Na Grace Michael
NAJISIKIA furaha kuona nchi yangu ikiadhimisha miaka 50 ya uhuru wake.
Nafarijika kwa kuwa nchi yangu ni kisima cha amani, imejaa utulivu tofauti na nchi zingine.
Nafurahi kuwaona Watanzania leo hii wakiandika historia kubwa ya muda wa miaka hiyo 50 tangu wapate uhuru wao, ambapo mbali na mambo mengine nchi imefanikiwa kupiga hatua katika nyanja mbalimbali.
Wakati tunaadhimisha maadhimisho haya ni vyema Watanzania tukatumia fursa hii kutafakari tulikotoka, tulipo na tunakokwenda.
Nasema hivyo kwa kuwa bila tafakari hiyo kamwe hatuwezi kufanya lolote katika safari inayoanza kesho ya miaka mingine 50 ya uhuru wetu.
Ikumbukwe kuwa pamoja na utulivu na amani iliyopo hapa nchini, lakini nchi ipo katika kipindi kigumu kwa kuwa yapo matatizo mbalimbali yanayowakabili wananchi ambayo kama hayatapatiwa ufumbuzi wa haraka tunaweza kubaki na utulivu tu lakini amani ikatoweka.
Ili mwananchi awe na amani ni lazima awe na uhakika wa maisha yake kwa mfano, vijana kuwa na uhakika wa ajira, wananchi kutokuwa na umasikini, upatikanaji wa huduma zote za kijamii uwepo wakati wote pamoja na familia za Watanzania kuwa na uhakika wa kuendesha maisha yake ya kila siku.
Kwa hali ya kawaida huwezi ukasema una amani huku huna fedha ya kugharamia matibabu ya mwanao au mwana familia wako, huwezi kuwa na amani wakati familia yako ikishinda na njaa, watoto kukosa huduma za elimu na mambo mengine mengi.
Hivyo pamoja na sifa kubwa iliyopo hapa nchini ambayo ni ya kudumisha amani, lakini ni vyema sasa wakati tukiadhimisha maadhimisho haya, Serikali ikafanya kila linalowezekana kuhakikisha inaweka mazingira rafiki kwa wananchi wake ili wapate vitu vya msingi ambavyo vitawafanya wadumishe hiyo amani.
Lakini pamoja na Serikali kuwa na mzigo wa kuweka mazingira hayo rafiki, na sisi kama wananchi tunao mzigo wa kuhakikisha tunafanya kazi zenye tija na si kukaa vibarazani tukitarajia Serikali ilete kila kitu.
Natambua nchi sasa iko katika mfumko mkubwa wa bei, wananchi wake wana umasikini mkubwa, tha
mani ya shilingi yetu imeshuka thamani mambo yote hayo yanasababisha kuongezeka kwa ugumu wa maisha.
Kutokana na hayo yote, kamwe tusije kudanganyika tukaipoteza amani na utulivu ambao viongozi waliopita walivilinda kwa gharama kubwa.
Nalazimika kusema hivyo kwani huwezi ukafanya kazi zozote za uzalishaji au maendeleo ukiwa katika migogoro au vita hivyo kwa maana hiyo ni lazima tuhakikishe amani iliyopo inalindwa.
Natambua hivi sasa Watanzania wanao uelewa mkubwa katika mambo mbalimbali ambao natarajia kila mmoja kwa nafasi yake atautumia katika kuijenga nchi yetu na si kuibomoa.
Mungu Tubariki Watanzania.
0782 35 66 88
No comments:
Post a Comment