Na Grace Michael
HAKUNA ubishi kuwa Katiba mpya inahitajika haraka ili ikidhi mahitaji ya sasa na kwa kulitambua hilo, Serikali imekubali kuanza mchakato huo ili wenye katiba kwa maana ya wananchi waamue ni kitu gani kiwe ndani ya katiba na nini kusiwemo.
Hatua ambayo imefikiwa na Serikali kwa sasa ni kuandaa muswada ambao utaruhusu kutungwa kwa katiba mpya ambao mbali na kuruhusu ndio unaotoa mwongozo wa nini kifanyike ili kufikia hatua ya kuwa na katiba mpya kama yalivyo mahitaji ya kila mmoja.
Muswada huo unatarajiwa kuwasilishwa katika mkutano wa tatu wa bunge 10 unaoanza kesho mjini Dodoma.
Pamoja na hatua hiyo kufikiwa, lakini bado wananchi wanayo haki ya kuendelea kutoa mawazo yao juu ya muswada huo na kwa kuzingatia hilo, juzi wasomi wa kada mbalimbali wakiwemo wanasheria, wanasiasa, wanaharakati na wananchi kwa ujumla walikutana Dar es Salaam kwa ajili ya kongamano ambalo lilijikita kujadili muswada huo.
Katika majadiliano hayo, ambayo kwa namna moja ama nyingine ndiyo yanatoa mwanga kwa wananchi wa kawaida kutokana na mazingira halisi ya muswada ulivyo.
Katika mjadala huo, hoja mbalimbali ziliibuliwa zikiwemo za mapungufu makubwa yaliyoko ndani ya muswada lakini jambo ambalo limenivuta na kuamua kuandika ukurasa huu ni hoja iliyowasilishwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Peter Maina ambaye alihoji sababu ya muswada huo kuandaliwa kwa lugha ya Kiswahili.
Hoja hii ilinivuta na kunionesha ukweli kuwa kuandaliwa kwa lugha ya kingereza si sahihi kwa kuwa muswada huo unatakiwa ueleweke ipasavyo kwa wananchi ambao ndio hasa walengwa au wamiliki wa katiba.
Nakubaliana na mhadhiri huyo kuwa robo tatu ya watanzania watabaki gizani kwa maana ya kutouelewa vyema muswada huo ambao endapo utapitishwa ndio utatungiwa sheria hivyo ingekuwa ni busara kwa serikali ikaona umuhimu wa kuandaa muswada huo kwa lugha ambayo kila mmoja angeisoma na kuielewa ili ajipange namna ya kuchangia maoni yake kwenye katiba tarajiwa.
Kila mmoja atakubaliana na mimi kuwa Katiba si ya serikali wala si mtu binafsi na wala si ya chama chochote cha siasa bali ni mali ya watanzania hivyo jambo la msingi ambalo ningetarajia lifanyike ni muswada huo kuwekwa katika lugha rafiki ambayo kila mmoja kwa nafasi yake angeuelewa.
Kuwekwa kwa lugha ya kingereza ni kuwanyima au kutaka wananchi wengine wasielewe na wasipoelewa kuna hatari kubwa ya wananchi hao kutoshiriki ipasavyo katika utoaji maoni yao wakati wa mchakato wa katiba inayotarajiwa kuandikwa hivyo ingekuwa ni jambo la busara serikali ikatambua kuwa suala la katiba si la mzaha hata kidogo kwa kuwa haki ya kila mmoja imo ndani ya chombo hicho.
Jambo jingine ambalo ningependa kulizungumzia ni muswada huo kuvizuia kwa vyama vya siasa kuelimisha wananchi, sidhani kama hilo ni sawa, ingekuwa vyema vyama navyo vikatumika katika kuelimisha wananchi ili waweze kutoa michango yao vyema wakati utakapofika wa kutoa maoni yao.
Nasema kwa kuwa uelimishaji ungesaidia hata wananchi kubaini mambo mbalimbali lakini pia wangepata mwamko wa kutoa maoni ya mambo wanayoona yakiwekwa ndani ya katiba yatasaidia kwa kiasi kikubwa.
Kutokana na hali hiyo, Serikali inatakiwa kuwa sikivu na kuchukua mawazo mazuri yanayotolewa na wadau mbalimbali na kuyafanyia kazi ili hatimaye tuweze kupata katiba ambayo itadumu au itakidhi matakwa ya wengi kwa muda mrefu.
Lakini wakati wa uchangiaji mawazo ingekuwa vyema kila mmoja akaheshimu mawazo ya mwingine nah ii inatokana na kila mtu kuwa na mawazo yake hivyo kila mawazo yanayotolewa yaheshimiwe kwa kuwa mwisho wa siku yapo mawazo yatakayochukuliwa na kuachwa hivyo hakuna sababu ya kukatishana tama katika mchakato huu.
Nimelazimika kusema hivyo kwa kuwa hali ya kudharau michango ya wengine ilijionesha dhahiri katika kongamano hilo wakati Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mashariki alipozomewa jukwaani wakati akitoa mchango wake kuhusiana na mjadala uliokuwepo wa kujadili muswada huo.
Jambo hili ni zito hivyo sisi kama Watanzania tunatakiwa kuonesha umoja wetu na ushirikiano katika jambo hili ili liweze kupita katika mchakato wote kwa amani na liwe na mafanikio ya kutosha.
Endapo tutaanza kuoneshana ubabe katika utoaji wa michango yetu mwisho wake utakuwa ni mbaya hivyo ni vyema mawazo ya kila mmoja yakaheshimiwa kwa kiwango kikubwa kwa kuwa kila mmoja wetu ana haki ya kusema au kuchangia suala hilo.
Kwa upande wa wanasiasa nao watangulize maslahi ya taifa mbele na kuachana na maslahi binafsi katika mchakato huu na kama maslahi ya nchi yatatangulizwa tutapata Katiba nzuri na ambayo kila mmoja wetu ataifurahia.
Mungu ibariki Tanzania
0755 23 42 57
Mwisho
No comments:
Post a Comment