Saturday, December 10, 2011

NIDA: Tuko makini suala la Vitambulisho

Na Grace Michael

MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imesema kuwa hakuna haja ya kukimbizana katika mchakato wa utoaji wa vitambulisho hivyo kwa kuwa suala hilo ni nyeti na linalohitaji umakini wa kutosha ili kuepukana na udanganyifu wa taarifa unaoweza kujitokeza.

Kutokana na hali hiyo, Mamlaka hiyo inatarajia kuanza kutoa vitambulisho vya awali ifikapo Aprili mwakani na ni matarajio ya vitambulisho hivyo kutumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 hali itakayopunguza gharama kwa Serikali katika uboreshaji wa daftari la wapiga kura.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa NIDA, Dickson Maimu wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu hatua iliyofikiwa na mamlaka hiyo katika mchakato wa vitambulisho.

"Niseme tu kwamba hakuna sababu ya kukimbiza kwa haraka na hili suala, tunahitaji tutoe vitambulisho vilivyo bora...tupate taarifa zilizo sahihi kwani vitambulisho hivi vitamwezesha Mtanzania kupata huduma zote za msingi,"

"Suala la vitambulisho vya Taifa ni suala la usalama kwani vitaonesha nani ni nani, yuko wapi, anamiliki nini na anafanya nini, vitasaidia hata kuwatambua majambazi na ndio maana hata wakimbizi watapewa ili kwa lengo la kuwatambua wanachofanya hapa nchini na wako wapi," alisema Maimu.

Alisema ili kuweza kuwa na taarifa sahihi, mamlaka hiyo itashirikiana kwa karibu na Serikali za Mitaa, RITA pamoja na Uhamiaji hivyo akaomba ushirikiano wa pamoja ili kufanisha suala hilo na kuwa na matunda mazuri.

Alisema kuwa vitambulisho hivyo ni ufungup wa kuiunganisha mifumo mingine ya Serikali na binafsi katika kumletea maisha bora kila Mtanzania na kuhakikisha yanafikiwa malengo ya maendeleo ifikapo 2025.

Akizungumzia hatua iliyofikiwa alisema kuwa wameanza utambuzi na usajili wa wafanyakazi wa Serikali na kundi litakaofuatiwa ni la wanafunzi, wafanyabisahara na hatimaye umma kwa ujumla.

"Tutaanza kutoa vitambulisho Aprili 26, mwakani wakati wa maadhimisho ya sherehe za muungano kwa watumishi wa Serikali ambao tayari usajili wao umeanza," alisema Maimu.

Mamlaka hiyo itatoa vitambulisho katika makundi matatu ambayo ni pamoja Watanzania, wageni wakaazi na wakimbizi hivyo baada ya usajili kukamilika jukumu kubwa litakuwa ni uhakiki wa taarifa za makazi, umri na uraia wa mwombaji aliyesajiliwa ili kuweza kupata uhakiki wa taarifa zake kwa lengo la kumpa kitambulisho kinachowianana kundi lake.

Kutokana na hali hiyo, Maimu aliwaomba watendaji wote wa Serikali za mitaa kusaidia katika utambuzi na usajili wa watu kwenye maeneo yao lakini akawataka kuwa wazalendo na waadilifu wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo ili kuepukana na vitendo vyovyote vya rushwa pamoja na ukiritimba wowote unaoelekea kudai au kupokea rushwa.

Maimu pia alielezea faida za vitambulisho kuwa ni pamoja na kuimarisha usalama wa raia na mali zao, kupunguza vitendo vya uhalifu hasa unaofanywa na raia wa nje, kuweka kumbukumbu za matukio ya uhalifu katika daftari lakini pia vitasaidia kuboresha daftari la wapiga kura na kupunguza mzigo mkubwa kwa Serikali katika uboreshaji wa daftari hilo.

Aidha kitambulisho hicho kitatumika kusafiria kati ya nchi uanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashiriki , kuwatambua wananchi watakaonufaika na ruzuku za pembejeo za kilimo na kuiongezea Serikali wigo wa ukusanyaji mapato na hivyo kuboresha huduma za kijamii.

No comments:

Post a Comment