Friday, August 17, 2012

NHIF yaipigiga Jeki zahanati ya Mbutu

Zahanati ya Mbutu iliyoppo Kata ya Somangila Manispaa ya Temeke ambayo imechangiwa shilingi milioni tatu na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa ajili ya ujenzi wa Wodi ya akina mama.

Diwani wa Kata ya Somangila, Aisha Mpanjila akitoa shukrani kwa msaada uliotolewa na BHIF

Mganga Mkuu wa Zahanati, Scholastika Munishi akitoa maelezo ya utangulizi katika hafla ya kukabidhiwa kwa hundi ya sh. milioni 3.

Mjumbe wa Bodi ya NHIF, Mariam Wilmore akikabidhi hundi hiyo.

Mmeona hundi hii?

Diwani akionesha hundi 

Meneja wa Kanda ya Temeke Imelda Likoko akibadilishana mawazo na Mganga wa Kituo



Na Mwandishi Wetu

DIWANI wa Kata ya Somangila, iliyopo Temeke, Aisha Mpanjila amesema kuwa
kitendo cha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya cha kusaidia Zahanati ya Mbutu
kitahamasisha wananchi wengine kuchangia ujenzi unaoendelea katika
zahanati hiyo na hatimaye kumaliza tatizo la miundombinu.

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, jana ulikabidhi hundi yenye thamani ya sh.
Milioni tatu kwa lengo la kusaidia ujenzi wa wodi ya akina mama na watoto.

Akipokea msaada huo, Diwani Mpanjila alisema kuwa NHIF imeonesha njia na
imekuwa mfano wa kuigwa hasa kwa kutambua mahitaji ya wananchi katika
sekta ya afya.

"Kweli nyie ni Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya…pamoja na kusaidia
wanachama wenu katika huduma za matibabu lakini mmekwenda mbali zaidi kwa
kutoa hata msaada wa kuboresha vituo vya kutolea huduma msaada ambao
unamgusa kila mtu…nawapongeza sana," alisema.

Kutokana na hali hiyo, Diwani huyo alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi
wa maeneo hayo ambao ni wanufaika wa moja kwa moja na zahati hiyo kuunga
mkono Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kuchangia ili ujenzi wa wodi
zilizopo zikamilike na zianze kutumika mara moja.

Naye Mjumbe wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Mariam Wilmore amesema NHIF imeguswa na matatizo ya wakazi wa kata hiyo hivyo itaendelae kusaidia kadiri ya uwezo wake.
 
Zahanati ya Mbutu inahudumiwa zaidi ya wakazi wa mitaa SITA inayozunguka kata hiyo.




Friday, August 10, 2012

Naibu Waziri wa Afya atembelea Mradi wa NHIF Dodoma

Meneja wa Kanda ya Kati wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Daudi Bunyinyiga akitoa maelezo ya
mradi wa Kituo cha Matibabu cha Kisasa kinachojengwa katika Hospitali ya Rufaa Dodoma, kwa
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alipotembelea mradi huo.

Naibu Waziri akipata maelezo kutoka kwa uongozi wa Hospitali ya Dodoma.

Akisikiliza maelezo ya huduma zitakazotolewa baada ya kukamilika kwa mradi wa kituo cha kisasa unatekelezwa na NHIF

Akiendelea kupata maelezo

Mradi wa Kituo cha Kisasa cha Huduma za Matibabu kinachojengwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imesema kuwa kukamilika kwa mradi wa Kituo cha Kisasa cha Uchunguzi wa Magonjwa unaotekelezwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Chuo Kikuu Dodoma utapunguza utegemezi wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa kuwa kitakuwa na vifaa vya kisasa na madaktari bingwa. 

Hayo yalisemwa na Waziri wa Kazi na Ajira Gaudensia Kabaka wakati akijibu hoja ya Kambi ya Upinzani ambayo ilihoji faida za uwezekezaji unaofanywa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya katika Chuo Kikuu cha Dodoma. 

“Uwekezaji katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Medicare Centre of Excellence) ni eneo mojawapo linalolenga kuhakikisha kuwa huduma za rufaa nchini zinaimarika ikiwemo kupunguza utegemezio wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi,” alisema Waziri.

Alisema kuwa mradi huo utakuwa na huduma muhimu kwa wanachama na wananchi kwa ujumla ikiwemo huduma za matibabu ya figo, huduma za vipimo muhimu kama Magnetic Resonance Imaging (MRI) na vipimo vingine vya uchunguzi.

Aidha kituo hicho cha kisasa kitakuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi wanaosomea shahada ya udaktari kujifunzia kwa vitendo.

Waziri Kabaka pia litumia fursa hiyo kufafanua kuwa, kwa mujibu wa sheria ya Mfuko huo kifungu cha 33b kinauruhusu Mfuko kuwekeza katika vitega uchumi ambavyo vinalenga moja kwa moja uboreshaji wa huduma za afya nchini.


Thursday, August 2, 2012

NHIF, TAMISEMI, WAUJ WAJADILI UBORESHAJI HUDUMA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma 

UBORESHAJI wa huduma za matibabu kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya hususan upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma ni moja ya mambo yaliyojadiliwa mwishoni mwa wiki katika kikao kazi kilichojumuisha wataalam kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na TAMISEMI. 

Katika kikao kazi hicho ambacho kilihudhuriwa na maofisa wa ngazi za juu katika taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na TAMISEMI wakiwemo mawaziri wa pande zote mbili, walijadili kwa kina namna ya kupunguza ama kuondoa kabisa tatizo la dawa ambalo wanachama na wananchi kwa ujumla wanakutana nalo wakati wa kupata huduma za matibabu.

Kwa upande wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, kupitia Mkurugenzi wake Mkuu, Emanuel Humba alisema kuwa Mfuko utaendelea na uboreshaji wa huduma za matibabu kupitia mpango wa Mfuko huo wa mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo kwa vituo vilivyosajiliwa na Mfuko huo lakini pia kuendelea kusajili maduka ya dawa muhimu ili wanachama wapate huduma inayotakiwa na wananchi waone umuhimu wa kujiunga na Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF). 

Aidha kwa upande wa Bohari ya Dawa (MSD) ambao ndio wana jukumu la usambazaji dawa, kupitia Mkurugenzi wake Mkuu Joseph Mgaya, alisema kuwa wanaendelea kushughulikia changamoto zilizopo kama kutokuwepo kwa maoteo sahihi ya dawa ili hatimaye idara hiyo iweze kuondokana na malalamiko yanayoelekezwa kwake. 

Wakihitimisha kikao kazi hicho, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) Hawa Ghasia, walizitaka pande zote mbili kuhakikisha zinatekeleza maafikiano yaliyofikiwa katika kikao hicho ili kipa upande uweze kutoa huduma nzuri kwa wananchi wa Tanzania.

Aidha walisema kuwa njia pekee ya kuwakomboa wananchi au kuwafanya wawe na uhakika wa kupata matibabu ni kuwahamasisha kujiunga na Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF) hivyo wakaitaka NHIF kuhakikisha inaongeza kasi ya uelimishaji huku Serikali ikiendelea na uboreshaji wa huduma za matibabu kwa kushirikiana na wadau wote wa sekta ya afya.

1. Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Emanuel Humba akitoa maelezo ya utangulizi katika mkutano huo, kulia ni Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, Jumanne Sagini

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hussein Mwinyi akitoa maelekezo kwa watendaji, kulia ni Waziri wa TAMISEMI, Hawa Ghasia.

Mawaziri wakiteta jambo katika mkutano huo.

Dk. Mwinyi akiendelea kusisitiza jambo



Ofisa kutoka NHIF anayeshughulikia CHF, Rehani Athumani akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Mfuko huo katika kikao kazi hicho

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Regina Kikuli akitoa mwongozo wa majadiliano.

Mkurugenzi NHIF akijibu hoja za wajumbe.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Joseph Mgaya na Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo wakifuatilia mjadala

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Hamis Mdee akifuatilia mjadala

Dk. Mwinyi akifunga kikao