Na Grace Michael
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), NEC, Dkt. Makongoro Mahanga ameingilia kati mgogoro uliopo kati ya wabunge wa Dar es Salaam na Meya wa Jiji hilo, Dkt. Didas Masaburi kwa kuzitaka pande zote kuachana na malumbano yaliyopo baina yao.
Malumbano yaliyopo kati ya Dkt. Massaburi na wabunge wa Dar es Salaam ni kuhusu sakata la uuzwaji wa Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA), sakata ambalo liliibuka bungeni wiki iliyopita hali iliyosababisha Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda kuzitaka mamlaka za uchunguzi kuingilia kati.
Dkt. Mahanga ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Segerea jijini Dar es Salaam, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Majira kwa njia ya simu kutoka mkoani Tanga, ambapo alisema kuwa kuendeleza malumbano hayo ni kuendelea kukiumiza CCM.
“Ningependa kuwashauri wabunge wenzangu wa Dar es Salaam na Meya kuachana na haya malumbano ambayo sasa wanayafanya kupitia vyombo vya habari, kuendelea na haya malumbano kwa njia hii ni kukiumiza chama na ukizingatia suala lenyewe hili liko kwenye mikono ya vyombo vya uchumguzi hivyo wasubiri vyombo hivyo vifanye kazi yake na majibu yatapatikana,” alishauri, Dkt. Mahanga.
Mbali na kuwataka kuachana na malumbano hayo, Dkt. Mahanga alitumia mwanya huo kumwomba Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam kuwakutanisha wabunge hao na Dkt. Massaburi kwa lengo la kumaliza tofauti zao kichama ili wote kwa pamoja waendelee na juhudi za kukijenga chama.
Mwishoni mwa wiki baada ya wabunge kulichachamalia suala la uuzwaji wa UDA kwa njia ambazo walidai zimegubikwa na ufisadi, Serikali kupitia Waziri Mkuu iliagiza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kufanya uchunguzi juu ya kashfa hiyo ili hatua zichukuliwe kwa viongozi waliohusika.
Wakati maagizo hayo yakitolewa, wabunge wa Dar es Dar es Salaam walitoa tamko wakitaka wote waliohusika akiwemo Meya Dkt. Massaburi kusimaishwa kazi wakati uchunguzi ukifanyika.
Kwa upande wake Dkt. Massaburi wakati akijibu tuhuma hizo aligoma kujiuzuru wadhifa wake akidai kuwa yeye ndiye aliyebaini ufisadi katika shirika hilo baada ya kuingia madarakani.
Dkt. Massaburi alikwenda mbali na kusema kuwa wabunge wa Dar es Salaam wanaotaka ajiuzuru ni wale wanaosimamia miradi inayolalamikiwa na wananchi hivyo wanataka ajiuzuru ili isikaguliwe.
No comments:
Post a Comment