Tuesday, December 20, 2011

Hatutalipa madai yasiyokuwa na taarifa-NHIF

Na Grace Michael, Morogoro

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya umesema kuwa hautakuwa tayari kulipa fedha za tele kwa tele kwa Halmashauri ambazo zitashindwa kuwasilisha madai yake yakiwa na taarifa muhimu kama majina ya wakuu wa kaya.

Imesema ni lazima madai yanayowasilishwa kwa ajili ya kulipwa fedha hizo yawe na majina hayo na si vinginevyo.

Hayo yalisemwa mjini hapa na mmoja wa watoa mada wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Rehani Ahuman wakati akijibu maswali ya waratibu waliohudhuria kongamano la kwanza la mfuko huo ambao walitaka kufahamu umuhimu wa kuambatanisha majina hayo kwenye madai.

"Jamani ni lazima tufike mahali tufanye kama inavyotakiwa, wapo ambao wameweza na kama hao wameweza wote mnaweza kufanya hivyo, kumbukeni hizi ni fedha ambazo haziwezi kulipwa bila kuwepo na utaratibu unaoeleweka na haya majina yatasaidia katika mambo mengi," alisema Rehani.
Alisema kuwa pamoja na sasa kuhitajika majina hayo kwenye madai yao, lakini kwa hapo baadae zitahitajika taarifa zaidi kwa kuwa lengo ni kujiridhisha na madai yanayodaiwa.

Alisema kuwa lengo la CHF ni kuhakikisha mwananchi aliyejiunga anaona umuhimu au faida ya mfuko huo hivyo bila kuwa na umakini katika uendeshaji wake lengo hilo haliwezi kukamilika.

Rehani pia alitumia mwanya huo kuwataka waratibu na wahasibu wa CHF kuhakikisha wanakuwa na akaunti za mfuko huo katika maeneo yao kwa kuwa hata Serikali imekubaliana na kuwepo kwa akaunti hizo.

"Tunataka ifikapo Machi mwakani kila Halamshauri iwe na akaunti ya CHF na hii itawezesha ukaguzi na ufuatiliaji wa fedha za mfuko huu na hasa namna zinavyotumika," alisema Rehani.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka waratibu kutambua kuwa kazi au jukumu walilonalo kwenye mfuko huo ni kubwa na linalohitaji kujituma bila kuweka maslahi yao mbele na badala yake waweke maslahi ya Watanzania hasa kuhakikisha huduma za afya zinakuwa bora zaidi.

"Waratibu mnatakiwa kutambua kuwa kazi mlinayo ni kubwa na wala msiendekeze malalamiko wala kujiuliza utanufaikaje, tuifanyeni hii kazi ili hata vizazi vijavyo vije vitambue kuwa kuna watu kweli walifanya jambo kwa maslahi ya Watanzania," alisema Rehani.

Kongamano hilo ambalo lina washiriki zaidi ya 300 kutoka katika halmashauri zote nchini lina lengo la kujadili mambo mbalimbali yanayohusiana na mfuko huo ili hatimaye yaweze kufikiwa mafanikio yanayotarajiwa ya kila mtanzania kuwa na bila ya afya.

Monday, December 19, 2011

Namna Kongamano la waratibu wa CHF lilivyofanyika

Kaimu Mkurugenzi wa CHF, Rehani Athuman akiwakaribisha washiriki wa kongamano la waratibu wa CHF

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emanuel Humba akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera katika kongamano la waratibu wa CHF

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emanuel Humba akiteta jambo na Kaimu Mkurugenzi wa CHF, Rehani Athuman

Wakiwa katika kongamano la Waratibu wa CHF

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emanuel Humba akitoa maelezo mafupi kwa washiriki wa kongamano la waratibu wa CHF

Baadhi ya Wakurugenzi wa NHIF (walioko mbele) wakiwajibika kwenye kongamano la waratibu wa CHF

Wakiteta jambo (Kikwazo cha CHF ni dawa Mkuu)

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emanuel Humba, Kaimu Mkurugenzi wa CHF, Rehani Athuman na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera wakiteta jambo kwenye kongamano la Waratibu wa CHF kutoka nchi nzima.

Wakuu hawa wakiteta jambo

KONGAMANO LA WARATIBU WA CHF MKOANI MOROGORO

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Joel Bendera akiwa na baadhi ya washiriki wa kongamano hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera akihutubiwa wana Kongamano

RC: CHF itafanikisha kuleta maisha bora

Na Grace Michael, Morogoro

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera amesema Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) una umuhimu mkubwa katika kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuleta maisha bora kwa Watanzania wote.

Amesema mafanikio ya CHF, kwa maana ya kuwa na idadi kubwa ya kaya zilizojiunga na huduma bora za tiba katika vituo vya matibabu, ndiyo dhamira ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, chini ya uongozi thabiti wa Rais Jakaya Kikwete.

Bendera aliyasema hayo jana mjini hapa wakati akifungua kongamano la waratibu wa CHF kutoka katika Halmashauri zote nchini, ambapo aliwasisitiza kuhakikisha wanaunga mkono kwa kuchapa kazi na kutimiza wajibu katika dhamira hiyo ili jambo hilo liwe na mafanikio makubwa.

"Ni ukweli ulio wazi kuwa gharama za matibabu zinapanda kila uchao, hivyo njia pekee ya kumkomboa Mtanzania ni kumpa uhakika wa kutibiwa yeye na familia yake kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii.

Wananchi wengi watakapojiunga na wakishirikishwa katika usimamizi wa huduma kupitia Bodi na Kamati za usimamizi wa vituo nina uhakika Halmashauri nyingi zitaondokana na changamoto ya ukosefu wa dawa kwa sababu watakuwa na fedha zinazowawezesha kuboresha huduma," alisema Bendera.

Alisema kuwa jambo hilo limewezekana katika baadhi ya Halmashauri hivyo linawezekana pia kwa Halmashauri zote.

"Kama ndugu zetu wa nchi jirani ya Rwanda wameweza kufikisha huduma za bima ya afya kwa zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wake, sisi pia tukijizatiti tunaweza kuwafikia Watanzania wote katika kipindi kifupi," alisema.

Akizungumzia usimamizi wa fedha, aliwataka Waratibu wa CHF kuhakikisha asilimia 66 ya fedha zinazotokana na uchangiaji wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na zile za Papo kwa Papo kutumika kununulia dawa.

Alisema kuwa endapo itafanyika hivyo itawezesha kuziba pengo la upungufu wa dawa hivyo akasisitiza kuhakikisha  usimamizi na udhibiti wa dawa vituoni unafanyika.

"Mahali penye uhalifu toeni taarifa katika mamlaka zinazohusika. Binafsi nisingependa fedha zilizolengwa katika ununuzi wa dawa zitumike katika kutengeneza magari na shughuli nyingine ambazo hazihusiki na huduma ya matibabu kwa mwanachama wa NHIF, CHF au mwananchi wa kawaida moja kwa moja," alisema Bendera.

Alisema kuwa fedha ambazo Serikali inatoa kama mchango wake wa Tele kwa Tele ni kuunga mkono juhudi za wananchi kuchangia huduma.

"Fedha hizo zitumike kununulia dawa. Kumbukeni kuwa Halmashauri zimeingia mkataba na Serikali Kuu kuhusu fedha hizo na matumizi yake. Fedha hizo si za kutoa kama sadaka kwa vikundi au watu wanaofanya shughuli zao katika Halmashauri. Kama kuna kikundi kinafanya shughuli zake hakikatazwi ili mradi kinafuata sheria lakini sio kitumie fedha hizi," alisema.

Alisema kuwa kila mwanachama anapoenda kwenye kituo cha matibabu anatarajia kupata huduma ya dawa na sio maneno mazuri ya kwa nini dawa hazipo hivyo akawaomba  Waratibu kwa kushirikiana na uongozi wa vituo vya matibabu vilivyo katika maeneo yao kuwajibika kushauri na kuhakikisha kuwa fedha zinazochangwa zinatumika kwa usahihi kwa kununulia dawa. Upatikanaji wa dawa ndio utakaowalindia heshima waratibu na kujenga uhalali wa kuendelea kuwepo kwa CHF.

Kutokana na hali hiyo aliwataka kuhakikisha dawa zinazotolewa na Serikali zitumike vizuri na kuratibiwa katika ngazi mbambali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Emanuel Humba, alisema kuwa tangu NHIF ikabidhiwe jukumu la kusimamia CHF, imefanya maboresho katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya kuongeza wigo kutoka kaya 120,000 hadi kaya 572,902 sawa na wanufaika 3,437,412.

Alisema imani na mtazamo wa wadau wa ndani na nje kuhusu CHF imeongezeka na hii imewezesha Mfuko kutunukiwa Cheti cha  heshima kutoka Taasisi inayojumuisha Mifuko ya hifadhi za jamii  duniani ISSA katika eneo la CHF.

Aidha alisema wamefanikiwa kulipa fedha za tele kwa tele kiasi cha sh.bilioni 3.3 bilioni hadi kufikia mwezi November 2011.

Tukifurahi kwa pamoja

Mambo yalikuwa kama hivi



Mambo ya kuongeza nondoooo

Editha Karlo akinipongeza

Kwa raha zanguuuu

Acha nifurahi mwaya

Neema Mgonja akinipongeza kwa hatua hiyo

Hongera mwaya

Irene Mark akinipongeza kutunukiwa stashahada ya uandishi wa habari katika Chuo cha Dar es Salaam (DSJ) Mwishoni mwa wiki iliyopita.

Zitto: Uchumi wa Taifa hatarini

Uchumi wa Taifa hatarini: Mfumuko wa Bei tishio kwa Serikali, Wafanyabishara na Wananchi.
Mfumuko wa Bei umezidi kuongezeka kama taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu inavyoonesha kwamba, wakati mfumuko wa bei mwezi Julai mwaka huu (Bajeti ya mwaka wa Fedha 2011/2012 ilipokuwa inaanza) ulikuwa asilimia 13, umefikia asilimia 19.2 mwezi Novemba. Hii maana yake ni kwamba, Bajeti ya Serikali iliyopitishwa na Bunge mwezi Juni 2011, imepunguza uwezo wa kununua bidhaa na huduma kwa takribani asilimia 6.

Hii ni sawa na shilingi 780 bilioni kuyeyuka katika Bajeti katika kipindi cha miezi Minne tu ya utekelezaji wa wake. Kutokana na kasi ya ukuaji wa Mfumuko wa Bei ni dhahiri kwamba, itakapofika mwisho wa mwaka wa Bajeti Serikali itakuwa imepoteza kwa kiasi kikubwa uwezo wa kununua bidhaa na huduma kwa zaidi ya robo ya Bajeti yake.

Hali ni mbaya zaidi kwa wananchi kwani Mfumuko wa Bei za vyakula umekua kwa kasi kikubwa mno. Ofisi ya Takwimu imeonesha kuwa wakati mfumuko wa Bei za vyakula ulikuwa asilimia 14.8 mwezi Julai, umefikia asilimia 24.7 mwezi Novemba 2011. Ukilinganisha na bei za vyakula mwaka 2010, mwananchi amepoteza uwezo wa kununua chakula kwa zaidi ya robo katika ya Novemba 2010 na Novemba 2011.

Jumla ya vyakula ambavyo mwananchi alinunua kwa shilingi 10,000 mwaka 2010, sasa atanunua kiwango kile kile kwa shilingi 12,500. Bei za vyakula zimeongezeka kwa kiwango hiki ilhali kipato cha mwananchi aghalabu kipo pale pale. Mwathirika mkubwa ni mwananchi wa kawaida wa kijijini ambaye mapato yake ni kidogo na hivyo sehemu kubwa huyatumia kununua chakula.

Ukiangalia kwa undani utakuta mfumuko wa bei wa bidhaa kama mchele, sukari, nyama na samaki umekua maradufu. Bei ya mchele imekua kwa asilimia 50, sukari asilimia 50, nyama asilimia 30 na Samaki kwa takribani asilimia 40. Bidhaa hizi zote ni muhimu sana kwa afya ya binadaamu na hasa watoto kwa upande wa vyakula vya protini.

Tusipokuwa makini na kupata majibu sahihi ya tatizo la mfumuko wa bei za vyakula, wananchi wengi na hasa watoto watapata utapiamlo na Taifa kuingia gharama kubwa katika kuwapatia huduma ya afya.

Kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula, mfumuko wa bei wa mafuta ya taa na gesi asilia unapaa kwa kasi kama moto wa nyikani. Wakati mafuta ya taa yamepanda bei kwa asilimia 71 katika ya mwezi Novemba mwaka 2010 na mwezi Novemba 2011, bei ya gesi asilia imepanda kwa asilimia 35.

Madhara ya hali hii ni makubwa mno maana wananchi watakimbilia kwenye matumizi ya mkaa na kuni, hata hivyo bei za mkaa zenyewe zimepanda kwa asilimia 24. Kwa hali hii, na kutokana na ukweli kwamba wananchi wengi wa Tanzania wapo kwenye mpaka wa umasikini na daraja la kati chini, juhudi za muongo mzima za kupunguza umasikini zitafutwa ndani ya mwaka mmoja tu.

Mfumuko wa Bei unasukuma Watanzania wengi zaidi kwenye dimbwi la umasikini, unapunguza uwezo wa Serikali kutoa huduma za jamii kupitia Bajeti na hata kutimiza mipango ya miradi ya maendeleo kama miundombinu ya barabara, umeme, bomba la gesi, madaraja nk. Mkakati mahususi unatakiwa kubadili hali hii. Hatua zifuatazo zinapendekezwa ili kuuhami uchumi na kupunguza upandaji wa kasi wa gharama za maisha.

1. Kuongeza uzalishaji wa chakula kwa kuweka mbinu za kukuza uchumi wa vijijini ni njia mojawapo endelevu ya kupunguza mfumuko wa Bei hapa nchini. Serikali sasa iache maneno matupu kuhusu sekta ya uchumi vijijini kwa kuelekeza nguvu nyingi huko. Serikali iruhusu na ivutie kwa kasi na kutoa vivutio kwa wazalishaji binafsi wa Sukari na mpunga katika mabonde makubwa. Waziri wa Kilimo na Maafisa wake watoke Ofisini na kuhimiza uzalishaji mashambani, fedha zielekezwe kujenga miundombinu ya barabara vijijini.

Vyakula vilivyolundikana mikoa ya Mbeya, Iringa na Rukwa ambapo Serikali iliahidi kununua na kutotimiza ahadi yake vinunuliwe mara moja na kusambazwa mikoa yenye shida ya chakula kama Mwanza, Mara, Kagera na mikoa ya Kaskazini. Chakula kukuta msimu mwingine katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ni kashfa kubwa kwa Serikali na inaonesha Serikali isivyokuwa makini na maisha ya wananchi.

Wakati huu ambapo tunaweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa chakula, Serikali inunue chakula cha kutosha na hasa mchele na sukari kutoka nje na kukisambaza kwenye soko ili kupunguza upungufu wa bidhaa (scarcity) katika masoko.

Mfumo uliotumika kununua Sukari tani laki moja hivi karibuni usitumike tena kwani ulizaa rushwa ya hatari na ufisadi ambao haujaripotiwa kwenye kutoa vibali. Wizara ya Kilimo iruhusu wauzaji kutoka nje walete sukari nchini moja kwa moja na kununuliwa na Bodi ya Sukari kisha kuiuza kwa wauzaji wa Jumla. Mfumo wa kutoa vibali umeonesha kutokuwa na tija na kwa kweli kunufaisha maafisa wachache wa Wizara ya Kilimo na Bodi ya Sukari.

2. Kitengenezwe kiwanda cha kutengeneza gesi ya matumizi nyumbani (LPG extraction plant) kwa haraka ili kupunguza bei ya gesi, kuepuka kuagiza gesi kutoka nje na hivyo kuokoa fedha za kigeni na kutengeneza ajira hapa nchini. Kupanda kwa bei ya gesi asilia kunatokana na kwamba Tanzania inaagiza gesi hii yote kutoka nje ilhali malighafi ya kutengeneza gesi ipo hapa Tanzania na kwa kweli huchomwa moto (flared). Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini liingie ubia na kampuni Binafsi ili kuwekeza katika kiwanda cha kuzalisha gesi hatimaye kushusha bei na hivyo kuwezesha wananchi wengi zaidi kutumia gesi kwa matumizi ya kupikia n.k, hivyo kutunza mazingira.

3. Ushuru wote unaokusanywa kwenye Mafuta ya Taa upelekwe Wakala wa Nishati Vijijini ili kufidia kupanda kwa bei ya mafuta ya Taa. Mfumuko wa Bei katika bidhaa ya mafuta ya taa unatokana na uamuzi wa kuwianisha bei ya mafuta ya taa na diseli ili kuondoa tatizo la uchakachuaji wa mafuta. Tatizo limeondoka (au hatulisikii tena) lakini wananchi wanaumia sana. Uamuzi sahihi wa kisera ni kupanua huduma za umeme vijijini kwa kuipa fedha zinazotokana na ushuru wa mafuta ya taa Wakala wa Umeme Vijijini. Usambazaji wa Umeme Vijijini utaongeza shughuli za kiuchumi vijijini, kukuza uchumi wa vijijini, kuongeza mapato ya wananchi kwa kuongeza thamani za mazao yao na hivyo kupunguza athari za mfumuko wa bei.

4. Sera ya Matumizi ya Serikali iangaliwe upya kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi yasiyo ya lazima, na kuelekeza fedha nyingi zaidi katika uwekezaji umma (public investments). Matumizi Mengineyo ya Serikali yanaongeza fedha kwenye mzunguko ama kwa kulipa watu wachache stahili mbalimbali kama posho n.k au kwa kununua bidhaa na huduma bila mpango, na hivyo kusukuma bei kuwa juu kinyume na uhalisia wa soko. Tafiti za mfumuko wa Bei Tanzania zinaonyesha kwamba sera za fedha na zile za matumizi (monetary and fiscal policy) zina nafasi kubwa katika kukuza mfumuko wa bei. Hivi sasa nakisi ya Bajeti inayopelekea Serikali kukopa kwa kwa kiwango kubwa inapandisha gharama za viwanda kukopa mitaji ya muda mfupi na hivyo kuongeza gharama za uzalishaji na kasha bei za bidhaa. Wizara ya Fedha ambayo mpaka sasa imekaa kama imeishiwa namna ya kufanya, inapaswa kuamka na kutoa maelekezo mapya kwa Wizara, Idara na Wakala za Serikali kuhusu namna ya kubana matumizi na kuziba mianya yote ya kukwepa kodi.
Hitimisho
Serikali imeonesha udhaifu mkubwa sana katika kusimamia uchumi katika nusu ya kwanza ya Bajeti ya mwaka 2011/2012 ambayo pia ni Bajeti ya kwanza ya kipindi cha pili cha Serikali ya awamu wa Nne. Kuna hatari ya dhahiri kwamba ifikapo mwezi Januari 2012 tutakuwa tumerejea mfumuko wa Bei wa kiwango cha mwaka 1992 (21.9%).

Tusipochukua hatua za haraka tutafikia na hata kuzidi mfumuko wa Bei kiwango cha juu kabisa ambacho kilifikiwa mwaka 1994 (33%) na hivyo viwanda kushindwa kukopa kwenye Mabenki kwa mahitaji yao ya haraka ya mitaji ya muda mfupi, wazalishaji wadogo kushindwa kulipa mikopo yao kwenye Taasisi za fedha na hivyo kufunga uzalishaji, Shirika la Umeme kushindwa kabisa kulipa gharama za mafuta ya kuendesha mitambo na kipato cha mwananchi kutomudu gharama za za kila siku. Uchumi utadorora kabisa. Taifa litakuwa hatarini.
Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania na Wizara ya Kilimo na Chakula iamke kuhami uchumi dhidi ya adui namba moja, Mfumuko wa Bei. Huu sio wakati wa kupiga porojo, viongozi wafanye kazi zao, Wananchi wajitume.

Inabidi sasa turejee kauli mbiu za miaka 50 iliyopita za Uhuru ni Kazi. Tuseme Demokrasia ni Kazi. Demokrasia sio lelemama.

Ndg. Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Waziri Kivuli Fedha na Uchumi
18 Disemba 2011

Tuesday, December 13, 2011

Miaka 50 ya uhuru

Mwandishi wa Habari wa Jambo Leo Grace Michael (mwenye koti jekundu) na Lina Denis wa Chanel Ten wakifuatilia sherehe za miaka 50 ya uhuru.

KUHITIMU RAHA EEH...

Consolata Mahanga (kushoto) akiwa na rafiki yake

 Happines Mahanga (kulia) akiwa na rafiki yake

Kusomesha ni jambo la msingi


Waalikwa wakipata vinywaji

Happy, Daniphod na Consolata Mahanga wakiwa na furaha katika hafla ya kuwapongeza kuhitimu elimu katika viwango mbalimbali.

Tumefanya kazi, tujipongeze


Dk Makongoro Mahanga akiwa na Mkewe Florence Mahanga wakicheza katika hafla ya kuwapongeza watoto wao Dan, Happy na Consolata kwa kuhitimu hatua mbalimbali za elimu.

Wakiwa katika tendo la kulishana keki


Watoto wa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira Makongoro Mahanga, Danphord, Happines na Consolata Mahanga wakiwa na marafiki zao katika hafla ya kuwapongeza kwa kumaliza elimu katika hatua mbalimbali.

Monday, December 12, 2011

Wakiwa katika hfala ya kuwapongeza Danford, Happy na Consolatha Mahanga watoto wa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira Makongoro Mahanga.

MAHANGA NA KUWAPONGEZA WANAWE KWA MASOMO

Mbunge wa Jimbo la Segerea Makongoro Mahanga akiwa na Fred Lowassa na Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Beno Malisa kwenye sherehe ya kuwapongeza Danford Mahanga, Happy Mahanga na Consolata Mahanga kwa kuhitimu elimu katika ngazi tofauti.

Saturday, December 10, 2011

Miaka 50 ya Uhuru bila maandamano haiwezekani

Wanafunzi wakiwa na mabango ya kupinga posho za wabunge.

MAHAFALI NA HEKA HEKA YA KUPINGA POSHO ZA WABUNGE

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili wakiwa katika heka heka ya kupinga kufanyika kwa mahafali ya tano ya chuo hicho mpaka Serikali ya Wanafunzi itakaporejeshwa na kupinga posho ya sh. 200,000 inayotolewa kwa wabunge.




NIDA: Tuko makini suala la Vitambulisho

Na Grace Michael

MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imesema kuwa hakuna haja ya kukimbizana katika mchakato wa utoaji wa vitambulisho hivyo kwa kuwa suala hilo ni nyeti na linalohitaji umakini wa kutosha ili kuepukana na udanganyifu wa taarifa unaoweza kujitokeza.

Kutokana na hali hiyo, Mamlaka hiyo inatarajia kuanza kutoa vitambulisho vya awali ifikapo Aprili mwakani na ni matarajio ya vitambulisho hivyo kutumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 hali itakayopunguza gharama kwa Serikali katika uboreshaji wa daftari la wapiga kura.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa NIDA, Dickson Maimu wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu hatua iliyofikiwa na mamlaka hiyo katika mchakato wa vitambulisho.

"Niseme tu kwamba hakuna sababu ya kukimbiza kwa haraka na hili suala, tunahitaji tutoe vitambulisho vilivyo bora...tupate taarifa zilizo sahihi kwani vitambulisho hivi vitamwezesha Mtanzania kupata huduma zote za msingi,"

"Suala la vitambulisho vya Taifa ni suala la usalama kwani vitaonesha nani ni nani, yuko wapi, anamiliki nini na anafanya nini, vitasaidia hata kuwatambua majambazi na ndio maana hata wakimbizi watapewa ili kwa lengo la kuwatambua wanachofanya hapa nchini na wako wapi," alisema Maimu.

Alisema ili kuweza kuwa na taarifa sahihi, mamlaka hiyo itashirikiana kwa karibu na Serikali za Mitaa, RITA pamoja na Uhamiaji hivyo akaomba ushirikiano wa pamoja ili kufanisha suala hilo na kuwa na matunda mazuri.

Alisema kuwa vitambulisho hivyo ni ufungup wa kuiunganisha mifumo mingine ya Serikali na binafsi katika kumletea maisha bora kila Mtanzania na kuhakikisha yanafikiwa malengo ya maendeleo ifikapo 2025.

Akizungumzia hatua iliyofikiwa alisema kuwa wameanza utambuzi na usajili wa wafanyakazi wa Serikali na kundi litakaofuatiwa ni la wanafunzi, wafanyabisahara na hatimaye umma kwa ujumla.

"Tutaanza kutoa vitambulisho Aprili 26, mwakani wakati wa maadhimisho ya sherehe za muungano kwa watumishi wa Serikali ambao tayari usajili wao umeanza," alisema Maimu.

Mamlaka hiyo itatoa vitambulisho katika makundi matatu ambayo ni pamoja Watanzania, wageni wakaazi na wakimbizi hivyo baada ya usajili kukamilika jukumu kubwa litakuwa ni uhakiki wa taarifa za makazi, umri na uraia wa mwombaji aliyesajiliwa ili kuweza kupata uhakiki wa taarifa zake kwa lengo la kumpa kitambulisho kinachowianana kundi lake.

Kutokana na hali hiyo, Maimu aliwaomba watendaji wote wa Serikali za mitaa kusaidia katika utambuzi na usajili wa watu kwenye maeneo yao lakini akawataka kuwa wazalendo na waadilifu wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo ili kuepukana na vitendo vyovyote vya rushwa pamoja na ukiritimba wowote unaoelekea kudai au kupokea rushwa.

Maimu pia alielezea faida za vitambulisho kuwa ni pamoja na kuimarisha usalama wa raia na mali zao, kupunguza vitendo vya uhalifu hasa unaofanywa na raia wa nje, kuweka kumbukumbu za matukio ya uhalifu katika daftari lakini pia vitasaidia kuboresha daftari la wapiga kura na kupunguza mzigo mkubwa kwa Serikali katika uboreshaji wa daftari hilo.

Aidha kitambulisho hicho kitatumika kusafiria kati ya nchi uanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashiriki , kuwatambua wananchi watakaonufaika na ruzuku za pembejeo za kilimo na kuiongezea Serikali wigo wa ukusanyaji mapato na hivyo kuboresha huduma za kijamii.

Friday, December 9, 2011

Baada ya miaka 50 ya uhuru tudumisheni amani

KILA mpenda nchi ya Tanzania angefurahi kuona nchi hii ikibaki kisima cha utulivu na amani, wakati wa maadhimishi ya miaka 50 ya uhuru, zana mbalimbali za kivita zilioneshwa na Jeshi la Wananchi (JWTZ).

Zana hizo ni vyema zikabaki kuoneshwa kwenye maadhimisho kama haya na si kuziona zikiwa tayari kwa kufanya kazi au kwa lolote.

Binafsi nilipoziona nilitamani kuwaomba Watanzania kuilinda amani tuliyonayo kwa gharama yoyote ili siku moja tufikie ndoto ya maisha bora kwa kila Mtanzania.

Mwito wangu kwa viongozi walioko madarakani ni kuhakikisha mnaepukana na rushwa, ufisadi na mambo mengine ambayo yanawakera wananchi na kuwafanya watamani kuingia hata kwenye migogoro.

Tungependa kuona viongozi sasa mkifanya kazi zenu kwa kuzingatia maadili ya kazi zenu na kwa maslahi ya Taifa letu.

Mungu ibari Tanzania.

Tuko imara Watanzania

Askari wa Kikosi cha Komando cha Jeshi la Wananchi Tanzania wakionesha uwezo wao wa kukabiliana na adui wakati wa hatari katika maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru.

Tumeweza Watanzania wenzangu tusonge mbele

Rais Jakaya Kikwete akiwapungia maelfu ya Watanzania katika uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam leo wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara.

Tumethubutu, tumeweza na tunasonga mbele

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emanuel Humba akiwa na ujumbe wa mfuko huo wakionesha tuzo ya ISSA mbele ya wanahabari waliyozawadiwa baada ya kuibuka washindi wa utoaji huduma bora.

'NHIF wanajitahidi eeh'

Grace Michael na Selina Wilson wakiteta jambo wakati NHIF ilivyoweka wazi sababu za kuibuka msindi na kupewa tuzo na ISSA.

NHIF ilivyoandika historia

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF akiwa na Maofisa wa Mfuko huo wakifurahia tuzo waliyopata kutoka ISSA baada ya kuibuka washindi wa kwanza katika utoaji wa huduma zao katika maeneo mbalimbali.

NHIF ilivyoandika historia kubwa ndani ya miaka 50 ya uhuru

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Emanuel Humba akionesha tuzo iliyotolewa kwa mfuko huo na Taasisi ya Kimataifa ya Mashirika ya Hifadhi ya Jamii Duniani (ISSA) baada ya kuibuka mshindi wa kwanza katika utoaji wa huduma bora katika maeneo mbalimbali.

JK afunguka miaka 50 ya uhuru

* Asema Tanzania itafanya mambo bila shinikizo
* Asema wakoloni waliiacha nchi ikiwa hoi
* Atamba hatua zilizofikiwa, asisitiza kuchapa kazi
* Atamba 2015 Tanzania itakuwa na Jeshi la Mfano

Na Grace Michael

RAIS Jakaya Kikwete jana aliwaongoza Watanzania katika maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru huku akisisitiza kuwa kamwe Tanzania haitaamliwa mambo yake na nchi nyingine.

Alisema kuwa amani, utulivu, mshikamano wa Watanzania ni mafanikio makubwa yaliyotokana na sera nzuri zilizoanzishwa na waasisi wa nchi hii akiwemo Mwalimu Julius Nyerere pamoja na viongozi waliofutia akiwemo Ally Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na yeye mwenyewe.

Kauli hiyo aliitoa katika maadhimisho hayo Dar es Salaam katika uwanja wa Uhuru ambapo, Rais Kikwete aliamua kuzungumza kutokana na umuhimu wa siku ya jana ambayo ilikuwa ni kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara.

"Niwahakikishie tu Watanzania wenzangu kuwa katika mambo tutakayoyafanya kamwe hatutaamuliwa na mtu yoyote...tutafanya tunachokiamua wenyewe kwani tunayo amani, utulivu, mshikamano na ni nchi ya aina yake," alisema Rais Kikwete.

Alisema kuwa katika safari ya miaka 50 ya uhuru nchi imepita katika changamoto mbalimbali na katika maadui watatu waliotangazwa baada ya kupata uhuru ambao ni umasikini, ujinga na maradhi nchi imepiga hatua katika mapambano dhidi ya maadui hao.

"Tuna mafanikio makubwa tena ya kujivunia ikilinganishwa na tulivyoachwa na wakoloni...walituacha weupe kabisa na kama barabara za lami waliacha ziko tatu tu ambazo ni Moshi- Arusha, Tanga- Korogwe na Dar es Salaam- Morogoro...walitugawa walipo wao ndio kulikuwa na umeme, maji na  lami lakini mtanzania alipo kama ni maji alipata ya debe," alisema Rais Kikwete.

Alisema kuwa pamoja na wakoloni kuiacha nchi ikiwa hoi lakini uongozi uliokuwepo baada ya uhuru na mpaka sasa umeweza kufanya kazi kubwa hali inayomwezesha Mtanzania kufika mahali popote kwa muda mfupi tofauti na hapo awali.

Alisema pamoja na mafanikio hayo, kama nchi bado kuna kazi ya kufanya kutokana na kasi ya mabadiliko na changamoto zilizopo hivi sasa hivyo kama Watanzania akawataka kuongeza bidii katika utendaji kazi ili kuweza kwenda sambamba na matarajio ya nchi.

"Niwakumbushe tu ambao hawalijui hili...waingereza hawakuacha chochote hivyo wananchi kamwe msivunjike moyo bado tuna kazi ya kufanya na cha kujivunia katika kipindi hiki tuna msingi mzuri," alisema Rais Kikwete.

Katika hatua nyingine Rais Kikwete aliwapongeza viongozi walioandaa na kuratibu maadhimisho hayo akiwemo Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Akizungumzia shamra shamra zilizokuwepo katika maadhimisho hayo, alilipongeza gwaride kwa namna lilivyojipanga lakini pia kuoneshwa kwa zana mbalimbali za kivita ambazo zinaonesha wazi kuwa nchi iko na zana za kutosha katika kuhakikisha ulinzi wake uko salama.

"Nadhani kila mmoja amejionea hapa vifaa na zana mbalimbali za kivita na hivyo ni baadhi tu kwani vingekuja vyote hapa pasingetosha na tunazidi kujiimarisha na ifikapo 2015 nchi yetu itakuwa na Jeshi la ambalo halikuwa na mfano," alisema Rais Kikwete.

Alisema kuwa kama Tanzania inayo mambo mengi ya kujivunia ambayo yameweka historia likiwemo la kupigana na kulisambaratisha Jeshi la Uganda hivyo hiyo ni ishara tosha kuwa Tanzania iko imara na itaendelea kuwa hivyo ili kuweza kulinda misingi iliyoachwa ikiwemo ya amani na utulivu.

Hata hivyo Rais Kikwete alitumia mwanya huo kuwakumbuka waasisi 17 ambao walikuwa mbele katika kupigania uhuru wa Tanzania Bara ambao alisisitiza kuwa kama nchi tunao wajibu wa kuwapa heshima kutokana na walichokifanya katika kipindi hicho.

"Ni lazima kuwatambua na kuwakumbuka kwa uamuzi wao wa kishujaa wa kudai uhuru wa nchi hii na kati ya waasisi hao 17 ni watatu tu ndio wapo hai na wengine 14 wametangulia mbele za haki...ni wajibu wetu kutoa heshima kwao kwani walifanya kazi kubwa," alisema.

Kutokana na hali hiyo, Rais Kikwete aliwaambia Watanzania kuwa katika miaka 50 ya uhuru ni dhahiri kuwa "Tumethubutu, Tumeweza na tunaendelea kusonga mbele".

Maadhimisho hayo mbali na wananchi kutoka katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, yalihudhuriwa na viongozi wa kitaifa wa ndani na nje wakiwemo marais wa nchi zingine ambapo Rais Kikwete alisema hiyo ni ishara ya ushirikiano ambapo aliahidi kuuendeleza.

NHIF yaweka historia miaka 50 ya Uhuru

Na Grace Michael

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya umeandika historia ndani ya miaka 50 ya uhuru kwa kuibuka mshindi wa kwanza wa ujumla Barani Afrika kwa Taasisi na Mashirika yanayotoa huduma za Hifadhi ya Jamii.

Ushindi huo umeufanya Mfuko huo kutunukiwa vyeti vitatu vya heshima kwa umahiri na jitihada za kuboresha huduma bora katika maeneo mbalimbali.

Akizungumzia ushindi huo Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emmanuel Humba, alisema kuwa ushindi huo si wa mfuko pekee bali umeleta heshima ya nchi nzima na Watanzania wake kwa ujumla.

Humba aliyataja maeneo ambayo yameufanya mfuko huo kuibuka kidedea ni pamoja na usimamizi wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) hasa kwenye kasi ya kuongezeka kwa wanaohudumiwa na mfuko huo katika kipindi kifupi tangu Serikali ilipokasimu madaraka kwa NHIF.

Huduma ya Vifaa tiba na watoa huduma na utoaji wa huduma uliowezesha kuboresha huduma na kupunguza ukubwa wa tatizo la dawa na vifaa tiba hivyo kutoa mchango muhimu katika maendeleo ya sekta ya afya nchini nalo ni eneo jingine ambalo liliufanya mfuko huo kutunukiwa vyeti.

"Utoaji wa mafao na kusogeza huduma za Mfuko karibu na wanachama wake kupitia ufunguzi wa ofisi za kanda nao uliwafanya wenzetu wa Taasisi ya Kimataifa ya Mashirika ya Hifadhi ya Jamii Duniani, (ISSA) kuona tunafaa kupata vyeti hivyo," alisema Humba.

Alisema tuzo hiyo ilitolewa mjini Arusha mapema wiki hii na Rais wa ISSA, Errol Frank kwenye mkutano wa wakuu wa mashirika ya pesheni na Bima za Afya kanda ya Afrika na NHIF iliwakilishwa na Mkurugenzi wa Uendeshaji Eugen Mikongoti.

Hata hivyo NHIF iliwahi kupata tuzo ya heshima kutoka kwa ISSA mwaka 2008, hivyo Humba akasema tuzo hiyo ina maana kubwa kwa mfuko kwa kuwa umeweza kuonesha kuwa umethubutu na umeweza.

"Tuzo hii imekuja wakati mwafaka kwani umedhihirisha kuwa ndani ya miaka 50 ya uhuru tumeweza...hii ni heshima kubwa kwa nchi na Mamlaka inayosimamia Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), lakini pia kwa wizara yetu ya Afya," alisema Humba.

Alisema kuwa mfuko unaamini kuwa imepata tuzo hiyo kutokana na mazingira na utamaduni wa Watanzania kujadiliana changamoto na kuzipatia ufumbuzi kwa pamoja na hivyo imefanikisha nchi kuonekana ni kivutio kwa mataifa mengine barani Afrika.

"Matarajio ya mfuko ni kuendelea kuzifanyia kazi changamoto za uboreshaji wa huduma...huduma za NHIF na CHF tunataka zifike ngazi ya chini kabisa ili wanachama waone umuhimu au faida za kujiunga...mtaji wa mtu yeyote ni afya yake hivyo kama mfuko hatuchezi na afya ya Mtanzania," alisema Humba.

Kutokana na hali hiyo, Humba alisema kuwa atakabidhi tuzo hiyo serikalini kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambayo ndiyo mama na mafanikio hayo yamepatikana kutokana na uongozi na ulezi mzuri.

"Nawashukuru sana Watanzania na wanachama wote kwa ujumla, tutaendelea kutambua mchango wenu kwa kuwapa huduma iliyo bora zaidi...tuna mafao ambayo nchi zingine zimeshindwa kuyatoa kwa wanachama wake," alisema Humba.

Miaka 50 ya uhuru tutafakari zaidi

Na Grace Michael

NAJISIKIA furaha kuona nchi yangu ikiadhimisha miaka 50 ya uhuru wake.
Nafarijika kwa kuwa nchi yangu ni kisima cha amani, imejaa utulivu tofauti na nchi zingine.

Nafurahi kuwaona Watanzania leo hii wakiandika historia kubwa ya muda wa miaka hiyo 50 tangu wapate uhuru wao, ambapo mbali na mambo mengine nchi imefanikiwa kupiga hatua katika nyanja mbalimbali.

Wakati tunaadhimisha maadhimisho haya ni vyema Watanzania tukatumia fursa hii kutafakari tulikotoka, tulipo na tunakokwenda.

Nasema hivyo kwa kuwa bila tafakari hiyo kamwe hatuwezi kufanya lolote katika safari inayoanza kesho ya miaka mingine 50 ya uhuru wetu.

Ikumbukwe kuwa pamoja na utulivu na amani iliyopo hapa nchini, lakini nchi ipo katika kipindi kigumu kwa kuwa yapo matatizo mbalimbali yanayowakabili wananchi ambayo kama hayatapatiwa ufumbuzi wa haraka tunaweza kubaki na utulivu tu lakini amani ikatoweka.

Ili mwananchi awe na amani ni lazima awe na uhakika wa maisha yake kwa mfano, vijana kuwa na uhakika wa ajira, wananchi kutokuwa na umasikini, upatikanaji wa huduma zote za kijamii uwepo wakati wote pamoja na familia za Watanzania kuwa na uhakika wa kuendesha maisha yake ya kila siku.

Kwa hali ya kawaida huwezi ukasema una amani huku huna fedha ya kugharamia matibabu ya mwanao au mwana familia wako, huwezi kuwa na amani wakati familia yako ikishinda na njaa, watoto kukosa huduma za elimu na mambo mengine mengi.

Hivyo pamoja na sifa kubwa iliyopo hapa nchini ambayo ni ya kudumisha amani, lakini ni vyema sasa wakati tukiadhimisha maadhimisho haya, Serikali ikafanya kila linalowezekana kuhakikisha inaweka mazingira rafiki kwa wananchi wake ili wapate vitu vya msingi ambavyo vitawafanya wadumishe hiyo amani.

Lakini pamoja na Serikali kuwa na mzigo wa kuweka mazingira hayo rafiki, na sisi kama wananchi tunao mzigo wa kuhakikisha tunafanya kazi zenye tija na si kukaa vibarazani tukitarajia Serikali ilete kila kitu.

Natambua nchi sasa iko katika mfumko mkubwa wa bei, wananchi wake wana umasikini mkubwa, tha
mani ya shilingi yetu imeshuka thamani mambo yote hayo yanasababisha kuongezeka kwa ugumu wa maisha.

Kutokana na hayo yote, kamwe tusije kudanganyika tukaipoteza amani na utulivu ambao viongozi waliopita walivilinda kwa gharama kubwa.

Nalazimika kusema hivyo kwani huwezi ukafanya kazi zozote za uzalishaji au maendeleo ukiwa katika migogoro au vita hivyo kwa maana hiyo ni lazima tuhakikishe amani iliyopo inalindwa.

Natambua hivi sasa Watanzania wanao uelewa mkubwa katika mambo mbalimbali ambao natarajia kila mmoja kwa nafasi yake atautumia katika kuijenga nchi yetu na si kuibomoa.
Mungu Tubariki Watanzania.

0782 35 66 88

Sumaye: Rushwa, ufisadi ni janga

* Ataka vita dhidi yake ipiganwe kwa pamoja
* Aifunda Chadema kuhusu Katiba Mpya

Na Grace Michael

WAZIRI Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye amesema kuwa bila kuwa na vita ya dhati na ya pamoja dhidi ya mapambano rushwa na ufisadi nchi itaangamia.

Sumaye aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika maonesho ya maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru ynayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere.

"Rushwa na ufisadi ni mambo yanayoangamiza Taifa letu na kama hatukuwa na umoja katika kupambana navyo Taifa litakwisha...vita hii isiachwe kwa Raifa peke yake tuipigane wote," alisema.

Alisema kuwa rushwa ni kikwazo kikubwa katika kuyafikia maendeleo ya kweli kwa kuwa ndiyo inasababisha kupokwa kwa haki za wanyonge, kutekelezwa kwa miradi chini ya kiwango, kupewa kazi mtu asiye na sifa za kufanya kazi hiyo hatua inayosababisha wananchi kuichukia hata Serikali yao.

Kutokana na hali hiyo aliwaomba Watanzania kuhakikisha mambo mabaya wanayapinga kwa uwazi ili yaweze kuachwa kwa maslahi ya umma.

*Asisitiza kulinda amani

Katika hatua nyingine, Sumaye alisema kuwa pamoja na matatizo ya umasikini ambayo bado yanawakabili wananchi wa Tanzania lakini kuna haja kubwa ya kuhakikisha amani inalindwa kwa nguvu zote.

"Nakubali kabisa kuwa unaweza ukakosa amani hata kama eneo lako halina vita, huwezi ukawa na amani huku ukiwa na matatizo ya njaa, huduma za msingi lakini ni lazima tutambue kuwa tunatakiwa kufanya kazi kufa na kupona ili kujikwamua na hali hii, hakuna Serikali inayoweza kumgawia mwananchi wake fedha bali inaweka mazingira mazuri," alisema.

Kutokana na hali hiyo alisisitiza kuwa ni lazima viangaliwe vitu vyote vinavyoweza kusababisha kutoweka kwa amani miongoni mwa wananchi ili vifanyiwe kazi na hatimaye amani iliyopo kubaki kama ilivyo.

Hata hivyo alisema kuwa Serikali inafanya juhudi mbalimbali katika kuhakikisha wananchi wake wanaachana na umasikini ikiwemo ya kutoa kipaumbele katika suala la kilimo ambalo linahusisha asilimia kubwa ya Watanzania.

*Anena kuhusu Katiba

Akizungumzia mchakato wa katiba ulivyo sasa, alisema kuwa hakuna haja ya kuwepo kwa malumbano katika hatua hizi za awali na ambazo zimefanyika kwa taratibu zinazotakiwa.

Alisema kuwa hoja zote zinazojadiliwa bungeni zinatakiwa kushindana kwa hoja na baada ya kutoka huko na kuwa mikononi mwa Rais ni vigumu kutengua hatua inayofuata.

"Kama kuna mbunge anapingana na hoja...ndo muda anaotakiwa kupambana na hoja hiyo bungeni huku wananchi wakimsikiliza lakini mbunge unapotoka kwa kususia hoja hiyo si njia sahihi sana kwani muswada huo ulipishwa bungeni na hatua iliyofuata ni Rais kutia saini na si vinginevyo," alisema.

Hata hivyo alisema kuwa hatua ambayo ni ya muhimu katika mchakato huo ni ya wananchi kutoa mawazo au maoni yao na si hatua hii hivyo akasema hakuna haja ya kulumbana kwa kuwa hata Serikali si mlemavu wa kusikia vilio vya wananchi hasa katika suala hili la Katiba.

*Umoja wa Kitaifa

Katika suala hilo, Sumaye alisema kuwa ni wakati wa Watanzania kukiri kuwa Umoja bado uko imara pamoja na kuwepo kwa mabadiliko ya mambo mbalimbali.

*Kupambana na umasikini, ujinga na Maradhi

Sumaye alisema kuwa katika kupambana na maadui hao watatu ambao walitangazwa mara tu baada ya kupata uhuru yapo mafanikio ambayo yamefikiwa pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali.

Kuhusu umasikini alisema kuwa ni lazima Watanzania kwa sasa tufanye kazi bila huruma ili tuweze kupambana na adui huyo.

Hata hivyo alisema kuwa changamoto alizopambana nazo Mwalimu Julius Nyerere ni tofauti kabisa na changamoto anazopambana nazo Rais Jakaya Kikwete kwa kuwa mambo mengi yamebadilika.

"Huwa najiuliza sijui Mwalimu alipataje hata Baraza la Mawaziri kwa kuwa watu walikuwa wachache lakini leo kuna wasomi wengi na ndio maana nasema yapo mabadiliko makubwa ambayo yamekuja na changamoto zake ambazo tunatakiwa kwa pamoja kupambana nazo," alisema Sumaye.

Alitumia mwanya huo kumpongeza Rais Kikwete kwa kuandaa utaratibu mzuri wa maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru ambao umewezesha wananchi kupata historia ya nchi yao kabla na baada ya uhuru.