Friday, December 9, 2011

NHIF yaweka historia miaka 50 ya Uhuru

Na Grace Michael

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya umeandika historia ndani ya miaka 50 ya uhuru kwa kuibuka mshindi wa kwanza wa ujumla Barani Afrika kwa Taasisi na Mashirika yanayotoa huduma za Hifadhi ya Jamii.

Ushindi huo umeufanya Mfuko huo kutunukiwa vyeti vitatu vya heshima kwa umahiri na jitihada za kuboresha huduma bora katika maeneo mbalimbali.

Akizungumzia ushindi huo Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emmanuel Humba, alisema kuwa ushindi huo si wa mfuko pekee bali umeleta heshima ya nchi nzima na Watanzania wake kwa ujumla.

Humba aliyataja maeneo ambayo yameufanya mfuko huo kuibuka kidedea ni pamoja na usimamizi wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) hasa kwenye kasi ya kuongezeka kwa wanaohudumiwa na mfuko huo katika kipindi kifupi tangu Serikali ilipokasimu madaraka kwa NHIF.

Huduma ya Vifaa tiba na watoa huduma na utoaji wa huduma uliowezesha kuboresha huduma na kupunguza ukubwa wa tatizo la dawa na vifaa tiba hivyo kutoa mchango muhimu katika maendeleo ya sekta ya afya nchini nalo ni eneo jingine ambalo liliufanya mfuko huo kutunukiwa vyeti.

"Utoaji wa mafao na kusogeza huduma za Mfuko karibu na wanachama wake kupitia ufunguzi wa ofisi za kanda nao uliwafanya wenzetu wa Taasisi ya Kimataifa ya Mashirika ya Hifadhi ya Jamii Duniani, (ISSA) kuona tunafaa kupata vyeti hivyo," alisema Humba.

Alisema tuzo hiyo ilitolewa mjini Arusha mapema wiki hii na Rais wa ISSA, Errol Frank kwenye mkutano wa wakuu wa mashirika ya pesheni na Bima za Afya kanda ya Afrika na NHIF iliwakilishwa na Mkurugenzi wa Uendeshaji Eugen Mikongoti.

Hata hivyo NHIF iliwahi kupata tuzo ya heshima kutoka kwa ISSA mwaka 2008, hivyo Humba akasema tuzo hiyo ina maana kubwa kwa mfuko kwa kuwa umeweza kuonesha kuwa umethubutu na umeweza.

"Tuzo hii imekuja wakati mwafaka kwani umedhihirisha kuwa ndani ya miaka 50 ya uhuru tumeweza...hii ni heshima kubwa kwa nchi na Mamlaka inayosimamia Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), lakini pia kwa wizara yetu ya Afya," alisema Humba.

Alisema kuwa mfuko unaamini kuwa imepata tuzo hiyo kutokana na mazingira na utamaduni wa Watanzania kujadiliana changamoto na kuzipatia ufumbuzi kwa pamoja na hivyo imefanikisha nchi kuonekana ni kivutio kwa mataifa mengine barani Afrika.

"Matarajio ya mfuko ni kuendelea kuzifanyia kazi changamoto za uboreshaji wa huduma...huduma za NHIF na CHF tunataka zifike ngazi ya chini kabisa ili wanachama waone umuhimu au faida za kujiunga...mtaji wa mtu yeyote ni afya yake hivyo kama mfuko hatuchezi na afya ya Mtanzania," alisema Humba.

Kutokana na hali hiyo, Humba alisema kuwa atakabidhi tuzo hiyo serikalini kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambayo ndiyo mama na mafanikio hayo yamepatikana kutokana na uongozi na ulezi mzuri.

"Nawashukuru sana Watanzania na wanachama wote kwa ujumla, tutaendelea kutambua mchango wenu kwa kuwapa huduma iliyo bora zaidi...tuna mafao ambayo nchi zingine zimeshindwa kuyatoa kwa wanachama wake," alisema Humba.

No comments:

Post a Comment