Friday, May 27, 2011

Kamati yataka mkazo fedha za dawa

Na Grace Michael

KAMATI ya Bunge ya Huduma za Jamii imeitaka Serikali kuweka mkazo kwa kutenga fedha zinazotosheleza mahitaji ya ununuzi wa dawa ili kuondokana na adha ya ukosefu wa dawa katika vituo vya kutolea huduma.

Imesema bila wananchi kuwa na afya zilizoimarika hakuna maendeleo yoyote yatakayofikiwa hivyo ni lazima eneo la ununuzi wa dawa liwekewe mkazo kwa kuwa na fedha za kutosha.

Mapendekezo hayo yalitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bi. Magreth Sitta wakati kamati yake ilipotembelea Bohari ya Dawa (MSD) na kukagua shughuli zinazofanywa na bohari hiyo.

"Bila kuwa na afya njema taifa haliwezi kusonga mbele ni lazima akina mama wapate huduma nzuri za matibabu pamoja na watoto lakini pia wananchi kwa ujumla hivyo kwa namna tulivyoelezwa na kuona hali halisi ya ufinyu wa bajeti unaofanya bohari kushindwa kutimiza malengo yake ni lazima serikali iangalie eneo hili kwa umakini," alisema Bi. Sitta.

Bi. Sitta aliweka bayana kuwa MSD inashindwa kufikia lengo la upatikanaji wa dawa kwa asilimia 100 kutokana na chgangamoto zilizopo kubwa ikiwa ni ukosefu wa fedha.

Kamati hiyo pia ilipata fursa ya kuhoji namna ufuatiliaji wa dawa unavyofanyika kutoka MSD hadi kwa walaji kwa lengo la kukabiliana na wizi wa dawa ambao unadaiwa kufanyika katika maeneo mbalimbali.
Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa MSD, Bw. Joseph Mgaya aliweka wazi kuwa kazi ya bohari hiyo ni kununua, kuhifadhi na kusambaza dawa hizo na haina jukumu la kufuatilia namna dawa hizo zinavyotumika katika maeneo husika.

"MSD haina jukumu la kugagua dawa hizo baada ya kumaliza makabidhiano na wahusika au waombaji...kwa upande wetu tuna mifumo ambayo iko wazi ambapo mwombaji huomba na kukabidhiwa dawa kwa maandishi hivyo kama kuna wizi wa dawa unafanyika baada ya dawa hizo kutoka mikononi mwetu hatuna jukumu hilo," alisema Bw. Mgaya.

Akizungumzia kiwango cha upatikanaji wa dawa kwa sasa, alisema ni asimilia 80 inayopatikana na imekuwa vigumu kwa bohari hiyo kufikisha asilimia 100 kutokana na mazingira inayokumbana nayo yakiwemo ya ufinyu wa bajeti lakini pia utegemezi wa kununua dawa nje kwa asilimia 80.

Bw. Mgaya pia alieleza namna bohari inavyolipa kodi ya foroda na ya ongezeko la thamani kwa vifaa vya hospitali vinavyoingizwa nchini na idara hiyo imekuwa ikilipa adhabu ya asilimia 120 kwa mifuko ya plastiki malipo ambayo yanaongeza gharama kubwa kwa idara.

"Tunaomba kamati ishauri serikali kufuta malipo ya kodi kwa vifaa vya hospitalini na adhabu kwa mifuko ya kuwekea dawa," aliomba Bw. Mgaya.

Pia alitumia mwanya huo kueleza namna sheria ya manunuzi inavyokuwa kikwazo katika mchakato wa ununuzi wa dawa ambapo alisema kuwa ununuzi wa dawa za kuokoa maisha ya wananchi unatakiwa kutofautishwa na manunuzi ya huduma zingine hivyo akaomba kuangaliwa kwa suala hilo.

"Suala jingine ni hali isiyoridhisha ya utunzaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma ambapo dawa nyingi zinaharibika kutokana na utunzaji mbovu hivyo naiomba kamati kuishauri serikali ijenge miundombinu itakayotunza ubora wa dawa," alisema Bw. Mgaya.

Akizungumzia kuongezeka kwa madeni alisema kuwa hadi Aprili mwaka huu, kiwango cha deni la serikali kimeongezeka na kufikia sh. bilioni 40 na sehemu kubwa ni dawa za mradi msonge.

MSD kwa sasa inasambaza dawa hadi kwenye vituo vya kutolea huduma katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani na Shinyanga hatua iliyopongezwa na wananchi kutokana na kufika dawa hizo kwa wakati.

No comments:

Post a Comment