Sunday, May 22, 2011

Ongezeni bidii kwenye kazi-Dkt. Mahanga


Na Grace Michael
WANANCHI wametakiwa kutambua kuwa njia pekee ya kujikwamua katika hali ngumu ya maisha na kuondokana na umasikini ni kuongeza bidii katika shughuli za uzalishaji ili ziwe za ufanisi na tija.
Hata hivyo wametakiwa kuondoa kasumba ya kubaki wakiilaumu serikali kwa kila jambo na badala yake watimize wajibu wao kwa kufanya kazi kwa ufanisi huku serikali kwa upande wake ikiboresha mazingira yatakayowezesha kufanyika kwa shughuli za maendeleo bila matatizo.
Hayo yalisemwa juzi na Mbunge wa Jimbo la Segerea, Dkt. Makongoro Mahanga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kazi na Ajira wakati akizindua umoja wa VICOBA 10 katika Mtaa wa Tembomgwaza, Kata ya Kimanga, Dar es Salaam.
“Ebu ifike mahali tuache kasumba ya kurusha lawama kwa serikali kuwa imeshindwa kuondoa umasikini, kila mmoja wetu ajiangalie katika lawama hizo amechangia kwa kiasi gani...huwezi ukawa unalaumu na wakati kazi unayofanya ni kukaa mabarazani na kucheza bao kila kukicha ...ni kweli serikali kuna mambo inayotakiwa kufanya hasa kwa kuweka mazingira mazuri kwa wananchi wake lakini pia wananchi nao wana wajibu wa kujituma kufanya kazi ili kuongeza uzalishaji kwani maendeleo hayaji kwa kubweteka,” alisema Dkt. Mahanga.
Alisema kuwa hakuna serikali yoyote duniani ambayo inaweza ikagawa fedha kwa kila mwananchi wake kwa lengo la kutatua matatizo aliyonayo bali kinachoweza kufanywa na serikali ni kuwasaidia wananchi kwenye makundi ikiwemo kuwakopesha mitaji ili waweze kuzalisha zaidi lakini pia kujiajiri wenyewe.
“Uwekezaji wa pamoja una faida kubwa zikiwemo za kupata kiurahisi elimu ya kuendesha shughuli za uzalishaji, mitaji, mikopo kutoka kwenye taasisi mbalimbali za fedha lakini pia hata serikali ni rahisi kutambua kundi la watu wengi na kulisaidia tofauti na mtu mmoja mmoja,” alisema Dkt. Mahanga.
Akizungumzia muungano wa vicoba hivyo, aliwataka kuhakikisha wanakuwa na Mfuko wa pamoja ambao utawafanya waongeze uaminifu hasa kwa taasisi za fedha wakati wanapohitaji mikopo.
Katika hafla hiyo jumla ya sh. Milioni mbili zilichangwa kwa lengo la kutunisha mifuko ya vicoba hivyo huku Dkt. Mahanga akikubali ombi la wana VICOBA hao ambao walimwomba kuwa mlezi wa umoja huo.
Alisema kuwa yuko tayari kushirikiana na wana vikundi hao kwa kuwatafutia wataalam kwa ajili ya kuwapa elimu ya namna ya kuendesha shughuli zao pamoja na mambo mengine.
Dkt. Mahanga alitumia mwanya huo kuwaeleza wananchi namna kero zinazowakabili hasa za maji na barabara zitakavyoshughulikiwa.
“Jamani nadhani mtakubali kabisa kuwa kero kubwa kwa kata yetu ya Kimanga ni maji na barabara na kero hizi tumeamua kuzipa kipaumbele kwa maana ya kutaka kuziondoa haraka ili wananchi wapate unafuu...fedha zimetengwa kwa lengo la kumaliza kero ya maji Dar es Salaam hivyo mwaka 2015 hatutaki kuja kwenu kwa ahadi ya maji,” alisema Dkt. Mahanga.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment