* Asema Tanzania itafanya mambo bila shinikizo
* Asema wakoloni waliiacha nchi ikiwa hoi
* Atamba hatua zilizofikiwa, asisitiza kuchapa kazi
* Atamba 2015 Tanzania itakuwa na Jeshi la Mfano
Na Grace Michael
RAIS Jakaya Kikwete jana aliwaongoza Watanzania katika maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru huku akisisitiza kuwa kamwe Tanzania haitaamliwa mambo yake na nchi nyingine.
Alisema kuwa amani, utulivu, mshikamano wa Watanzania ni mafanikio makubwa yaliyotokana na sera nzuri zilizoanzishwa na waasisi wa nchi hii akiwemo Mwalimu Julius Nyerere pamoja na viongozi waliofutia akiwemo Ally Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na yeye mwenyewe.
Kauli hiyo aliitoa katika maadhimisho hayo Dar es Salaam katika uwanja wa Uhuru ambapo, Rais Kikwete aliamua kuzungumza kutokana na umuhimu wa siku ya jana ambayo ilikuwa ni kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara.
"Niwahakikishie tu Watanzania wenzangu kuwa katika mambo tutakayoyafanya kamwe hatutaamuliwa na mtu yoyote...tutafanya tunachokiamua wenyewe kwani tunayo amani, utulivu, mshikamano na ni nchi ya aina yake," alisema Rais Kikwete.
Alisema kuwa katika safari ya miaka 50 ya uhuru nchi imepita katika changamoto mbalimbali na katika maadui watatu waliotangazwa baada ya kupata uhuru ambao ni umasikini, ujinga na maradhi nchi imepiga hatua katika mapambano dhidi ya maadui hao.
"Tuna mafanikio makubwa tena ya kujivunia ikilinganishwa na tulivyoachwa na wakoloni...walituacha weupe kabisa na kama barabara za lami waliacha ziko tatu tu ambazo ni Moshi- Arusha, Tanga- Korogwe na Dar es Salaam- Morogoro...walitugawa walipo wao ndio kulikuwa na umeme, maji na lami lakini mtanzania alipo kama ni maji alipata ya debe," alisema Rais Kikwete.
Alisema kuwa pamoja na wakoloni kuiacha nchi ikiwa hoi lakini uongozi uliokuwepo baada ya uhuru na mpaka sasa umeweza kufanya kazi kubwa hali inayomwezesha Mtanzania kufika mahali popote kwa muda mfupi tofauti na hapo awali.
Alisema pamoja na mafanikio hayo, kama nchi bado kuna kazi ya kufanya kutokana na kasi ya mabadiliko na changamoto zilizopo hivi sasa hivyo kama Watanzania akawataka kuongeza bidii katika utendaji kazi ili kuweza kwenda sambamba na matarajio ya nchi.
"Niwakumbushe tu ambao hawalijui hili...waingereza hawakuacha chochote hivyo wananchi kamwe msivunjike moyo bado tuna kazi ya kufanya na cha kujivunia katika kipindi hiki tuna msingi mzuri," alisema Rais Kikwete.
Katika hatua nyingine Rais Kikwete aliwapongeza viongozi walioandaa na kuratibu maadhimisho hayo akiwemo Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Akizungumzia shamra shamra zilizokuwepo katika maadhimisho hayo, alilipongeza gwaride kwa namna lilivyojipanga lakini pia kuoneshwa kwa zana mbalimbali za kivita ambazo zinaonesha wazi kuwa nchi iko na zana za kutosha katika kuhakikisha ulinzi wake uko salama.
"Nadhani kila mmoja amejionea hapa vifaa na zana mbalimbali za kivita na hivyo ni baadhi tu kwani vingekuja vyote hapa pasingetosha na tunazidi kujiimarisha na ifikapo 2015 nchi yetu itakuwa na Jeshi la ambalo halikuwa na mfano," alisema Rais Kikwete.
Alisema kuwa kama Tanzania inayo mambo mengi ya kujivunia ambayo yameweka historia likiwemo la kupigana na kulisambaratisha Jeshi la Uganda hivyo hiyo ni ishara tosha kuwa Tanzania iko imara na itaendelea kuwa hivyo ili kuweza kulinda misingi iliyoachwa ikiwemo ya amani na utulivu.
Hata hivyo Rais Kikwete alitumia mwanya huo kuwakumbuka waasisi 17 ambao walikuwa mbele katika kupigania uhuru wa Tanzania Bara ambao alisisitiza kuwa kama nchi tunao wajibu wa kuwapa heshima kutokana na walichokifanya katika kipindi hicho.
"Ni lazima kuwatambua na kuwakumbuka kwa uamuzi wao wa kishujaa wa kudai uhuru wa nchi hii na kati ya waasisi hao 17 ni watatu tu ndio wapo hai na wengine 14 wametangulia mbele za haki...ni wajibu wetu kutoa heshima kwao kwani walifanya kazi kubwa," alisema.
Kutokana na hali hiyo, Rais Kikwete aliwaambia Watanzania kuwa katika miaka 50 ya uhuru ni dhahiri kuwa "Tumethubutu, Tumeweza na tunaendelea kusonga mbele".
Maadhimisho hayo mbali na wananchi kutoka katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, yalihudhuriwa na viongozi wa kitaifa wa ndani na nje wakiwemo marais wa nchi zingine ambapo Rais Kikwete alisema hiyo ni ishara ya ushirikiano ambapo aliahidi kuuendeleza.
No comments:
Post a Comment