* Ataka vita dhidi yake ipiganwe kwa pamoja
* Aifunda Chadema kuhusu Katiba Mpya
Na Grace Michael
WAZIRI Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye amesema kuwa bila kuwa na vita ya dhati na ya pamoja dhidi ya mapambano rushwa na ufisadi nchi itaangamia.
Sumaye aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika maonesho ya maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru ynayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere.
"Rushwa na ufisadi ni mambo yanayoangamiza Taifa letu na kama hatukuwa na umoja katika kupambana navyo Taifa litakwisha...vita hii isiachwe kwa Raifa peke yake tuipigane wote," alisema.
Alisema kuwa rushwa ni kikwazo kikubwa katika kuyafikia maendeleo ya kweli kwa kuwa ndiyo inasababisha kupokwa kwa haki za wanyonge, kutekelezwa kwa miradi chini ya kiwango, kupewa kazi mtu asiye na sifa za kufanya kazi hiyo hatua inayosababisha wananchi kuichukia hata Serikali yao.
Kutokana na hali hiyo aliwaomba Watanzania kuhakikisha mambo mabaya wanayapinga kwa uwazi ili yaweze kuachwa kwa maslahi ya umma.
*Asisitiza kulinda amani
Katika hatua nyingine, Sumaye alisema kuwa pamoja na matatizo ya umasikini ambayo bado yanawakabili wananchi wa Tanzania lakini kuna haja kubwa ya kuhakikisha amani inalindwa kwa nguvu zote.
"Nakubali kabisa kuwa unaweza ukakosa amani hata kama eneo lako halina vita, huwezi ukawa na amani huku ukiwa na matatizo ya njaa, huduma za msingi lakini ni lazima tutambue kuwa tunatakiwa kufanya kazi kufa na kupona ili kujikwamua na hali hii, hakuna Serikali inayoweza kumgawia mwananchi wake fedha bali inaweka mazingira mazuri," alisema.
Kutokana na hali hiyo alisisitiza kuwa ni lazima viangaliwe vitu vyote vinavyoweza kusababisha kutoweka kwa amani miongoni mwa wananchi ili vifanyiwe kazi na hatimaye amani iliyopo kubaki kama ilivyo.
Hata hivyo alisema kuwa Serikali inafanya juhudi mbalimbali katika kuhakikisha wananchi wake wanaachana na umasikini ikiwemo ya kutoa kipaumbele katika suala la kilimo ambalo linahusisha asilimia kubwa ya Watanzania.
*Anena kuhusu Katiba
Akizungumzia mchakato wa katiba ulivyo sasa, alisema kuwa hakuna haja ya kuwepo kwa malumbano katika hatua hizi za awali na ambazo zimefanyika kwa taratibu zinazotakiwa.
Alisema kuwa hoja zote zinazojadiliwa bungeni zinatakiwa kushindana kwa hoja na baada ya kutoka huko na kuwa mikononi mwa Rais ni vigumu kutengua hatua inayofuata.
"Kama kuna mbunge anapingana na hoja...ndo muda anaotakiwa kupambana na hoja hiyo bungeni huku wananchi wakimsikiliza lakini mbunge unapotoka kwa kususia hoja hiyo si njia sahihi sana kwani muswada huo ulipishwa bungeni na hatua iliyofuata ni Rais kutia saini na si vinginevyo," alisema.
Hata hivyo alisema kuwa hatua ambayo ni ya muhimu katika mchakato huo ni ya wananchi kutoa mawazo au maoni yao na si hatua hii hivyo akasema hakuna haja ya kulumbana kwa kuwa hata Serikali si mlemavu wa kusikia vilio vya wananchi hasa katika suala hili la Katiba.
*Umoja wa Kitaifa
Katika suala hilo, Sumaye alisema kuwa ni wakati wa Watanzania kukiri kuwa Umoja bado uko imara pamoja na kuwepo kwa mabadiliko ya mambo mbalimbali.
*Kupambana na umasikini, ujinga na Maradhi
Sumaye alisema kuwa katika kupambana na maadui hao watatu ambao walitangazwa mara tu baada ya kupata uhuru yapo mafanikio ambayo yamefikiwa pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali.
Kuhusu umasikini alisema kuwa ni lazima Watanzania kwa sasa tufanye kazi bila huruma ili tuweze kupambana na adui huyo.
Hata hivyo alisema kuwa changamoto alizopambana nazo Mwalimu Julius Nyerere ni tofauti kabisa na changamoto anazopambana nazo Rais Jakaya Kikwete kwa kuwa mambo mengi yamebadilika.
"Huwa najiuliza sijui Mwalimu alipataje hata Baraza la Mawaziri kwa kuwa watu walikuwa wachache lakini leo kuna wasomi wengi na ndio maana nasema yapo mabadiliko makubwa ambayo yamekuja na changamoto zake ambazo tunatakiwa kwa pamoja kupambana nazo," alisema Sumaye.
Alitumia mwanya huo kumpongeza Rais Kikwete kwa kuandaa utaratibu mzuri wa maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru ambao umewezesha wananchi kupata historia ya nchi yao kabla na baada ya uhuru.
No comments:
Post a Comment