Thursday, May 26, 2011

Wazee Tarime walaani kushambuliwa msafara wa mbunge

Na Grace Michael

SAKATA la kupopolewa mawe kwa msafara wa Mbunge wa Jimbo la Tarime, Bw. Nyambari Nyangwine ambalo lilitokana na tukio la mauaji ya watu watano, limechukua sura mpya baada ya Mwakilishi wa wazee wa kimila jimboni humo Bw. Enock Chambili kulaani kitendo hicho.

Mbali na kulaani kitendo hicho, pia amekemea vitendo vya uchochezi vinavyodaiwa kufanywa na baadhi ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kuwataka wabunge hao watumie muda huo kuhamasisha maendeleo na si uchochezi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana, Bw. Chambili alisema kuwa wananchi wa Tarime hawana utamaduni wa kupiga viongozi wao hivyo kitendo cha kushambulia msafara wa mbunge kilisababishwa na uchochezi wa wanasiasa kwa ajili ya maslahi yao binafsi.

"Wanasiasa ambao hawahusiki jimboni Tarime wasilete uchochezi kwa wananchi na hatimaye wakaturejesha tulikotoka katika mapigano ya kimila, ni vyema wakatumia muda wanaokuja Tarime kuchochea majimboni mwao na si kuleta vurugu kwetu," alisema Bw. Chambili.

Alisema kuwa kinachotakiwa ni kuwaacha wananchi wa Tarime wafanye maamuzi yao wenyewe lakini pia waishi kwa amani na kuendelea na shughuli zao za maendeleo.

Hata hivyo alisema kuwa ni vyema sasa madai ya wananchi wa Nyamongo yakashughulikiwa kwa haraka ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara.

"Ni kweli wananchi wanayo madai yao ambayo yamekuwa ni ya muda mrefu sasa, hawawezi wakavumilia kuona wawekezaji wakinufaika huku wao wakiwa na umasikini mkubwa hivyo kinachotakiwa ni wananchi waendelezwe na wanufaike na uwekezaji na kuboreshewa huduma za kijamii ambazo kimsingi walikubaliana nao," alisema Bw.Chambili.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa suala la kutekeleza madai ya wananchi wa Nyamongo ni la Msingi ili kumaliza migongano iliyopo.

Naye Mbunge wa Jimbo hilo, Bw. Nyangwine aliwataka wanasiasa kutotumia nafasi zao za kisiasa kwa maslahi binafsi ambayo yanasababisha uvunjifu wa amani jimboni mwake.
"Tarime ima mamlaka kalimi kwa maana ya serikali pamoja na uwakilishi hivyo matatizo ya Tarime yanaweza kutatuliwa ndani ya mamlaka hiyo na si wabunge wa chama fulani kuja Tarime na kutoa maamuzi yao," alisema.

Alisema hayuko tayari kuvumilia hali hiyo ikitokea kwa wananchi wake hivyo akawaomba wananchi wa jimbo lake wamuunge mkono kupingana na uchochezi unaofanywa na wanasiasa hao.
Mei 16, mwaka huu mamia ya wakazi wa Nyamongo wilayani Tarime walivamia hifadhi ya mgodi wa North Mara kwa lengo la kutaka kuchukua mchanga wa dhahabu hatua iliyosababisha mauaji ya wananchi watano.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment