Thursday, May 26, 2011

Mauaji ya Tarime yasiwe mtaji wa kisiasa

Na Grace Michael

HAKUNA asiyekumbuka kilichotokea alfajiri ya Mei 16 mwaka huu, pale Nyamongo
wilayani Tarime ambapo watu watano waliuawa na wengine kujeruhiwa katika mapambano kati ya Polisi na wananchi waliodaiwa kuvamia mgodi wa North Mara kwa lengo la kupora mawe ya dhahabu.

Tukio hilo halikuwa zuri machoni pa Watanzania kwa kuwa limeacha simanzi kwa  ndugu jamaa na marafiki wa marehemu, lakini pia limepoteza nguvu kazi kwa hao waliouawa katika mapambano hayo.

Nina hakika kwamba tukio hilo limesababishwa na baadhi ya watendaji waliopewa  mamlaka ya kushughulikia matatizo ya wananchi wa eneo hilo kutotimiza wajibu wao ipasavyo.

Vitendo vya wenye mamlaka kutotimiza mahitaji ya wananchi vimejenga chuki miongoni mwa jamii hatua inayosababisha wananchi wengi sasa kujikuta wakijichukulia sheria mkononi hatua ambayo huwa ni mbaya kwa kuwa huambatana na athari kama zilizotokea huko Tarime.

Utakubaliana na mimi kuwa matukio yote yanayoendelea kutokea Tarime tangu kuuawa
kwa wananchi hao yanatokana na wananchi kuichoka Serikali yao kwa kuwa
imeshindwa kutatua kwa muda mrefu madai yao.

Itakumbukwa baada ya kufanyika mauaji hayo, Mbunge wa Jimbo la Tarime Bw.
Nyambari Nyangwine pengine kwa kutimiza wajibu wake kwa wananchi anaowawakilisha
alimua kufunga safari kwa lengo la kwenda kuzungumza na wananchi wake lakini
alichokipata huko anakijua mwenyewe.

Wananchi hao walisikika waziwazi wakisema ‘Hatumtaki mbunge wala Serikali’ sasa
maneno hayo yanaishara mbaya kwa taifa letu kwa kuwa Serikali ndio huwa chombo
ambacho kinaheshimika na kila mtu hivyo kuona wana Tarime wakiikataa hadharani
ni mwanzo mbaya.

Mbali na kitendo cha wananchi hao kumkimbiza mbunge wao na kuushambulia msafara wake, lakini pia wananchi hao wameonekana kuendelea kukereka na mchakato
unaofanywa hasa wa kufikia hatua ya maziko ya ndugu zao.

Tayari mgogoro uliibuka wakati wa uchukuaji maiti ambapo Polisi walidaiwa kuchukua maiti hizo bila ridhaa ya ndugu hatua inayozidi kuimarisha chuki miongoni mwa wananchi wa Tarime lakini pia kutokana na mgogoro huo, umesababisha baadhi ya wabunge wa CHADEMA na makada wengine kuwekwa rumande.

Matukio yote haya yasipoangaliwa kwa umakini, yataleta mgogoro wa kudumu wilayani humo hatua itakayowafanya wananchi wa wilaya hiyo kuishi bila amani.

Ni wakati sasa umefika kwa Serikali kuketi kitako na kuona ni namna gani matatizo hayo yanafanyiwa kazi na hatimaye wananchi hao waweze kuishi kwa amani na wafurahie uwekezaji uliofanywa kwenye eneo lao.

Ni ukweli usiopingika kuwa amani haiwezi ikawepo wakati wananchi wamezama kwenye
tope la ufukara huku wakiona rasilimali zilizopo katika maeneo yao zikitumika bila wao kunufaika nazo.

Nadhani mahitaji makubwa ya wana Tarime ni kuwezeshwa kwa kupewa maeneo yatakayowasaidia wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao za kiuchumi lakini suala hili limekuwa gumu katika utekelezaji wake.

Kutotekelezwa kwa suala hilo ndiko kulichochea wananchi hawa kufanya maandamano ambayo ukiyaangalia kwa umakini unagundua hitaji lao ni kudai haki ambayo wanaona kama imepokwa na wa kuirejesha hawapo.

Mbaya zaidi badala ya kusimamiwa kwa tatizo hilo na kushughulikiwa kwa maana ya kutatua mgogoro uliopo, suala hilo sasa limefanywa kuwa la kisiasa CCM na CHADEMA wanataka kutumia mauaji hayo kuwa mtaji wa kisiasa.

Ninachotaka kusema hapa ni kuwa Serikali sasa ifike pahala imalize tatizo hili ili amani irejeshwe kwa wananchi hawa kwa kuwa bila amani hakuna shughuli yoyote ya maendeleo inayoweza kufanyika katika eneo lao.

Lakini pamoja na hayo, wanasiasa nanyi tumieni nafasi zenu za kisiasa kwa mambo yanayowahusu na si kupandikiza chuki kwa wananchi ambayo baadae inaweza ikasababisha uvunjifu wa amani kwa maslahi yenu badala ya taifa.

Mnayo haki ya kushughulikia matatizo ya wananchi lakini si kwa ajili ya maslahi yenu ya kisiasa kwa kuwa mwisho wake utakuwa ni mbaya.

Kutokana na hayo ni vema sasa sheria za nchi na taratibu zilizopo zikafuatwa ili kuondokana na migogoro ambayo mwisho wa siku inasababisha mauaji kama yaliyotokea kwa wenzetu wa Tarime.

Haki haiwezi kupatikana kwa nguvu bali itapatikana endapo watu wenye hekima na busara zao wataketi kisha kujadiliana na hatimaye kukubaliana namna ya kufanya.

Yaliyotokea Tarime ni aibu na doa kwa nchi yetu kwa sababu itaonekana kuwa haina
misingi ya sheria na utawala bora.

gracemichaelkisinga@yahoo.com

Mwisho.

No comments:

Post a Comment