Sunday, May 29, 2011

Mambo ya Funcity

MKURUGENZI wa ufukwe wa Funcity uliyopo Kigamboni, Dar es Salaam, Bw. Hasan Rizvi akielezea waandishi wa habari namna uwekezaji uliofanywa katika ufukwe huo ambapo kuna michezo ya aina mbalimbali, kushoto ni Bw. Jaffer Jaffer (Picha na Grace Michael).

Dkt. Mahanga aja na mkakati wa uhamasishaji

Na Grace Michael

MBUNGE wa Jimbo la Segerea Dkt. Makongoro Mahanga ameahidi kuendesha kampeni ya uhamasishaji kwa wananchi ili wajenge tabia ya kufanya kazi kwa kujituma na kuondokana na dhana iliyojengeka ya kulaumu serikali katika kila jambo.

Dkt. Mahanga aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na majira namna alivyojipanga katika kuwatumikia wananchi wa jimbo lake ili waweze kujikwamua na hali ngumu ya maisha.

"Kwanza kinachotakiwa kufanyika ni kuwahamasisha wananchi ili wajenge utamaduni wa kujituma katika kazi...maendeleo hayawezi yakamfuata mwananchi ambaye hajitumi na wala hafuatilii hata fursa zilizopo, nitafanya kila linalowezekana ili wananchi wa jimbo langu watambue kwanza umuhimu wa kujituma na baada ya hapo tutafanikiwa katika kujikomboa," alisema Dkt. Mahanga.

Alisema kuwa hata kama Serikali ingetoa mabilioni ya fedha kwa wananchi lakini bila kuwepo kwa dhana ya uwajibikaji wa kujituma katika shughuli za uzalishaji hakuna kitu kitakachofikiwa hivyo akasisitiza kuwepo kwa ubunifu na kuongeza bidii katika shughuli za uzalishaji.

"Wapo wananchi wanatambua umuhimu wa kujituma katika kazi na ndio maana wanafanikiwa na kuwa katika hali nzuri ya maisha lakini wapo ambao bado hawajaelewa umuhimu wa kufanya kazi hivyo suala hili nitalieleza kwa wananchi ili walielewe hata serikali inapoweka nguvu yake kunakuwa na matunda mazuri," alisema Dkt. Mahanga na kuongeza.

Alitumia mwanya huo kuwaomba wananchi kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kujikwamua lakini akasisitiza umuhimu wa kujiunga kwenye vikundi ambavyo vinarahisisha upatikanaji wa mitaji au mikopo kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo.

"Kidole kimoja huwa hakivunji chawa hivyo vikundi vina faida yake na umuhimu mkubwa kwanza hata namna ya kusaidiwa inakuwa ni rahisi kwa kuwa serikali haiwezi kuona mtu mmoja mmoja," alisema.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa ana mpango wa kukutana na makundi ya aina mbalimbali wakiwemo vijana, akina mama na wengine ili kuona ni namna gani makundi hayo yanaweza kujikomboa katika umasikini na kuwa katika hali nzuri ya maisha kama sera ya Chama Cha Mapinduzi inavyotaka.

Akizungumzia kero zilizoko jimboni mwake zikiwemo za barabara, maji na zingine alisema ziko katika hatua ya kutatuliwa na baadhi yake tayari fedha zimetengwa kwa ajili ya kuzitatua.

Friday, May 27, 2011

Kamati yataka mkazo fedha za dawa

Na Grace Michael

KAMATI ya Bunge ya Huduma za Jamii imeitaka Serikali kuweka mkazo kwa kutenga fedha zinazotosheleza mahitaji ya ununuzi wa dawa ili kuondokana na adha ya ukosefu wa dawa katika vituo vya kutolea huduma.

Imesema bila wananchi kuwa na afya zilizoimarika hakuna maendeleo yoyote yatakayofikiwa hivyo ni lazima eneo la ununuzi wa dawa liwekewe mkazo kwa kuwa na fedha za kutosha.

Mapendekezo hayo yalitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bi. Magreth Sitta wakati kamati yake ilipotembelea Bohari ya Dawa (MSD) na kukagua shughuli zinazofanywa na bohari hiyo.

"Bila kuwa na afya njema taifa haliwezi kusonga mbele ni lazima akina mama wapate huduma nzuri za matibabu pamoja na watoto lakini pia wananchi kwa ujumla hivyo kwa namna tulivyoelezwa na kuona hali halisi ya ufinyu wa bajeti unaofanya bohari kushindwa kutimiza malengo yake ni lazima serikali iangalie eneo hili kwa umakini," alisema Bi. Sitta.

Bi. Sitta aliweka bayana kuwa MSD inashindwa kufikia lengo la upatikanaji wa dawa kwa asilimia 100 kutokana na chgangamoto zilizopo kubwa ikiwa ni ukosefu wa fedha.

Kamati hiyo pia ilipata fursa ya kuhoji namna ufuatiliaji wa dawa unavyofanyika kutoka MSD hadi kwa walaji kwa lengo la kukabiliana na wizi wa dawa ambao unadaiwa kufanyika katika maeneo mbalimbali.
Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa MSD, Bw. Joseph Mgaya aliweka wazi kuwa kazi ya bohari hiyo ni kununua, kuhifadhi na kusambaza dawa hizo na haina jukumu la kufuatilia namna dawa hizo zinavyotumika katika maeneo husika.

"MSD haina jukumu la kugagua dawa hizo baada ya kumaliza makabidhiano na wahusika au waombaji...kwa upande wetu tuna mifumo ambayo iko wazi ambapo mwombaji huomba na kukabidhiwa dawa kwa maandishi hivyo kama kuna wizi wa dawa unafanyika baada ya dawa hizo kutoka mikononi mwetu hatuna jukumu hilo," alisema Bw. Mgaya.

Akizungumzia kiwango cha upatikanaji wa dawa kwa sasa, alisema ni asimilia 80 inayopatikana na imekuwa vigumu kwa bohari hiyo kufikisha asilimia 100 kutokana na mazingira inayokumbana nayo yakiwemo ya ufinyu wa bajeti lakini pia utegemezi wa kununua dawa nje kwa asilimia 80.

Bw. Mgaya pia alieleza namna bohari inavyolipa kodi ya foroda na ya ongezeko la thamani kwa vifaa vya hospitali vinavyoingizwa nchini na idara hiyo imekuwa ikilipa adhabu ya asilimia 120 kwa mifuko ya plastiki malipo ambayo yanaongeza gharama kubwa kwa idara.

"Tunaomba kamati ishauri serikali kufuta malipo ya kodi kwa vifaa vya hospitalini na adhabu kwa mifuko ya kuwekea dawa," aliomba Bw. Mgaya.

Pia alitumia mwanya huo kueleza namna sheria ya manunuzi inavyokuwa kikwazo katika mchakato wa ununuzi wa dawa ambapo alisema kuwa ununuzi wa dawa za kuokoa maisha ya wananchi unatakiwa kutofautishwa na manunuzi ya huduma zingine hivyo akaomba kuangaliwa kwa suala hilo.

"Suala jingine ni hali isiyoridhisha ya utunzaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma ambapo dawa nyingi zinaharibika kutokana na utunzaji mbovu hivyo naiomba kamati kuishauri serikali ijenge miundombinu itakayotunza ubora wa dawa," alisema Bw. Mgaya.

Akizungumzia kuongezeka kwa madeni alisema kuwa hadi Aprili mwaka huu, kiwango cha deni la serikali kimeongezeka na kufikia sh. bilioni 40 na sehemu kubwa ni dawa za mradi msonge.

MSD kwa sasa inasambaza dawa hadi kwenye vituo vya kutolea huduma katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani na Shinyanga hatua iliyopongezwa na wananchi kutokana na kufika dawa hizo kwa wakati.

Thursday, May 26, 2011

Mauaji ya Tarime yasiwe mtaji wa kisiasa

Na Grace Michael

HAKUNA asiyekumbuka kilichotokea alfajiri ya Mei 16 mwaka huu, pale Nyamongo
wilayani Tarime ambapo watu watano waliuawa na wengine kujeruhiwa katika mapambano kati ya Polisi na wananchi waliodaiwa kuvamia mgodi wa North Mara kwa lengo la kupora mawe ya dhahabu.

Tukio hilo halikuwa zuri machoni pa Watanzania kwa kuwa limeacha simanzi kwa  ndugu jamaa na marafiki wa marehemu, lakini pia limepoteza nguvu kazi kwa hao waliouawa katika mapambano hayo.

Nina hakika kwamba tukio hilo limesababishwa na baadhi ya watendaji waliopewa  mamlaka ya kushughulikia matatizo ya wananchi wa eneo hilo kutotimiza wajibu wao ipasavyo.

Vitendo vya wenye mamlaka kutotimiza mahitaji ya wananchi vimejenga chuki miongoni mwa jamii hatua inayosababisha wananchi wengi sasa kujikuta wakijichukulia sheria mkononi hatua ambayo huwa ni mbaya kwa kuwa huambatana na athari kama zilizotokea huko Tarime.

Utakubaliana na mimi kuwa matukio yote yanayoendelea kutokea Tarime tangu kuuawa
kwa wananchi hao yanatokana na wananchi kuichoka Serikali yao kwa kuwa
imeshindwa kutatua kwa muda mrefu madai yao.

Itakumbukwa baada ya kufanyika mauaji hayo, Mbunge wa Jimbo la Tarime Bw.
Nyambari Nyangwine pengine kwa kutimiza wajibu wake kwa wananchi anaowawakilisha
alimua kufunga safari kwa lengo la kwenda kuzungumza na wananchi wake lakini
alichokipata huko anakijua mwenyewe.

Wananchi hao walisikika waziwazi wakisema ‘Hatumtaki mbunge wala Serikali’ sasa
maneno hayo yanaishara mbaya kwa taifa letu kwa kuwa Serikali ndio huwa chombo
ambacho kinaheshimika na kila mtu hivyo kuona wana Tarime wakiikataa hadharani
ni mwanzo mbaya.

Mbali na kitendo cha wananchi hao kumkimbiza mbunge wao na kuushambulia msafara wake, lakini pia wananchi hao wameonekana kuendelea kukereka na mchakato
unaofanywa hasa wa kufikia hatua ya maziko ya ndugu zao.

Tayari mgogoro uliibuka wakati wa uchukuaji maiti ambapo Polisi walidaiwa kuchukua maiti hizo bila ridhaa ya ndugu hatua inayozidi kuimarisha chuki miongoni mwa wananchi wa Tarime lakini pia kutokana na mgogoro huo, umesababisha baadhi ya wabunge wa CHADEMA na makada wengine kuwekwa rumande.

Matukio yote haya yasipoangaliwa kwa umakini, yataleta mgogoro wa kudumu wilayani humo hatua itakayowafanya wananchi wa wilaya hiyo kuishi bila amani.

Ni wakati sasa umefika kwa Serikali kuketi kitako na kuona ni namna gani matatizo hayo yanafanyiwa kazi na hatimaye wananchi hao waweze kuishi kwa amani na wafurahie uwekezaji uliofanywa kwenye eneo lao.

Ni ukweli usiopingika kuwa amani haiwezi ikawepo wakati wananchi wamezama kwenye
tope la ufukara huku wakiona rasilimali zilizopo katika maeneo yao zikitumika bila wao kunufaika nazo.

Nadhani mahitaji makubwa ya wana Tarime ni kuwezeshwa kwa kupewa maeneo yatakayowasaidia wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao za kiuchumi lakini suala hili limekuwa gumu katika utekelezaji wake.

Kutotekelezwa kwa suala hilo ndiko kulichochea wananchi hawa kufanya maandamano ambayo ukiyaangalia kwa umakini unagundua hitaji lao ni kudai haki ambayo wanaona kama imepokwa na wa kuirejesha hawapo.

Mbaya zaidi badala ya kusimamiwa kwa tatizo hilo na kushughulikiwa kwa maana ya kutatua mgogoro uliopo, suala hilo sasa limefanywa kuwa la kisiasa CCM na CHADEMA wanataka kutumia mauaji hayo kuwa mtaji wa kisiasa.

Ninachotaka kusema hapa ni kuwa Serikali sasa ifike pahala imalize tatizo hili ili amani irejeshwe kwa wananchi hawa kwa kuwa bila amani hakuna shughuli yoyote ya maendeleo inayoweza kufanyika katika eneo lao.

Lakini pamoja na hayo, wanasiasa nanyi tumieni nafasi zenu za kisiasa kwa mambo yanayowahusu na si kupandikiza chuki kwa wananchi ambayo baadae inaweza ikasababisha uvunjifu wa amani kwa maslahi yenu badala ya taifa.

Mnayo haki ya kushughulikia matatizo ya wananchi lakini si kwa ajili ya maslahi yenu ya kisiasa kwa kuwa mwisho wake utakuwa ni mbaya.

Kutokana na hayo ni vema sasa sheria za nchi na taratibu zilizopo zikafuatwa ili kuondokana na migogoro ambayo mwisho wa siku inasababisha mauaji kama yaliyotokea kwa wenzetu wa Tarime.

Haki haiwezi kupatikana kwa nguvu bali itapatikana endapo watu wenye hekima na busara zao wataketi kisha kujadiliana na hatimaye kukubaliana namna ya kufanya.

Yaliyotokea Tarime ni aibu na doa kwa nchi yetu kwa sababu itaonekana kuwa haina
misingi ya sheria na utawala bora.

gracemichaelkisinga@yahoo.com

Mwisho.

Wazee Tarime walaani kushambuliwa msafara wa mbunge

Na Grace Michael

SAKATA la kupopolewa mawe kwa msafara wa Mbunge wa Jimbo la Tarime, Bw. Nyambari Nyangwine ambalo lilitokana na tukio la mauaji ya watu watano, limechukua sura mpya baada ya Mwakilishi wa wazee wa kimila jimboni humo Bw. Enock Chambili kulaani kitendo hicho.

Mbali na kulaani kitendo hicho, pia amekemea vitendo vya uchochezi vinavyodaiwa kufanywa na baadhi ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kuwataka wabunge hao watumie muda huo kuhamasisha maendeleo na si uchochezi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana, Bw. Chambili alisema kuwa wananchi wa Tarime hawana utamaduni wa kupiga viongozi wao hivyo kitendo cha kushambulia msafara wa mbunge kilisababishwa na uchochezi wa wanasiasa kwa ajili ya maslahi yao binafsi.

"Wanasiasa ambao hawahusiki jimboni Tarime wasilete uchochezi kwa wananchi na hatimaye wakaturejesha tulikotoka katika mapigano ya kimila, ni vyema wakatumia muda wanaokuja Tarime kuchochea majimboni mwao na si kuleta vurugu kwetu," alisema Bw. Chambili.

Alisema kuwa kinachotakiwa ni kuwaacha wananchi wa Tarime wafanye maamuzi yao wenyewe lakini pia waishi kwa amani na kuendelea na shughuli zao za maendeleo.

Hata hivyo alisema kuwa ni vyema sasa madai ya wananchi wa Nyamongo yakashughulikiwa kwa haraka ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara.

"Ni kweli wananchi wanayo madai yao ambayo yamekuwa ni ya muda mrefu sasa, hawawezi wakavumilia kuona wawekezaji wakinufaika huku wao wakiwa na umasikini mkubwa hivyo kinachotakiwa ni wananchi waendelezwe na wanufaike na uwekezaji na kuboreshewa huduma za kijamii ambazo kimsingi walikubaliana nao," alisema Bw.Chambili.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa suala la kutekeleza madai ya wananchi wa Nyamongo ni la Msingi ili kumaliza migongano iliyopo.

Naye Mbunge wa Jimbo hilo, Bw. Nyangwine aliwataka wanasiasa kutotumia nafasi zao za kisiasa kwa maslahi binafsi ambayo yanasababisha uvunjifu wa amani jimboni mwake.
"Tarime ima mamlaka kalimi kwa maana ya serikali pamoja na uwakilishi hivyo matatizo ya Tarime yanaweza kutatuliwa ndani ya mamlaka hiyo na si wabunge wa chama fulani kuja Tarime na kutoa maamuzi yao," alisema.

Alisema hayuko tayari kuvumilia hali hiyo ikitokea kwa wananchi wake hivyo akawaomba wananchi wa jimbo lake wamuunge mkono kupingana na uchochezi unaofanywa na wanasiasa hao.
Mei 16, mwaka huu mamia ya wakazi wa Nyamongo wilayani Tarime walivamia hifadhi ya mgodi wa North Mara kwa lengo la kutaka kuchukua mchanga wa dhahabu hatua iliyosababisha mauaji ya wananchi watano.
Mwisho.

'Serikali ipunguze utegemezi wa bajeti'

Na Grace Michael

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) umeitaka serikali kuhakikisha inapunguza utegemezi wa bajeti kutoka kwa wafadhili kwa kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kupunguza ukubwa wa serikali.

“Ikizingatiwa kuwa bajeti ya serikali ni tegemezi kwa kiasi kikubwa kwa wafadhili na deni la taifa linazidi kukua kutoka sh. trilioni 7.6 (2008/2009) hadi sh. trilioni 10.5  (2009/2010) ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 38, je, ni kwa vipi serikali inapanga kuongeza ukubwa wa bajeti wakati deni linazidi kukua na ikizingatiwa mikopo na misaada ya wafadhili haitabiriki...ni vyema sasa kuangalia namna ya kupunguza ukubwa wa serikali,” ilisema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na mtandao huo na kusainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Bi. Ussu Mallya, mtandao huo mbali na kuomba kupunguzwa kwa utegemezi lakini pia unaitaka serikali kutenga rasilimali za kutosha zitakazowezesha mchakato wa mabadiliko ya katiba kufanyika kwa ufanisi zaidi.

Taarifa hiyo ilihusu namna kikosi kazi cha mtandao huo kilivyochambua muongozo wa mpango wa miaka mitano wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2011/2012 hadi 2015/16 ambapo uchambuzi huo umefanywa kwa mtazamo wa ukombozi wa wanawake kimapinduzi, wakiongozwa na kaulimbiu ya “Haki ya Uchumi, Rasilimali ziwanufaishe wanawake walioko pembezoni”.

“Tunataka ushiriki zaidi wa wananchi katika mchakato mzima wa kutengeneza katiba mpya ili kuainisha vipaumbele vyao... mikakati ya kuimarisha soko la bidhaa za ndani kwa kuimarisha barabara za vijijini zitakazosaidia kuchukua mazao ya wakulima wadogo ambao wengi wao ni wanawake ili kuinua pato la ndani la taifa na kuimarisha uchumi mkuu lakini mikakati maalumi ya kuongeza ajira, maisha endelevu na kipato kwa wote, wanawake na wanaume, mijini na vijijini,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
TGNP inataka ushiriki wa wananchi katika michakato yote ya bajeti kuanzia mwanzo ili mambo yote muhimu yaweze kuingizwa na kupewa bajeti ya kutosha.

Alisema kuwa mategemeo ya muongozo huo wa bajeti yalikuwa kuona msimamo wa serikali katika kutetea haki na usawa wa kila mwananchi, kwa kuelekeza rasilimali za kutosha ili kufanikisha mchakato huu wa mabadiliko ya katiba, ambao ndio mhimili kwa wapiga kura walio wengi, hasa wanawake walioko pembezoni ikiwa ni pamoja na makundi mengine ya watu wanaoishi na ulemavu aina zote, VVU na UKIMWI.

Taarifa hiyo ilisema kuwa mwongozo wa bajeti ni lazima ulenge namna uchumi wa nchi utakavyojenga maisha ya watu wake kwanza, na si kuangalia tu wawekezaji wa ndani na nje ya nchi na suala la ajira na maisha endelevu kwa wote liwekewe kipaumbele.

Akirejea muongozo wa bajeti unasisitiza uimarishaji na uendelezaji wa masuala ya uchumi mpana na siasa kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, kuzuia mfumuko wa bei, kuendeleza sekta binafsi, kusimamia usawa katika bei ya mafuta kwa kuwekeza kupitia rasilimali watu.

“Sisi kama wanaharakati tulitarajia kuona muongozo huu wa bajeti unaweka kipaumbele katika kusimamia mgawanyo sawa wa rasilimali katika jamii,  kurasimisha kazi zisizo na kipato zinazofanywa na wanawake na wanaume walioko pembezoni, tunataka kuwe na mdahalo mpana wa kitaifa juu ya mawazo haya, maana
inaweza kuleta matokeo hasi kwa maendeleo ya uchumi wa taifa,” alisema.

“Vilevile tunapinga suala la kuweka kipaumbele katika uuzaji wa bidhaa nje ya nchi kwa wawekezaji wakubwa wakati soko la ndani la bidhaa linakufa.”

Vipaumbele vilivyoainishwa katika muongozo wa bajeti kwa mpango wa miaka mitano 2011/12-1025/16 vimeelekezwa zaidi kwenye Kilimo, miundo mbinu, viwanda, uwekezaji katika rasilimali watu, mazingira endelevu, usimamizi wa ardhi, mipango miji na makazi,kuimarisha mahusiano kati ya sekta ya umma na binafsi na  kuendeleza mafanikio katika sekta za kijamii.

Tuesday, May 24, 2011

ZIARA YA WAZIRI WA AFYA DKT. MPONDA

Dkt. Haji Mponda akisalimiana na Mhasibu Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bi. Grace

Mambo ya VICOBA

Dkt. Makongoro Mahanga akipongezana na wana VICOBA katika Mtaa wa Tembomgwaza, Kata ya Kimanga, Dar es Salaam

Mfumko wa bei za dawa unatisha-NHIF


Na Grace Michael
SERIKALI imetakiwa kuangalia uwezekano wa kuwa na chombo cha kudhibiti na kuangalia bei za dawa ili kukabiliana na tatizo la mfumko wa bei unaozidi kuongezeka kila kukicha.
Ombi hilo lilitolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bw. Emanuel Humba mbele ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Haji Mponda ambaye alitembelea mfuko huo kwa lengo la kuangalia namna majukumu ya mfuko yanavyotekelezwa.
“Katika kutekeleza majukumu yetu, bado tunazo changamoto kadhaa lakini kubwa zaidi ni ukosefu wa huduma bora vijijini hali inayochangia kwa kiasi kikubwa wananchi kutojiunga na mfuko wa afya wa jamii na kama inavyojulikana kuwa wanachama wetu wengi wako vijijini hivyo kuna haja ya kuangalia namna ya kuboresha huduma hizi,” alisema Bw. Humba.
Alisema kuwa tatizo jingine ambalo limekuwa ni changamoto kwa mfuko huo ni ongezeko la bei za dawa ambapo alitumia mwanya huo kumwomba Waziri mwenye dhamana kuliangalia suala hilo kwa jicho la pekee ili kuokoa maisha ya watanzania ambao wengi wao hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
“Kwa kweli tunaomba suala hili liangaliwe kwa upana wake, kwani hata sisi tunalazimika kutumia nguvu ya ziada kuhakikisha wanachama wetu wanapata  huduma za matibabu hasa dawa lakini ukiangalia kuna wananchi ambao hawana uwezo wa kumudu bei za dawa na ndio maana vijijini wanafikia hatua ya kugawa kidonge kimoja na kugawana na mgonjwa mwingine,” alisema Bw. Humba.
Bw. Humba alielezea matarajio ya Mfuko huo ambapo alisema kuwa wanatarajia kuongeza wigo wa wanachama ili kwenda sambamba na ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo inataka wananchi wengi zaidi kuwa wanachama wa mifuko ya afya.
Alisema kuwa mfuko unaoweza kufanikisha ahadi hiyo ni CHF hivyo akasema ili wananchi waweze kuvutiwa na kujiunga nao kuna haja ya kuboresha huduma zake ili ziwe na wigo mpana zaidi kwa kumwezesha mwanachama kutibiwa katika kituo chochote ndani ya mkoa anaootoka.
“Yapo mafanikio makubwa ambayo tumeyaona baada ya CHF kuwa chini yetu lakini ni lazima tuboreshe baadhi ya maeneo kama huduma vijijini ili wananchi waweze kuvutiwa zaidi na kujiunga,” alisema Bw. Humba.
Akijibu hoja hizo, Dkt. Mponda alisema kuwa tatizo la huduma vijijini tayari wizara imeliona na hatua zimeanza kuchukuliwa ikiwemo Bohari ya Dawa (MSD) kuanza kusambaza dawa hadi kwenye vituo vya kutolea huduma.
Alisema kuwa awali ukosefu wa dawa ulikuwa ukichangia na mlolongo mrefu wa usambazaji na baadhi ya dawa ziliibwa zikiwa katika mchakato huo ambapo sasa jukumu hilo limeanza kufanywa na MSD kwa baadhi ya mikoa ili dawa zipelekwe moja kwa moja na ziweze kufika kwa wakati uliokusudiwa.
“Zipo sababu ambazo zinasababisha upungufu wa dawa lakini kubwa ni ufinyu wa bajeti hivyo ni lazima vyanzo vingine vya fedha katika halmashauri vitumike kwa ajili ya kununulia dawa ili kuboresha huduma za afya.
Suala la mfuko wa bei, Dkt. Mponda alisema wizara itaangalia ili kuona kama kuna haja ya kuwepo kwa chombo hicho ambacho kitaangalia mfumko wa bei za dawa ambazo kwa sasa zinasababishwa na mfumo wa soko huria.
Kwa upande wa wafanyakazi waliowakilishwa na Mwenyekiti wa TUGHE, Bw. Baraka Maduhu, waliiomba serikali kuhakikisha inalifanya suala la mifuko ya afya kuwa agenda ya kitaifa ili wananchi wahamasike kujiunga zaidi.
Mwisho.

Monday, May 23, 2011

Maranda, Farijala jela miaka 21

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu kifungo cha miaka 21 jela, Kada wa Chama Cha Mapinduzi Bw. Rajab Maranda na ndugu yake Bw. Hussein Farijala baada ya kupatikana na hatia katika makosa ya wizi wa mabilioni katika akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

Kesi hiyo ya wizi wa mabilioni hayo ambazo zinawakabili wafanyabiashara mbalimbali, imekuwa ya kwanza kutolewa uamuzi huku kesi zingine zikziwa katika hatua mbalimbali.

Waziri wa afya kutembelea NHIF kesho

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), unatarajia kutembelewa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii kesho asubuhi.

Sunday, May 22, 2011

JK atakiwa kuwabana waliosababisha mgawo

Na Grace Michael

RAIS Jakaya Kikwete ametakiwa kuueleza umma hatua ambazo serikali yake inakusudia kuchukua kurekebisha matatizo yanayoikumba sekta ya umeme ikiwemo kuwachukulia hatua wote waliohusika au kushindwa kuwajibika ipasavyo kumaliza tatizo hilo.

Mbali na hilo, Waziri wa Nishati na Madini Bw. William Ngeleja naye ametakiwa kuwajibika kutokana na athari za kutochukua hatua haraka hali inayosababisha kuendelea kuwepo kwa mgawo wa umeme.

Tamko hilo limetolewa jana na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, Bw. John Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Ubungo kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

“Rais akiwa ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri anatakiwa kueleza kwa umma hatua ambazo serikali yake inakusudia kuchukua kurekebisha hali hiyo kwani
alishatembelea wizara na kutoa maagizo na akarudia tena maagizo yale yale kwa kutumia mamilioni ya walipa kodi kupitia semina elekezi, kinachotakiwa hivi sasa
sio maagizo tena bali ni mkuu wa nchi kuchukua hatua,” alisema Bw. Mnyika.

Alisema kuwa endapo tamko hilo halitazingatia maelezo na vielelezo zaidi vitawasilishwa kwenye vikao vya kambi rasmi ya upinzani na hatimaye masuala husika na mengine zaidi kuibuliwa bungeni kwa ajili ya wahusika kuwajibishwa.

Katika tamko hilo, Bw. Mnyika alieleza kuhusu mgawo wa umeme unaotokana na upungufu wa gesi ambapo alisema kuwa hali hiyo imetokana na mamlaka husika
kutokuwajibika ipasavyo.

Alisema kuwa  matengenezo ya mitambo hiyo yalifahamika kwa serikali kuanzia mwishoni mwa mwaka 2010 na Februari 2011 na kujadiliwa ndani ya serikali.


“Kuna tuhuma za muda mrefu kuwa Kampuni ya Pan African imekuwa haifanyi matengenezo ya ukamilifu na kwa wakati hata hivyo wizara inayohusika haikueleza
hatua ambazo zimechukuliwa hali ambayo imeongeza hitaji la matengenezo makubwa kwa wakati mmoja yaliyosababisha gesi kutokusambazwa na kuleta upungufu wa umeme wa kati ya Megawati 200 mpaka 359 katika kipindi husika lakini serikali haijachukua hatua za haraka kumaliza tatizo hilo,” alisema Bw. Mnyika.

Alisema kuwa hali ya utegemezi wa serikali kwenye sekta ya gesi kwa kampuni yenye mwelekeo wa udalali imesababisha hasara na ina mwelekeo pia wa kuhatarisha
usalama wa nchi katika siku za usoni kama hatua stahili hazitachukuliwa

Hivyo Bw Mnyika aliiomba Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kuchunguza hali hiyo na
kuchukua hatua mapema.

“Serikali inapaswa kupitia upya mikataba na kampuni ya Songas, Pan African na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) ili kuondoa migongano na kupunguza mzigo
kwa taifa wakati gesi asilia ni mali asili ya Watanzania sambamba na kupanua wigo wa usafirishaji wa gesi katika mwaka wa fedha 2011/2012,” alisema.

Alisema suala lingine ambalo alizungumzia ni hatua za dharura za kupunguza upungufu wa umeme ambapo alitahadharisha kwamba mgawo mkubwa na wa muda mrefu utalikumba taifa kuanzia Julai mwaka huu kutokana na hatua za dharura kutochukuliwa kwa wakati.

Alisema pamoja na serikali kushikilia  msimamo wa kukodi mitambo ya umeme wa Megawtai 260 ambayo itatumika kwa kipindi cha miezi sita pekee kwa gharama za zaidi ya bilioni 400 badala ya kuweka mkazo katika kununua mitambo kama ambavyo imeshauriwa na wadau mbalimbali, Wizara ya Nishati na Madini haijawajibika kwa kiasi cha kutosha kuhakikisha nchi haikumbwi na mgawo.

Bw. Mnyika alisema kuwa mchakato wa kutekeleza mpango wa dharura umecheleweshwa na hivyo kuna hatari ya mitambo hiyo kuwa tayari kutoa huduma mwezi Januari
katika kipindi ambacho haihitajiki na kusababisha hasara kwa taifa kama ilivyokuwa kwa mitambo ya Richmond.

Kutokana na hali hiyo, alisema serikali inapaswa kusitisha mara moja mpango huo na kuelekeza fedha hizo za umma katika hatua za dharura za kununua mitambo ya
kudumu na kinyume na hapo itathibitika kwamba kuna mazingira ya ufisadi katika mpango huo wenye kutaka kuongeza mzigo wa madeni kwa TANESCO na gharama za umeme kwa wananchi wa kawaida.

Alisema kuwa madhara na hasara yote ambayo wananchi, sekta binafsi na serikali imekuwa ikipata kuanzia  Februari mwaka mwaka huu mpaka Desemba 2012
inatokana na kutokuwajibika kikamilifu kwa mamlaka husika kwa kuwa dharura ilifahamika tangu 2008

Alisema kuwa serikali ikapanga kwamba utekelezaji wa miradi ikiwemo ya kutumia mafuta mazito Mwanza na Mradi wa  kutumia gesi asilia Ubungo, Kiwira ilipaswa kukamilika Februari mwaka huu lakini kutokana na uzembe, ufisadi miradi hiyo itakamilika 2012/2013.

Suala lingine alilozungumzia ni tuhuma za ufisadi katika manunuzi kwa ajili ya miradi ya umeme ambapo aliweka wazi kuwa serikali haijawajibika ipasavyo
kushughulikia tuhuma za ufisadi katika ununuzi wa mafuta mazito ambayo Waziri wa Nishati na Madini alieleza bungeni Aprili kwamba zimetumika sh. bilioni 46 kwa ajili ya kuendesha mitambo ya kufua umeme ya IPTL ambapo Mei, mwaka huu.

Alisema kuwa Wizara ya Nishati na Madini kupitia taarifa nyingine ilisema kwamba fedha zilizotumika kwenye ununuzi wa mafuta katika kipindi husika ni sh. bilioni 28 bila kueleza sababu za kutofautiana kwa maelezo ya waziri bungeni na haya yaliyotolewa.

Alisema kuwa kutokana na hali hiyo, Kamati ya Nishati na Madini inapaswa kufanya uchunguzi maalum kama ilivyoombwa na Mwenyekiti wa Kamati za Hesabu za Mashirika ya Umma, Bw.Zitto Kabwe.

Mwisho.

Tusiweke mzaha suala la Katiba

Na Grace Michael
HAKUNA ubishi kuwa Katiba mpya inahitajika haraka ili ikidhi mahitaji ya sasa na kwa kulitambua hilo, Serikali imekubali kuanza mchakato huo ili wenye katiba kwa maana ya wananchi waamue ni kitu gani kiwe ndani ya katiba na nini kusiwemo.
Hatua ambayo imefikiwa na Serikali kwa sasa ni kuandaa muswada ambao utaruhusu kutungwa kwa katiba mpya ambao mbali na kuruhusu ndio unaotoa mwongozo wa nini kifanyike ili kufikia hatua ya kuwa na katiba mpya kama yalivyo mahitaji ya kila mmoja.
Muswada huo unatarajiwa kuwasilishwa katika mkutano wa  tatu wa bunge 10 unaoanza kesho mjini Dodoma.
Pamoja na hatua hiyo kufikiwa, lakini bado wananchi wanayo haki ya kuendelea kutoa mawazo yao juu ya muswada huo na kwa kuzingatia hilo, juzi wasomi wa kada mbalimbali wakiwemo wanasheria, wanasiasa, wanaharakati na wananchi kwa ujumla walikutana Dar es Salaam kwa ajili ya kongamano ambalo lilijikita kujadili muswada huo.
Katika majadiliano hayo, ambayo kwa namna moja ama nyingine ndiyo yanatoa mwanga kwa wananchi wa kawaida kutokana na mazingira halisi ya muswada ulivyo.
Katika mjadala huo, hoja mbalimbali ziliibuliwa zikiwemo za mapungufu makubwa yaliyoko ndani ya muswada lakini jambo ambalo limenivuta na kuamua kuandika ukurasa huu ni hoja iliyowasilishwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Peter Maina ambaye alihoji sababu ya muswada huo kuandaliwa kwa lugha ya Kiswahili.
Hoja hii ilinivuta na kunionesha ukweli kuwa kuandaliwa kwa lugha ya kingereza si sahihi kwa kuwa muswada huo unatakiwa ueleweke ipasavyo kwa wananchi ambao ndio hasa walengwa au wamiliki wa katiba.
Nakubaliana na mhadhiri huyo kuwa robo tatu ya watanzania watabaki gizani kwa maana ya kutouelewa vyema muswada huo ambao endapo utapitishwa ndio utatungiwa sheria hivyo ingekuwa ni busara kwa serikali ikaona umuhimu wa kuandaa muswada huo kwa lugha ambayo kila mmoja angeisoma na kuielewa ili ajipange namna ya kuchangia maoni yake kwenye katiba tarajiwa.
Kila mmoja atakubaliana na mimi kuwa Katiba si ya serikali wala si mtu binafsi na wala si ya chama chochote cha siasa bali ni mali ya watanzania hivyo jambo la msingi ambalo ningetarajia lifanyike ni muswada huo kuwekwa katika lugha rafiki ambayo kila mmoja kwa nafasi yake angeuelewa.
Kuwekwa kwa lugha ya kingereza ni kuwanyima au kutaka wananchi wengine wasielewe na wasipoelewa kuna hatari kubwa ya wananchi hao kutoshiriki ipasavyo katika utoaji maoni yao wakati wa mchakato wa katiba inayotarajiwa kuandikwa hivyo ingekuwa ni jambo la busara serikali ikatambua kuwa suala la katiba si la mzaha hata kidogo kwa kuwa haki ya kila mmoja imo ndani ya chombo hicho.
Jambo jingine ambalo ningependa kulizungumzia ni muswada huo kuvizuia kwa vyama vya siasa kuelimisha wananchi, sidhani kama hilo ni sawa, ingekuwa vyema vyama navyo vikatumika katika kuelimisha wananchi ili waweze kutoa michango yao vyema wakati utakapofika wa kutoa maoni yao.
Nasema kwa kuwa uelimishaji ungesaidia hata wananchi kubaini mambo mbalimbali lakini pia wangepata mwamko wa kutoa maoni ya mambo wanayoona yakiwekwa ndani ya katiba yatasaidia kwa kiasi kikubwa.
Kutokana na hali hiyo, Serikali inatakiwa kuwa sikivu na kuchukua mawazo mazuri yanayotolewa na wadau mbalimbali na kuyafanyia kazi ili hatimaye tuweze kupata katiba ambayo itadumu au itakidhi matakwa ya wengi kwa muda mrefu.
Lakini wakati wa uchangiaji mawazo ingekuwa vyema kila mmoja akaheshimu mawazo ya mwingine nah ii inatokana na kila mtu kuwa na mawazo yake hivyo kila mawazo yanayotolewa yaheshimiwe kwa kuwa mwisho wa siku yapo mawazo yatakayochukuliwa na kuachwa hivyo hakuna sababu ya kukatishana tama katika mchakato huu.
Nimelazimika kusema hivyo kwa kuwa hali ya kudharau michango ya wengine ilijionesha dhahiri katika kongamano hilo wakati Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mashariki alipozomewa jukwaani wakati akitoa mchango wake kuhusiana na mjadala uliokuwepo wa kujadili muswada huo.
Jambo hili ni zito hivyo sisi kama Watanzania tunatakiwa kuonesha umoja wetu na ushirikiano katika jambo hili ili liweze kupita katika mchakato wote kwa amani na liwe na mafanikio ya kutosha.
Endapo tutaanza kuoneshana ubabe katika utoaji wa michango yetu mwisho wake utakuwa ni mbaya hivyo ni vyema mawazo ya kila mmoja yakaheshimiwa kwa kiwango kikubwa kwa kuwa kila mmoja wetu ana haki ya kusema au kuchangia suala hilo.
Kwa upande wa wanasiasa nao watangulize maslahi ya taifa mbele na kuachana na maslahi binafsi katika mchakato huu na kama maslahi ya nchi yatatangulizwa tutapata Katiba nzuri na ambayo kila mmoja wetu ataifurahia.
Mungu ibariki Tanzania
0755 23 42 57
Mwisho

Ongezeni bidii kwenye kazi-Dkt. Mahanga


Na Grace Michael
WANANCHI wametakiwa kutambua kuwa njia pekee ya kujikwamua katika hali ngumu ya maisha na kuondokana na umasikini ni kuongeza bidii katika shughuli za uzalishaji ili ziwe za ufanisi na tija.
Hata hivyo wametakiwa kuondoa kasumba ya kubaki wakiilaumu serikali kwa kila jambo na badala yake watimize wajibu wao kwa kufanya kazi kwa ufanisi huku serikali kwa upande wake ikiboresha mazingira yatakayowezesha kufanyika kwa shughuli za maendeleo bila matatizo.
Hayo yalisemwa juzi na Mbunge wa Jimbo la Segerea, Dkt. Makongoro Mahanga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kazi na Ajira wakati akizindua umoja wa VICOBA 10 katika Mtaa wa Tembomgwaza, Kata ya Kimanga, Dar es Salaam.
“Ebu ifike mahali tuache kasumba ya kurusha lawama kwa serikali kuwa imeshindwa kuondoa umasikini, kila mmoja wetu ajiangalie katika lawama hizo amechangia kwa kiasi gani...huwezi ukawa unalaumu na wakati kazi unayofanya ni kukaa mabarazani na kucheza bao kila kukicha ...ni kweli serikali kuna mambo inayotakiwa kufanya hasa kwa kuweka mazingira mazuri kwa wananchi wake lakini pia wananchi nao wana wajibu wa kujituma kufanya kazi ili kuongeza uzalishaji kwani maendeleo hayaji kwa kubweteka,” alisema Dkt. Mahanga.
Alisema kuwa hakuna serikali yoyote duniani ambayo inaweza ikagawa fedha kwa kila mwananchi wake kwa lengo la kutatua matatizo aliyonayo bali kinachoweza kufanywa na serikali ni kuwasaidia wananchi kwenye makundi ikiwemo kuwakopesha mitaji ili waweze kuzalisha zaidi lakini pia kujiajiri wenyewe.
“Uwekezaji wa pamoja una faida kubwa zikiwemo za kupata kiurahisi elimu ya kuendesha shughuli za uzalishaji, mitaji, mikopo kutoka kwenye taasisi mbalimbali za fedha lakini pia hata serikali ni rahisi kutambua kundi la watu wengi na kulisaidia tofauti na mtu mmoja mmoja,” alisema Dkt. Mahanga.
Akizungumzia muungano wa vicoba hivyo, aliwataka kuhakikisha wanakuwa na Mfuko wa pamoja ambao utawafanya waongeze uaminifu hasa kwa taasisi za fedha wakati wanapohitaji mikopo.
Katika hafla hiyo jumla ya sh. Milioni mbili zilichangwa kwa lengo la kutunisha mifuko ya vicoba hivyo huku Dkt. Mahanga akikubali ombi la wana VICOBA hao ambao walimwomba kuwa mlezi wa umoja huo.
Alisema kuwa yuko tayari kushirikiana na wana vikundi hao kwa kuwatafutia wataalam kwa ajili ya kuwapa elimu ya namna ya kuendesha shughuli zao pamoja na mambo mengine.
Dkt. Mahanga alitumia mwanya huo kuwaeleza wananchi namna kero zinazowakabili hasa za maji na barabara zitakavyoshughulikiwa.
“Jamani nadhani mtakubali kabisa kuwa kero kubwa kwa kata yetu ya Kimanga ni maji na barabara na kero hizi tumeamua kuzipa kipaumbele kwa maana ya kutaka kuziondoa haraka ili wananchi wapate unafuu...fedha zimetengwa kwa lengo la kumaliza kero ya maji Dar es Salaam hivyo mwaka 2015 hatutaki kuja kwenu kwa ahadi ya maji,” alisema Dkt. Mahanga.
Mwisho.

Thursday, May 19, 2011

Serikali yaanzisha taasisi ya maadili

Na Grace Michael

KATIKA kuhakikisha inapambana na changamoto zinazotokana na uongozi mbovu na ukosefu wa maadili, serikali imeanzisha taasisi maalumu kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa viongozi wa ngazi za juu yatakayowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Taasisi hiyo inayojulikana kwa jina 'Uongozi Institude' inatarajia kutoa mafunzo yatakayo wajengea uwezo zaidi viongozi walioko madarakani pamoja na kuandaa vijana watakao kuwa viongozi hapo baadaye.

Akizundua Bodi ya Wakurugenzi wa taasisi hiyo Dar es Salaam jana, Rais Jakaya Kikwete, alisema Tanzania na nchi nyingine barani afrika zinakabiliwa na uhaba wa viongozi wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi, jambo ambalo linakwamisha ukuaji wa maendeleo.

Rais Kikwete alisema changamoto hizo zinazorudisha maendeleo nyuma zinaweza kuondoka endapo viongozi watajengewa uwezo utakaofanya kuwajibika na kufuata misingi sheria na utawala bora.

Alisema changamoto hizo ni pamoja na kudorora kwa uchumi, kasi ndogo ya ukuaji wake, uhaba wa chakula, mfumuko wa bei katika sekta ya nishati ya mafuta na uwezo mdogo klatika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Kutokana na hali hiyo, Rais Kikwete ameiagiza Bodi ya taasis hiyo kuhakikisha kuwa inakuja na mbinu mpya zitakazowawezesha viongozi kukabiliana na changamoto mpya zinazoibuka hasa kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia.

Aliseka kuwa serikali ya Tanzania itatoa ushirikiano kwa taasisi hiyo ili kuhakikisha inafanya kazi iliyokusudiwa na viongozi wake watashiriki katika mafunzo mbalimbali ili wajenge uwezo zaidi wa kiuongozi.

"Tumetoa hekari 400 kwa ajili ya taasisi hii, hatukuwahi kuwa na chuo cha ngazi ya juu kama hiki, hivyo bodi mnalo jukumu la kuhakikisha mnaongeza wigo nje ya Tanzania kwa kuwa azma ni kuona taasisi inafahamika Afrika nzima kama kituo bora cha maendeleo ya uongozi," alisema Rais.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Prof. Joseph Semboja alisema kuwa taasisi hiyo inafanya kazi na viongozi kutoka ngazi za juu serikalini lakini pia ina mpango wa kujumuisha viongozi wa makampuni na taasisi za kiraia na viongozi kutoka mataifa mengine.

"Taasisi hii itawasaidia viongozi kufanya vizuri katika kutimiza jukumu lao kuendeleza jamii ili iweze kutumia fursa za maendeleo barani Afrika katika mfumo endelevu, uongozi ndio nguzo ya maendeleo hivyo viongozi wanatakiwa kuelewa mambo kwa mtazamo mpana, ajenda ya maendeleo ya Taifa na athari zake kutokana na muktadha wa ukanda wa Afrika na dunia," alisema Prof. Semboja.

Alisema kuwa ili maendeleo yaweze kufikiwa ni lazima viongozi wawe ni watu wa kuona mbali na watu wanaowatumikia wawe na imani nao lakini pia wawe mfano wa kuigwa na wengine ili kutimiza malengo na utekelezaji wa malengo yaliyokusudiwa.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa taasisi itafanya kazi na viongozi kwa lengo la kuendeleza agenda ya taifa na kusimamia utekelezaji wa mikakati ya taifa, kuchambua na kuelewa mambo mapya yanayoathiri maendeleo kitaifa, kikanda na kimataifa na kutafsiri athari zake kwa taifa lakini pia kuafuatilia maslahi ya nchi katika kanda ya Afrika na dunia.

"Tutawasaidia viongozi kwa kutoa programu za kuimarisha uongozi, kusaidia maendeleo ya sera na uchambuzi pamoja na mitandao ya kubadilishana ujuzi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi Bi. Ritva Koukku alisema kuwa lengo la taasisi hiyo ni kuboresha uwajibikaji wa viongozi na watendaji wa ngazi za juu serikalini, ombwe ambalo linazidi kuwa kubwa.

Alisema ukubwa wa changamoto zilizopo zinahitaji nguvu ya pamoja na ushirikiano kati ya nchi na nchi, ndio maaana selikali ya Finland imekubali kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuhakikisha lengo hilo linafikiwa.

Uzinduzi huo ulihudhuliwa na viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri, mabalozi, makatibu wakuu na viongozi wengine wa ngazi za juu serikalini.

Serikali yapinga Zombe kulipwa fidia

Na Grace Michael

UPANDE wa Serikali katika kesi ya madai ya sh. bilioni tano iliyofunguliwa na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Abdallah Zombe umesema  mlalamikaji hana madai ya msingi dhidi ya serikali hivyo kumtaka athibitishe.

Bw. Zombe aliishitaki serikali akidai mabilioni hayo ya fedha kutokana na madai ya kunyanyaswa, kudhalilishwa na kubambikiziwa kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wanne wa madini kutoka mkoani Morogoro.

Kwa mujibu wa hati ya majibu iliyowasilishwa Mahakama Kuu na upande wa Serikali, si kweli kwamba kitendo cha ukamataji uliyofanywa dhidi ya Bw. Zombe haukufuata sheria kama mlalamikaji anavyodai.

Pia upande huo unadai kuwa madai ya mlalamikaji kuwa hakupewa haki ya kusikilizwa kwa mujibu wa sheria si ya kweli na polisi walifuata utaratibu wa sheria ikiwa ni pamoja na taratibu zote za kumkamata.

Hati hiyo inaeleza kuwa Bw. Zombe hana sababu za msingi za kuidai serikali kwa kuwa katika hati ya madai ameshindwa kuthibitisha uvunjwani wa sheria dhidi yake wakati akikamatwa.

Pamoja na madai hayo, Upande wa Serikali unaieleza mahakama kuwa kesi ya madai ya Bw. Zombe dhidi ya serikali si halali kwa sasa kutokana na kuwepo kwa rufaa dhidi ya uamuzi wa awali wa Mahakama Kuu ambayo ilimwachia huru Bw. Zombe katika kesi ya mauaji wa watu wanne.

Mlalamikaji katika kesi hiyo anatetewa na Wakili Richard Rweyongeza ambapo kesi hiyo ilitajwa jana Mahakama Kuu ya Tanzania na mahakama hiyo kumwamuru mlalamikaji kujibu majibu ya serikali Mei 23, mwaka huu.

Kesi hiyo ambayo iko mbele ya Jaji Upendo Msuya mbali na kupangwa tarehe ya Bw. Zombe kujibu majibu ya serikali pia imepangwa kutajwa Juni 20 mwaka huu.

Katika madai ya mlalamikaji, anadai kuwa Jeshi la Polisi lilikiuka sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 inayotaka kabla ya mtu kukamatwa aelezwe sababu zilizomfanya akamatwe lakini pia ni lazima achukuliwe maelezo yake ambayo baadaye hutumika mahakamani kama kielelezo.

“Jeshi la polisi lilikwenda kinyume na sheria hiyo kwani lilinikamata, na kunifungulia kesi hiyo ya mauji bila ya hata ya kunihoji wala kuchukua maelezo yangu, hivyo sikupewa haki zangu wakati wa kukamatwa,” anadai Bw. Zombe.

Bw. Zombe aliachiwa huru Agosti 17, mwaka 2009 baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuona hana hatia dhidi ya kesi ya mauaji ya watu hao wanne.

Nape: Ikithibitika nilipeleka siri CCJ nitawajibika

Na Grace Michael
SIKU moja baada ya Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Fred Mpendazoe kuanika wazi kuwa, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
CCM, Bw. Nape Nnauye alikuwa ndio injini ya uanzishwaji wa Chama cha Jamii (CCJ) na alikuwa akivujisha siri za Chama Cha Mapinduzi (CCM), amesema yuko tayari kuwajibika endapo siri hizo zitatajwa hadharani.

Bw. Nnauye aliweka msimamo wake jana baada ya kuhojiwa na Majira kuhusu  tuhuma mbalimbali zinazoelekezwa kwake na CHADEMA.

“Tuhuma ya mimi kuwepo kwenye mkakati wa uanzishwaji wa CCJ ni uzushi usio na mashiko kwani jana (juzi) niliposikia ndo nikaanza kuuliza hata ofisi zao zilipo...lakini kubwa waeleze pia CCJ ilikufaje na hizo siri wanazodai nilikuwa nawapa wazitaje hadharani nitawajibika,” alisema Bw. Nnauye.

Kuhusu tuhuma za kula mishahara miwili wa CCM na wa Mkuu wa Wilaya, alisema kuwa tangu ateuliwe hata mwezi haujaisha tangua ashikea nafasi hiyo hivyo kukanusha kupokea mishahara miwili.

Tuhuma nyingine ambayo ilielekezwa kwake ni ya kuhusika na kula fedha zilizotokana na ufisadi wa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ambapo kwa hilo alidai kuwa wakati ufisadi huo ukifanyika yeye alikuwa masomoni India.

“Ushauri wangu kwa CHADEMA wajifunze kula vya kuchinja waachane na vya kunyonga,” alisema.

Akifafanua usemi huo alisema kuwa CHADEMA wanatakiwa waishi kwa kufanya kazi halali na sio kupika majungu na kupandikiza chuki kwa Watanzania kwa kuwa mwisho wa uongo ni aibu na akasema kuwa mwisho wa chama hicho umefika.

Juzi Bw. Mpendazoe akihutubia wananchi wa Mbamba Bay mkoani Ruvuma alianika mpango mzima wa waliohusika na uanzishaji wa CCJ na kuweka bayana kuwa Bw. Nnauye ndiyeo aliyekuwa akitumika kuandaa katiba ya chama hicho na kukusanya siri mbalimbali za CCM.

Alisema kuwa “Nape ni mnafiki, msaliti na mhaini ndani ya CCM kwa kuwa alishakula njama za kukiangusha CCM...tulifanya naye vikao vya siri hadi tukaanzisha CCJ leo anaitetea CCM ambayo alikuwa ameiona haifai, ni mnafiki mkubwa,” alisema Bw. Mpendazoe.

Alisema kuwa Bw. Nape ndiye alikuwa akitumika ndani ya CCJ kwenda kwa wafadhili kupokea fedha za kuanzisha chama hicho na ndiye aliyehusika kutafuta pango la chama.

Alikwenda mbali kwa kusema Rais Jakaya Kikwete anaongoza chama feki kwa kuwa kina watu wanafiki na walishamdharau kwa uongozi wake dhaifu lakini yeye aliwapa vyeo bila ya kuwajua unafiki wao.