Bei ya mafuta juu tena
Na Grace Michael
FURAHA ya watumiaji wa mafuta kwa bei bidhaa hiyo kuteremshwa kwa asilimia 9 na kusababisha wafanyabiashara wa mafuta kugoma, ilikuwa ya muda tu na
sasa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) imetangaza kupanda tena kwa kati ya asilimia 5 na 6 kuanzia leo.
Bei hizo zilizotangazwa na mamlaka hiyo Dar es Salaam jana na kutanza kutumika leo, zimeongezeka kwa asilimia 5.51 kwa petroli, dizeli (6.30%) na mafuta ya taa 5.30%. Hivyo, petroli itauzwa kwa sh. 100.34 zaidi ya bei elekezi ya iliyoleta kizaazaa wiki iliyopita, dizeli kwa sh. 120.47 zaidi na mafuta ya taa kwa sh. 100.87.
Akitangaza mabadiliko ya bei hizo, Meneja Biashara wa Mazao ya Petroli wa EWURA, Mhandisi Godwin Samwel, alisema kuwa kupanda kwa bei hizo kunatokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na kuendelea kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na dola ya Marekani.
Alisema kuwa kwa viwango vya bei vilivyotumika katika chapisho hilo jipya, bei katika soko la dunia zimepanda kwa wastani wa asilimia 5.42 huku thamani ya shilingi ya Tanzania ikishuka kwa shilingi 47.12 ambayo ni sawa na asilimia 296 kwa dola moja ya Marekani.
Bei ya mafuta ya petroli kwa Mkoa wa Dar es Salaam na bei za awali kwenye mabano ni sh. 2,114.12 (sh. 2,004), dizeli 2,031.31 (sh. 1,911) huku mafuta ya taa yakiwa sh. 2,005.40 (sh. 1,905) kwa lita.
Hata hivyo, Mhandisi Samwel alisema kuwa bei hiyo ina unafuu kutokana na kutumika kwa kanuni mpya ya ukokotoaji wa bei, na iwapo ingetumika kanuni ya zamani, petroli kwa Dar es Salaam ineuzwa kwa sh. 2,298.33, dizeli 2,213.36 na mafuta ya taa kwa sh. 2,188.89.
Alisema kuwa kwa mujibu wa sheria ya mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko, EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta kwa lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta.
Aidha alisema kuwa vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za mafuta katika mabango yanayoonekana yakionesha bei, kwa kuwa ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vyema kwa wateja.
“Jambo jingine tunalosisitiza ni wanunuzi kuhakikisha wanapata stakabadhi ya malipo inayoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta na bei kwa lita, ili kuwapata wanaouza mafuta kwa bei ambazo hazijapangwa na mamlaka yetu,” alisema.
Hata hivyo EWURA ilisema kuwa bei hizo zinaweza kushuka baadaye endapo hapatakuwa na kupanda zaidi kwa dola ya Marekani au kushuka kwa shilingi ya Tanzania.
Hali ya mafuta
Alisema kuwa hali ya mafuta nchini kwa sasa ni nzuri kwa kuwa mwishoni mwa wiki mafuta yaliuzwa kwa wingi sana vituoni ambapo kwa siku ya Ijumaa jumla ya lita milioni 9.5 ziliuzwa kutoka visima kwenda vituoni na Jumamosi ziliuzwa lita milioni 4.9 na meli zinaendelea kuingia.
Ongezeko hili linakuja siku chache baada ya kumalizika mgogoro uliokuwepo wa wafanyabiashara wa mafuta kugoma kuuza mafuta kutokana na kushuka kwa bei za mafuta hatua iliyosababisha EWURA kuifungia leseni ya kuuza mafuta ya petroli, dizeli na taa Kampuni ya BP kwa muda wa miezi mitatu.
No comments:
Post a Comment