Sunday, May 29, 2011

Dkt. Mahanga aja na mkakati wa uhamasishaji

Na Grace Michael

MBUNGE wa Jimbo la Segerea Dkt. Makongoro Mahanga ameahidi kuendesha kampeni ya uhamasishaji kwa wananchi ili wajenge tabia ya kufanya kazi kwa kujituma na kuondokana na dhana iliyojengeka ya kulaumu serikali katika kila jambo.

Dkt. Mahanga aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na majira namna alivyojipanga katika kuwatumikia wananchi wa jimbo lake ili waweze kujikwamua na hali ngumu ya maisha.

"Kwanza kinachotakiwa kufanyika ni kuwahamasisha wananchi ili wajenge utamaduni wa kujituma katika kazi...maendeleo hayawezi yakamfuata mwananchi ambaye hajitumi na wala hafuatilii hata fursa zilizopo, nitafanya kila linalowezekana ili wananchi wa jimbo langu watambue kwanza umuhimu wa kujituma na baada ya hapo tutafanikiwa katika kujikomboa," alisema Dkt. Mahanga.

Alisema kuwa hata kama Serikali ingetoa mabilioni ya fedha kwa wananchi lakini bila kuwepo kwa dhana ya uwajibikaji wa kujituma katika shughuli za uzalishaji hakuna kitu kitakachofikiwa hivyo akasisitiza kuwepo kwa ubunifu na kuongeza bidii katika shughuli za uzalishaji.

"Wapo wananchi wanatambua umuhimu wa kujituma katika kazi na ndio maana wanafanikiwa na kuwa katika hali nzuri ya maisha lakini wapo ambao bado hawajaelewa umuhimu wa kufanya kazi hivyo suala hili nitalieleza kwa wananchi ili walielewe hata serikali inapoweka nguvu yake kunakuwa na matunda mazuri," alisema Dkt. Mahanga na kuongeza.

Alitumia mwanya huo kuwaomba wananchi kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kujikwamua lakini akasisitiza umuhimu wa kujiunga kwenye vikundi ambavyo vinarahisisha upatikanaji wa mitaji au mikopo kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo.

"Kidole kimoja huwa hakivunji chawa hivyo vikundi vina faida yake na umuhimu mkubwa kwanza hata namna ya kusaidiwa inakuwa ni rahisi kwa kuwa serikali haiwezi kuona mtu mmoja mmoja," alisema.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa ana mpango wa kukutana na makundi ya aina mbalimbali wakiwemo vijana, akina mama na wengine ili kuona ni namna gani makundi hayo yanaweza kujikomboa katika umasikini na kuwa katika hali nzuri ya maisha kama sera ya Chama Cha Mapinduzi inavyotaka.

Akizungumzia kero zilizoko jimboni mwake zikiwemo za barabara, maji na zingine alisema ziko katika hatua ya kutatuliwa na baadhi yake tayari fedha zimetengwa kwa ajili ya kuzitatua.

No comments:

Post a Comment