Monday, December 19, 2011

RC: CHF itafanikisha kuleta maisha bora

Na Grace Michael, Morogoro

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera amesema Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) una umuhimu mkubwa katika kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuleta maisha bora kwa Watanzania wote.

Amesema mafanikio ya CHF, kwa maana ya kuwa na idadi kubwa ya kaya zilizojiunga na huduma bora za tiba katika vituo vya matibabu, ndiyo dhamira ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, chini ya uongozi thabiti wa Rais Jakaya Kikwete.

Bendera aliyasema hayo jana mjini hapa wakati akifungua kongamano la waratibu wa CHF kutoka katika Halmashauri zote nchini, ambapo aliwasisitiza kuhakikisha wanaunga mkono kwa kuchapa kazi na kutimiza wajibu katika dhamira hiyo ili jambo hilo liwe na mafanikio makubwa.

"Ni ukweli ulio wazi kuwa gharama za matibabu zinapanda kila uchao, hivyo njia pekee ya kumkomboa Mtanzania ni kumpa uhakika wa kutibiwa yeye na familia yake kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii.

Wananchi wengi watakapojiunga na wakishirikishwa katika usimamizi wa huduma kupitia Bodi na Kamati za usimamizi wa vituo nina uhakika Halmashauri nyingi zitaondokana na changamoto ya ukosefu wa dawa kwa sababu watakuwa na fedha zinazowawezesha kuboresha huduma," alisema Bendera.

Alisema kuwa jambo hilo limewezekana katika baadhi ya Halmashauri hivyo linawezekana pia kwa Halmashauri zote.

"Kama ndugu zetu wa nchi jirani ya Rwanda wameweza kufikisha huduma za bima ya afya kwa zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wake, sisi pia tukijizatiti tunaweza kuwafikia Watanzania wote katika kipindi kifupi," alisema.

Akizungumzia usimamizi wa fedha, aliwataka Waratibu wa CHF kuhakikisha asilimia 66 ya fedha zinazotokana na uchangiaji wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na zile za Papo kwa Papo kutumika kununulia dawa.

Alisema kuwa endapo itafanyika hivyo itawezesha kuziba pengo la upungufu wa dawa hivyo akasisitiza kuhakikisha  usimamizi na udhibiti wa dawa vituoni unafanyika.

"Mahali penye uhalifu toeni taarifa katika mamlaka zinazohusika. Binafsi nisingependa fedha zilizolengwa katika ununuzi wa dawa zitumike katika kutengeneza magari na shughuli nyingine ambazo hazihusiki na huduma ya matibabu kwa mwanachama wa NHIF, CHF au mwananchi wa kawaida moja kwa moja," alisema Bendera.

Alisema kuwa fedha ambazo Serikali inatoa kama mchango wake wa Tele kwa Tele ni kuunga mkono juhudi za wananchi kuchangia huduma.

"Fedha hizo zitumike kununulia dawa. Kumbukeni kuwa Halmashauri zimeingia mkataba na Serikali Kuu kuhusu fedha hizo na matumizi yake. Fedha hizo si za kutoa kama sadaka kwa vikundi au watu wanaofanya shughuli zao katika Halmashauri. Kama kuna kikundi kinafanya shughuli zake hakikatazwi ili mradi kinafuata sheria lakini sio kitumie fedha hizi," alisema.

Alisema kuwa kila mwanachama anapoenda kwenye kituo cha matibabu anatarajia kupata huduma ya dawa na sio maneno mazuri ya kwa nini dawa hazipo hivyo akawaomba  Waratibu kwa kushirikiana na uongozi wa vituo vya matibabu vilivyo katika maeneo yao kuwajibika kushauri na kuhakikisha kuwa fedha zinazochangwa zinatumika kwa usahihi kwa kununulia dawa. Upatikanaji wa dawa ndio utakaowalindia heshima waratibu na kujenga uhalali wa kuendelea kuwepo kwa CHF.

Kutokana na hali hiyo aliwataka kuhakikisha dawa zinazotolewa na Serikali zitumike vizuri na kuratibiwa katika ngazi mbambali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Emanuel Humba, alisema kuwa tangu NHIF ikabidhiwe jukumu la kusimamia CHF, imefanya maboresho katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya kuongeza wigo kutoka kaya 120,000 hadi kaya 572,902 sawa na wanufaika 3,437,412.

Alisema imani na mtazamo wa wadau wa ndani na nje kuhusu CHF imeongezeka na hii imewezesha Mfuko kutunukiwa Cheti cha  heshima kutoka Taasisi inayojumuisha Mifuko ya hifadhi za jamii  duniani ISSA katika eneo la CHF.

Aidha alisema wamefanikiwa kulipa fedha za tele kwa tele kiasi cha sh.bilioni 3.3 bilioni hadi kufikia mwezi November 2011.

No comments:

Post a Comment