Thursday, May 19, 2011

Serikali yaanzisha taasisi ya maadili

Na Grace Michael

KATIKA kuhakikisha inapambana na changamoto zinazotokana na uongozi mbovu na ukosefu wa maadili, serikali imeanzisha taasisi maalumu kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa viongozi wa ngazi za juu yatakayowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Taasisi hiyo inayojulikana kwa jina 'Uongozi Institude' inatarajia kutoa mafunzo yatakayo wajengea uwezo zaidi viongozi walioko madarakani pamoja na kuandaa vijana watakao kuwa viongozi hapo baadaye.

Akizundua Bodi ya Wakurugenzi wa taasisi hiyo Dar es Salaam jana, Rais Jakaya Kikwete, alisema Tanzania na nchi nyingine barani afrika zinakabiliwa na uhaba wa viongozi wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi, jambo ambalo linakwamisha ukuaji wa maendeleo.

Rais Kikwete alisema changamoto hizo zinazorudisha maendeleo nyuma zinaweza kuondoka endapo viongozi watajengewa uwezo utakaofanya kuwajibika na kufuata misingi sheria na utawala bora.

Alisema changamoto hizo ni pamoja na kudorora kwa uchumi, kasi ndogo ya ukuaji wake, uhaba wa chakula, mfumuko wa bei katika sekta ya nishati ya mafuta na uwezo mdogo klatika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Kutokana na hali hiyo, Rais Kikwete ameiagiza Bodi ya taasis hiyo kuhakikisha kuwa inakuja na mbinu mpya zitakazowawezesha viongozi kukabiliana na changamoto mpya zinazoibuka hasa kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia.

Aliseka kuwa serikali ya Tanzania itatoa ushirikiano kwa taasisi hiyo ili kuhakikisha inafanya kazi iliyokusudiwa na viongozi wake watashiriki katika mafunzo mbalimbali ili wajenge uwezo zaidi wa kiuongozi.

"Tumetoa hekari 400 kwa ajili ya taasisi hii, hatukuwahi kuwa na chuo cha ngazi ya juu kama hiki, hivyo bodi mnalo jukumu la kuhakikisha mnaongeza wigo nje ya Tanzania kwa kuwa azma ni kuona taasisi inafahamika Afrika nzima kama kituo bora cha maendeleo ya uongozi," alisema Rais.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Prof. Joseph Semboja alisema kuwa taasisi hiyo inafanya kazi na viongozi kutoka ngazi za juu serikalini lakini pia ina mpango wa kujumuisha viongozi wa makampuni na taasisi za kiraia na viongozi kutoka mataifa mengine.

"Taasisi hii itawasaidia viongozi kufanya vizuri katika kutimiza jukumu lao kuendeleza jamii ili iweze kutumia fursa za maendeleo barani Afrika katika mfumo endelevu, uongozi ndio nguzo ya maendeleo hivyo viongozi wanatakiwa kuelewa mambo kwa mtazamo mpana, ajenda ya maendeleo ya Taifa na athari zake kutokana na muktadha wa ukanda wa Afrika na dunia," alisema Prof. Semboja.

Alisema kuwa ili maendeleo yaweze kufikiwa ni lazima viongozi wawe ni watu wa kuona mbali na watu wanaowatumikia wawe na imani nao lakini pia wawe mfano wa kuigwa na wengine ili kutimiza malengo na utekelezaji wa malengo yaliyokusudiwa.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa taasisi itafanya kazi na viongozi kwa lengo la kuendeleza agenda ya taifa na kusimamia utekelezaji wa mikakati ya taifa, kuchambua na kuelewa mambo mapya yanayoathiri maendeleo kitaifa, kikanda na kimataifa na kutafsiri athari zake kwa taifa lakini pia kuafuatilia maslahi ya nchi katika kanda ya Afrika na dunia.

"Tutawasaidia viongozi kwa kutoa programu za kuimarisha uongozi, kusaidia maendeleo ya sera na uchambuzi pamoja na mitandao ya kubadilishana ujuzi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi Bi. Ritva Koukku alisema kuwa lengo la taasisi hiyo ni kuboresha uwajibikaji wa viongozi na watendaji wa ngazi za juu serikalini, ombwe ambalo linazidi kuwa kubwa.

Alisema ukubwa wa changamoto zilizopo zinahitaji nguvu ya pamoja na ushirikiano kati ya nchi na nchi, ndio maaana selikali ya Finland imekubali kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuhakikisha lengo hilo linafikiwa.

Uzinduzi huo ulihudhuliwa na viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri, mabalozi, makatibu wakuu na viongozi wengine wa ngazi za juu serikalini.

No comments:

Post a Comment