Thursday, May 19, 2011

Serikali yapinga Zombe kulipwa fidia

Na Grace Michael

UPANDE wa Serikali katika kesi ya madai ya sh. bilioni tano iliyofunguliwa na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Abdallah Zombe umesema  mlalamikaji hana madai ya msingi dhidi ya serikali hivyo kumtaka athibitishe.

Bw. Zombe aliishitaki serikali akidai mabilioni hayo ya fedha kutokana na madai ya kunyanyaswa, kudhalilishwa na kubambikiziwa kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wanne wa madini kutoka mkoani Morogoro.

Kwa mujibu wa hati ya majibu iliyowasilishwa Mahakama Kuu na upande wa Serikali, si kweli kwamba kitendo cha ukamataji uliyofanywa dhidi ya Bw. Zombe haukufuata sheria kama mlalamikaji anavyodai.

Pia upande huo unadai kuwa madai ya mlalamikaji kuwa hakupewa haki ya kusikilizwa kwa mujibu wa sheria si ya kweli na polisi walifuata utaratibu wa sheria ikiwa ni pamoja na taratibu zote za kumkamata.

Hati hiyo inaeleza kuwa Bw. Zombe hana sababu za msingi za kuidai serikali kwa kuwa katika hati ya madai ameshindwa kuthibitisha uvunjwani wa sheria dhidi yake wakati akikamatwa.

Pamoja na madai hayo, Upande wa Serikali unaieleza mahakama kuwa kesi ya madai ya Bw. Zombe dhidi ya serikali si halali kwa sasa kutokana na kuwepo kwa rufaa dhidi ya uamuzi wa awali wa Mahakama Kuu ambayo ilimwachia huru Bw. Zombe katika kesi ya mauaji wa watu wanne.

Mlalamikaji katika kesi hiyo anatetewa na Wakili Richard Rweyongeza ambapo kesi hiyo ilitajwa jana Mahakama Kuu ya Tanzania na mahakama hiyo kumwamuru mlalamikaji kujibu majibu ya serikali Mei 23, mwaka huu.

Kesi hiyo ambayo iko mbele ya Jaji Upendo Msuya mbali na kupangwa tarehe ya Bw. Zombe kujibu majibu ya serikali pia imepangwa kutajwa Juni 20 mwaka huu.

Katika madai ya mlalamikaji, anadai kuwa Jeshi la Polisi lilikiuka sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 inayotaka kabla ya mtu kukamatwa aelezwe sababu zilizomfanya akamatwe lakini pia ni lazima achukuliwe maelezo yake ambayo baadaye hutumika mahakamani kama kielelezo.

“Jeshi la polisi lilikwenda kinyume na sheria hiyo kwani lilinikamata, na kunifungulia kesi hiyo ya mauji bila ya hata ya kunihoji wala kuchukua maelezo yangu, hivyo sikupewa haki zangu wakati wa kukamatwa,” anadai Bw. Zombe.

Bw. Zombe aliachiwa huru Agosti 17, mwaka 2009 baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuona hana hatia dhidi ya kesi ya mauaji ya watu hao wanne.

No comments:

Post a Comment