Tuesday, December 20, 2011

Hatutalipa madai yasiyokuwa na taarifa-NHIF

Na Grace Michael, Morogoro

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya umesema kuwa hautakuwa tayari kulipa fedha za tele kwa tele kwa Halmashauri ambazo zitashindwa kuwasilisha madai yake yakiwa na taarifa muhimu kama majina ya wakuu wa kaya.

Imesema ni lazima madai yanayowasilishwa kwa ajili ya kulipwa fedha hizo yawe na majina hayo na si vinginevyo.

Hayo yalisemwa mjini hapa na mmoja wa watoa mada wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Rehani Ahuman wakati akijibu maswali ya waratibu waliohudhuria kongamano la kwanza la mfuko huo ambao walitaka kufahamu umuhimu wa kuambatanisha majina hayo kwenye madai.

"Jamani ni lazima tufike mahali tufanye kama inavyotakiwa, wapo ambao wameweza na kama hao wameweza wote mnaweza kufanya hivyo, kumbukeni hizi ni fedha ambazo haziwezi kulipwa bila kuwepo na utaratibu unaoeleweka na haya majina yatasaidia katika mambo mengi," alisema Rehani.
Alisema kuwa pamoja na sasa kuhitajika majina hayo kwenye madai yao, lakini kwa hapo baadae zitahitajika taarifa zaidi kwa kuwa lengo ni kujiridhisha na madai yanayodaiwa.

Alisema kuwa lengo la CHF ni kuhakikisha mwananchi aliyejiunga anaona umuhimu au faida ya mfuko huo hivyo bila kuwa na umakini katika uendeshaji wake lengo hilo haliwezi kukamilika.

Rehani pia alitumia mwanya huo kuwataka waratibu na wahasibu wa CHF kuhakikisha wanakuwa na akaunti za mfuko huo katika maeneo yao kwa kuwa hata Serikali imekubaliana na kuwepo kwa akaunti hizo.

"Tunataka ifikapo Machi mwakani kila Halamshauri iwe na akaunti ya CHF na hii itawezesha ukaguzi na ufuatiliaji wa fedha za mfuko huu na hasa namna zinavyotumika," alisema Rehani.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka waratibu kutambua kuwa kazi au jukumu walilonalo kwenye mfuko huo ni kubwa na linalohitaji kujituma bila kuweka maslahi yao mbele na badala yake waweke maslahi ya Watanzania hasa kuhakikisha huduma za afya zinakuwa bora zaidi.

"Waratibu mnatakiwa kutambua kuwa kazi mlinayo ni kubwa na wala msiendekeze malalamiko wala kujiuliza utanufaikaje, tuifanyeni hii kazi ili hata vizazi vijavyo vije vitambue kuwa kuna watu kweli walifanya jambo kwa maslahi ya Watanzania," alisema Rehani.

Kongamano hilo ambalo lina washiriki zaidi ya 300 kutoka katika halmashauri zote nchini lina lengo la kujadili mambo mbalimbali yanayohusiana na mfuko huo ili hatimaye yaweze kufikiwa mafanikio yanayotarajiwa ya kila mtanzania kuwa na bila ya afya.

No comments:

Post a Comment