Saturday, August 13, 2011

BP yafungiwa leseni kwa miezi mitatu

Na Grace Michael
MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA)imesitisha leseni ya Biashara ya Kampuni ya mafuta ya BP (T)Ltd kwa muda wa miezi mitatu kuuza mafuta ya Petroli, dizeli na mafuta ya taa.
Hatua hiyo imetangazwa jana na Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Bw. Haruna Masebu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi uliofikiwa na bodi kutokana na sakata la mafuta.
Bw. Masebu alisema kuwa kampuni hiyo itaruhusiwa kuuza mafuta ya ndege kwa kuwa EWURA haidhibiti bei za mafuta hayo.
“Tumeamua kusitisha leseni ya BP kwa kuwa wameonekana kutotekeleza agizo ambalo tulilitoa la kuwataka warejeshe huduma za kuuza mafuta kwa wananchi na hata utetezi waliouwasilisha kupitia mwanasheria wao bado haukukidhi matakwa hivyo hawaruhusiwi kuuza mafuta hayo niliyoyataja,” alisema Bw. Masebu.
Alisema kuwa kitu kingine ambacho BP wataruhusiwa kukifanya ni kuuza mafuta yake yaliyoko kwenye maghala yake kwa kampuni zingine za jumla na uuzaji huo utafanyika chini ya usimamizi wa EWURA.
Alisema kuwa wameruhusu hilo ili kunusuru mafuta waliyonayo kutoharibika kwa kuwa muda wa miezi mitatu ni mkubwa ambao unaweza ukasababisha mafuta yaliyopo kuharibika.
“Vituo vya reja reja na vyenye nembo ya BP vitaruhusiwa kuuza mafuta kwa kununua mafuta kwa wafanyabiashara wengine wa jumla na si kwa BP,” alisema Bw. Masebu.
Mbali na hilo, alisema kuwa bodi ya wakurugenzi wa mamlaka hiyo wameagiza Mtendaji Mkuu na Mwenyekiti wa kampuni ya BP kufikishwa mahakamani kwa kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).
Akizizungumzia kampuni zingine za mafuta ambazo zilipewa amri ya kurejesha huduma ambazo ni Oilcom (T) Ltd, Camel Oit (T)Ltd na Engen Petroleum (T) Ltd, alisema kuwa pamoja na kurekebisha kwa kiwango Fulani huduma zao, EWURA itawaandikia onyo kali la kuwaonya kutorudia tabia waliyoionesha ambayo ni kinyume na sheria.
“Katika onyo hilo tutawataka wauze mafuta kwa watu wote bila ubaguzi na amri hii tutaifuatilia kwa ukaribu na ikibainika wamekiuka hatua kali zitachukuliwa dhidi yao mara moja,” alisema Bw. Masebu.
Aidha alisema kuwa mamlaka hiyo itaendelea kuangalia mfumo mzima wa mafuta yanayoingia bandarini na kufuatilia bei zinazouzwa vituo kama zinafanana na zile zilizotangazwa.
Alisema kuwa kwa sasa hali ya huduma ya mafuta inaendelea vyema na kutokana na kurejea kwa huduma hiyo, amewataka wananchi kuachana na utamaduni ambao umejengeka wakati huduma ya mafuta ilipoyumba ya kununua mafuta kwenye vidumu kwa kuwa utaratibu huo unahatarisha usalama hata wa vituo vyenyewe.
“Tunatarajia sasa kutoona wananchi wakinunua mafuta kwenye vidumu kama ambavyo ilifanyika wakati hali ilipokuwa mbaya ya mafuta ambapo wengi magari yao yalizimika,” alisema.
Agosti 9, mwaka huu EWURA ilitoa agizo kwa kampuni hizo nne ambazo zilionekana kinara wa mgomo ambapo zilitakiwa zianze mara moja kutoa huduma hiyo, kuacha vitendo vinavyozuia uuzwaji wa mafuta na vitoa maelezo kwa maandishi kwa kuvunja sheria ya petrol.
Hata hivyo, kampuni ya BP ilionekana kukaidi amri halali ya mamlaka hiyo hatua iliyosababisha kusitishwa kwa leseni yake.

No comments:

Post a Comment