Na Grace Michael
KUMEKUWA na malumbano ya hapa na pale kuhusu maandamano ambayo yamekuwa yakifanywa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),kwa lengo la kuishinikiza serikali kutatua baadhi ya matatizo ambayo yanajitokeza kwa nyakati tofauti.
Hoja ya maandamano imekuwa gumzo na wengine kuipa maana nyingine kwa lengo la kuwapotosha wananchi na kuwaacha njiapanda ili wasijue cha kufanya.
Kwa mujibu wa kamusi, maandamano ni mfuatano au msururu wa watu wengi wanaotembea kuelekea mahali ili kutimiza lengo Fulani.
Mbali na maana hiyo, maandamano yamekuwa yakifanywa kwa lengo la kufikisha ujumbe Fulani kwa serikali ili iweze kuufanyia kazi, hivyo kutokana na matatizo lukuki yanayoikabili nchi kwa sasa, wananchi ni lazima waitumie njia hiyo ili kilio chao kifanyiwe kazi.
Hivi karibuni hoja ya maandamano ilipamba moto bungeni ambapo wabunge wa CCM wamefikia hatua ya kugawanyika kwa maana ya baadhi kuunga mkono maandamano yanayofanywa na CHADEMA huku wengine wakipinga maandamano hayo kwa madai kuwa yanalenga uchochezi hasa wa kuing’oa serikali iliyopo madarakani.
Nilipata fursa ya kuwasikiliza baadhi ya wabunge wa CCM kuhusu hoja hiyo ambapo baadhi walitoa angalizo kwa serikali kwa kuitaka kutekeleza yanayoombwa na wananchi hasa wakati wa maandamano kwa kuwa dawa ya kuondokana na maandamano ni kumaliza kero zinazowakabili.
Mbunge ambaye aliunga mkono maandamano alikuwa ni Mbunge wa Kahama, Bw. James Lembeli ambaye kwa ufupi alisema kuwa “Wabunge tuacheni kunyoosheana vidole bungeni kuhusiana na tatizo la migomo na maandamano yanayofanywa katika maeneo mbalimbali na badala yake tuishinikize Serikali kushughulikia kero zinazosababisha matatizo hayo,”.
Alikwenda mbali zaidi kwa kuitaka serikali kusoma ujumbe ulioko kwenye mabango na kuufanyia kazi kwani hakuna njia nyingine inayoweza kufanywa na wananchi kama serikali haitimizi wajibu wake.
Mbali na Lembeli, tumemsikia Mbunge wa Ludewa Bw. Deo Filikujombe ambaye naye aliweka wazi msimamo wake hivi karibuni bungeni kuwa angehamaisha wananchi kuandamana endapo serikali isingeongeza fedha katika Wizara ya Uchukuzi.
Wakati wabunge hao wakiunga mkono maandamano yanayofanywa na CHADEMA, wapo baadhi ya wabunge wa CCM wanaoyapinga kwa nguvu zote na ukiachana na wabunge hao, tumemsikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Fredrick Werema bungeni wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, alisema kuwa suala la maandamano ni haki ya kikatiba, lakini pia moja ya masharti ya chama cha siasa kinapoandikishwa, ni kuhakikisha hakitumii njia ya mapambano katika kufikia malengo.
Werema alikwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa kuna haja ya kufanya marekebisho ya kisheria yatakayodhibiti maandamano yanayofanywa na vyama vya siasa nchini.
Kauli hii ya Jaji Werema inanishangaza kwa kuwa hakuna maandamano yoyote ambayo yamefanywa na CHADEMA yakiwa na lengo la kuchochea bali ni maandamano ya amani ambayo yamebeba ujumbe kwa serikali, hivyo kinachotakiwa ni serikali kuuchukua ujumbe huo na kuufanyia kazi.
Hakuna namna hasa kwa wakati kama huu ambao maisha yamekuwa ni magumu kwa wananchi wa kawaida kutokana kupanda kwa gharama za maisha, kutokuwepo na nishati ya umeme ya uhakika na sasa kuwepo kwa tatizo kubwa la ukosefu wa mafuta hali inayosababisha kuongeza ugumu wa maisha.
Wananchi wanapozidiwa na kunakuwa na chama makini kinachotambua tatizo hilo ni lazima kihamasishe maandamano ili serikali isikie kilio hicho.
Ni vigumu kwa viongozi wetu mlioko madarakani kuona ugumu wa maisha uliopo hivi sasa kwa kuwa mahitaji mengi kama mafuta ya magari, muda wa maongezi, bili za maji, umeme na mahitaji mengine mengi mnalipiwa na serikali hivyo hali hiyo inawafanya kutoona ni namna gani wananchi huku nje wanatesema na ndio maana hata Jaji Werema alifikia hatua ya kutaka kufanyike mabadiliko ya sheria ili maandamano yaminywe.
Dawa ya kumaliza maandamano ni serikali iliyoko madarakani kushughulikia matatizo yaliyopo, wananchi wako katika hali ngumu, thamani ya shilingi imeshuka, gharama za maisha zimepanda hivyo wananchi wako njia panda na ndio maana wanaunga mkono maandamano yanayoitishwa na vyama vya upinzani.
Wananchi wanakerwa na kikundi cha watu wachache kuishi maisha yenye neema huku mabilioni ya wananchi wakitaabika.
Hakuna anayependa kuacha shughuli zake na kuingia mtaani kuandamana bali hali halisi iliyopo ndiyo inayowafanya wananchi kuingia mtaani kwa lengo na kuiamsha serikali ione matatizo yaliyopo.
Acheni maandamano yawepo na hoja ya maandamano ya CHADEMA isipotoshwe kwa kuwa haina lengo la kuleta machafuko bali ni kutaka kuwaamsha viongozi walioko usingizini ili washughulikie kero za wananchi.
Mungu Ibariki Tanzania
0755-23-42-57
Mwisho.
No comments:
Post a Comment