Na Grace Michael
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Freeman Mbowe amesema, endapo madiwani waliovuliwa uanachama na kupoteza nafasi za udiwani katika kata mbalimbali za jijini Arusha wanaingia kwenye vikao vya baraza la madiwani, kitakuwa ni kitendo cha kushangaza na cha kihuni.
Alisema kuwa hatarajii kusikia madiwani hao waliopoteza nafasi zao kutokana na maamuzi ya Kamati Kuu ya chama kuona wakiingia vikaoni.
“Kwanza nitashangaa sana kuona kama Mkurugenzi anawaruhusu kuingia kwenye vikao vya madiwani na wakati taarifa tena kwa barua amekabidhiwa na hao wahusika wenyewe tumewapa...kama wanafanya hivyo itakuwa ni kuendeleza vitendo vya kihuni lakini kama chama tutafuatilia na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo,” alisema Bw. Mbowe.
Bw. Mbowe aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Majira kwa njia ya simu akiwa safarini kutoka Arusha kwenda Dodoma, alisema kuwa endapo kitendo hicho kinafanyika, watafuatilia na kuona namna ya kulishughulikia.
“Kama kweli watakuwa wanaingia na Mkurungenzi anawaruhusu, basi itakuwa ni kuendeleza yale waliyokuwa wamekusudia tangu awali na kitakuwa ni kitendo cha ajabu na cha kihuni tena na cha utovu wa nidhamu kwa kuwa taarifa wanazo tena kwa maandishi lakini pia kwa upande wa hao wahusika walikuwepo siku wanavuliwa uanachama...lakini tutafuatilia,” alisema Bw. Mbowe.
Bw. Mbowe alifikia hatua ya kusema hayo baada ya kuhojiwa na Majira kuhusu kitendo cha madiwani hao kuendelea kuingia kwenye vikao vya kamati za madiwani kwa kutumia jina la chama hicho huku kikiwa kimewatimua uanachama.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo kwenye vyombo vya habari, madiwani hao wanadaiwa kuhudhuria kikao cha kamati ya fedha na wakaahidi kuendelea kuhudhuria vikao hivyo mpaka Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda atakapotangaza nafasi zao kuwa wazi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Arusha alikanusha kupokea barua ya kuvuliwa kwa madiwani hao.
No comments:
Post a Comment