Monday, February 13, 2012

Wanachama NHIF watibiwe kwa heshima-Humba

Na Mwandishi Wetu

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema kuwa unafanya kila linalowezekana ili kuhakikisha unakabiliana na changamoto zilizopo hasa za huduma kwa wanachama wake ili hatimaye waweze kupata huduma kwa heshima inayostahili.

Umesema kuwa wanachama wa Mfuko huo wanastahili kupata huduma kwa heshima kwa kuwa huduma hiyo wameilipia.

Akizungumza na watumishi wa Mfuko huo Dar es Salaam juzi wakati wa sherehe ya kukaribisha mwaka 2012, Mkurugenzi Mkuu, Emanuel Humba alisema kuwa pamoja na mafanikio makubwa ya kitaifa na kimataifa lakini bado kuna kila sababu ya kuhakikisha watumishi hao wanafanya kazi bila kuchoka kwa ajili ya wanachama na Watanzania kwa ujumla.

"Ni wazi kuwa ukiangalia tulikotoka ni kugumu zaidi, tumevuka mawimbi ya kila aina na sasa Mfuko uko pazuri na umefanikiwa kuboresha mambo mbalimbali yakiwemo mafao ya wanachama, lakini mafanikio haya yasitufanye tukaridhika, tufanyeni kazi bila kuchoka huku tukiweka mbele maslahi ya Watanzania," alisema Humba.

Alisema kuwa Mfuko huo ulianza na wanachama 164,000 mwaka 2001 lakini idadi ya wanachama imekuwa ikiongezeka kwa wastani wa asilimia 14.5 kila mwaka ambapo mpaka Desemba mwaka jana Mfuko ulikuwa na wanachama 473,771 ikiwa na maana ya wanufaika 2,509,583.

Humba pia alisema kuwa Mfuko pia umejipanga katika kuhakikisha elimu inaenezwa kwa wanachama wote wa Mfuko na wananchi kwa ujumla kwa lengo la kuzifahamu haki zao wakati wa kupata huduma lakini pia mambo ya kuzingatia kama wanachama.

Aidha alisema kuwa Mfuko umedhamiria kusogeza huduma kwa wanachama wake ambapo umeanzisha ofisi katika baadhi ya Mikoa na lengo kubwa ni kuwa na ofisi katika Mikoa yote.

Naye Mjumbe wa Bodi, Bw. Gratian Mukoba aliupongeza uongozi wa Mfuko huo kwa kuwa imara na kuufikisha hapo ulipo ukiwa na mafanikio makubwa.

Kutokana na hali hiyo, aliutaka kuendekea kuwa imara na kutoyumbishwa kwa namna yoyote ili wanachama wake waendelee kunufaika na huduma bora zinazotolewa mpaka sasa.

"Tunatambua uongozi wa Mfuko ni imara na ndio maana umeweza kuvuka mawimbi yote yaliyokuwepo na leo hii tunaona wanachama wakinufaika na mafao yaliyopo...yawezekana uimara huu umewezeshwa na aliyekikamata chombo hiki ambaye kwa kweli tuna kila sababu ya kumpongeza, uimara wake ndo unaowezesha hata haya mafanikio yaliyopo sasa," alisema Mukoba.


Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya akitoa nasaha kwa wafanyakazi.
 Kutokana na hayo, alitoa mwito kwa watumishi wa Mfuko huo kutanguliza maslahi ya Watanzania wakati wa kutimiza majukumu yao.

No comments:

Post a Comment