Na Grace Michael
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) umeitaka serikali kuhakikisha inapunguza utegemezi wa bajeti kutoka kwa wafadhili kwa kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kupunguza ukubwa wa serikali.
“Ikizingatiwa kuwa bajeti ya serikali ni tegemezi kwa kiasi kikubwa kwa wafadhili na deni la taifa linazidi kukua kutoka sh. trilioni 7.6 (2008/2009) hadi sh. trilioni 10.5 (2009/2010) ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 38, je, ni kwa vipi serikali inapanga kuongeza ukubwa wa bajeti wakati deni linazidi kukua na ikizingatiwa mikopo na misaada ya wafadhili haitabiriki...ni vyema sasa kuangalia namna ya kupunguza ukubwa wa serikali,” ilisema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na mtandao huo na kusainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Bi. Ussu Mallya, mtandao huo mbali na kuomba kupunguzwa kwa utegemezi lakini pia unaitaka serikali kutenga rasilimali za kutosha zitakazowezesha mchakato wa mabadiliko ya katiba kufanyika kwa ufanisi zaidi.
Taarifa hiyo ilihusu namna kikosi kazi cha mtandao huo kilivyochambua muongozo wa mpango wa miaka mitano wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2011/2012 hadi 2015/16 ambapo uchambuzi huo umefanywa kwa mtazamo wa ukombozi wa wanawake kimapinduzi, wakiongozwa na kaulimbiu ya “Haki ya Uchumi, Rasilimali ziwanufaishe wanawake walioko pembezoni”.
“Tunataka ushiriki zaidi wa wananchi katika mchakato mzima wa kutengeneza katiba mpya ili kuainisha vipaumbele vyao... mikakati ya kuimarisha soko la bidhaa za ndani kwa kuimarisha barabara za vijijini zitakazosaidia kuchukua mazao ya wakulima wadogo ambao wengi wao ni wanawake ili kuinua pato la ndani la taifa na kuimarisha uchumi mkuu lakini mikakati maalumi ya kuongeza ajira, maisha endelevu na kipato kwa wote, wanawake na wanaume, mijini na vijijini,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
TGNP inataka ushiriki wa wananchi katika michakato yote ya bajeti kuanzia mwanzo ili mambo yote muhimu yaweze kuingizwa na kupewa bajeti ya kutosha.
Alisema kuwa mategemeo ya muongozo huo wa bajeti yalikuwa kuona msimamo wa serikali katika kutetea haki na usawa wa kila mwananchi, kwa kuelekeza rasilimali za kutosha ili kufanikisha mchakato huu wa mabadiliko ya katiba, ambao ndio mhimili kwa wapiga kura walio wengi, hasa wanawake walioko pembezoni ikiwa ni pamoja na makundi mengine ya watu wanaoishi na ulemavu aina zote, VVU na UKIMWI.
Taarifa hiyo ilisema kuwa mwongozo wa bajeti ni lazima ulenge namna uchumi wa nchi utakavyojenga maisha ya watu wake kwanza, na si kuangalia tu wawekezaji wa ndani na nje ya nchi na suala la ajira na maisha endelevu kwa wote liwekewe kipaumbele.
Akirejea muongozo wa bajeti unasisitiza uimarishaji na uendelezaji wa masuala ya uchumi mpana na siasa kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, kuzuia mfumuko wa bei, kuendeleza sekta binafsi, kusimamia usawa katika bei ya mafuta kwa kuwekeza kupitia rasilimali watu.
“Sisi kama wanaharakati tulitarajia kuona muongozo huu wa bajeti unaweka kipaumbele katika kusimamia mgawanyo sawa wa rasilimali katika jamii, kurasimisha kazi zisizo na kipato zinazofanywa na wanawake na wanaume walioko pembezoni, tunataka kuwe na mdahalo mpana wa kitaifa juu ya mawazo haya, maana
inaweza kuleta matokeo hasi kwa maendeleo ya uchumi wa taifa,” alisema.
“Vilevile tunapinga suala la kuweka kipaumbele katika uuzaji wa bidhaa nje ya nchi kwa wawekezaji wakubwa wakati soko la ndani la bidhaa linakufa.”
Vipaumbele vilivyoainishwa katika muongozo wa bajeti kwa mpango wa miaka mitano 2011/12-1025/16 vimeelekezwa zaidi kwenye Kilimo, miundo mbinu, viwanda, uwekezaji katika rasilimali watu, mazingira endelevu, usimamizi wa ardhi, mipango miji na makazi,kuimarisha mahusiano kati ya sekta ya umma na binafsi na kuendeleza mafanikio katika sekta za kijamii.
No comments:
Post a Comment