kwa wananchama wa Mfuko ambapo malengo ya Mfuko ni kuhakikisha kila mwanachama anapata huduma za matibabu kwa heshima kubwa kwa kuwa wamelipia.

Hata hivyo, Humba hakusita kuwaomba watumishi hao kutojiona wanyonge mbele za umma kwa kuwa mambo yaliyofanywa na Mfuko mpaka sasa ni makubwa ikilinganishwa na namna ulivyoanza ambapo baadhi ya watu walikuwa wakiwakatisha tamaa watumishi wa mfuko huo.

"Mtakumbuka tulianza na changamoto nyingi sana lakini sasa tuko pazuri...watu walidiriki kutuita 'njiti' lakini hilo hatukulijali kwani kuzaliwa njiti haina maana hata akili huna na ndio maana mpaka sasa tunafanya vizuri hivyo hakuna sababu ya kujisikia wanyonge," alisema Humba.

No comments:

Post a Comment