Tuesday, May 24, 2011

Mfumko wa bei za dawa unatisha-NHIF


Na Grace Michael
SERIKALI imetakiwa kuangalia uwezekano wa kuwa na chombo cha kudhibiti na kuangalia bei za dawa ili kukabiliana na tatizo la mfumko wa bei unaozidi kuongezeka kila kukicha.
Ombi hilo lilitolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bw. Emanuel Humba mbele ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Haji Mponda ambaye alitembelea mfuko huo kwa lengo la kuangalia namna majukumu ya mfuko yanavyotekelezwa.
“Katika kutekeleza majukumu yetu, bado tunazo changamoto kadhaa lakini kubwa zaidi ni ukosefu wa huduma bora vijijini hali inayochangia kwa kiasi kikubwa wananchi kutojiunga na mfuko wa afya wa jamii na kama inavyojulikana kuwa wanachama wetu wengi wako vijijini hivyo kuna haja ya kuangalia namna ya kuboresha huduma hizi,” alisema Bw. Humba.
Alisema kuwa tatizo jingine ambalo limekuwa ni changamoto kwa mfuko huo ni ongezeko la bei za dawa ambapo alitumia mwanya huo kumwomba Waziri mwenye dhamana kuliangalia suala hilo kwa jicho la pekee ili kuokoa maisha ya watanzania ambao wengi wao hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
“Kwa kweli tunaomba suala hili liangaliwe kwa upana wake, kwani hata sisi tunalazimika kutumia nguvu ya ziada kuhakikisha wanachama wetu wanapata  huduma za matibabu hasa dawa lakini ukiangalia kuna wananchi ambao hawana uwezo wa kumudu bei za dawa na ndio maana vijijini wanafikia hatua ya kugawa kidonge kimoja na kugawana na mgonjwa mwingine,” alisema Bw. Humba.
Bw. Humba alielezea matarajio ya Mfuko huo ambapo alisema kuwa wanatarajia kuongeza wigo wa wanachama ili kwenda sambamba na ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo inataka wananchi wengi zaidi kuwa wanachama wa mifuko ya afya.
Alisema kuwa mfuko unaoweza kufanikisha ahadi hiyo ni CHF hivyo akasema ili wananchi waweze kuvutiwa na kujiunga nao kuna haja ya kuboresha huduma zake ili ziwe na wigo mpana zaidi kwa kumwezesha mwanachama kutibiwa katika kituo chochote ndani ya mkoa anaootoka.
“Yapo mafanikio makubwa ambayo tumeyaona baada ya CHF kuwa chini yetu lakini ni lazima tuboreshe baadhi ya maeneo kama huduma vijijini ili wananchi waweze kuvutiwa zaidi na kujiunga,” alisema Bw. Humba.
Akijibu hoja hizo, Dkt. Mponda alisema kuwa tatizo la huduma vijijini tayari wizara imeliona na hatua zimeanza kuchukuliwa ikiwemo Bohari ya Dawa (MSD) kuanza kusambaza dawa hadi kwenye vituo vya kutolea huduma.
Alisema kuwa awali ukosefu wa dawa ulikuwa ukichangia na mlolongo mrefu wa usambazaji na baadhi ya dawa ziliibwa zikiwa katika mchakato huo ambapo sasa jukumu hilo limeanza kufanywa na MSD kwa baadhi ya mikoa ili dawa zipelekwe moja kwa moja na ziweze kufika kwa wakati uliokusudiwa.
“Zipo sababu ambazo zinasababisha upungufu wa dawa lakini kubwa ni ufinyu wa bajeti hivyo ni lazima vyanzo vingine vya fedha katika halmashauri vitumike kwa ajili ya kununulia dawa ili kuboresha huduma za afya.
Suala la mfuko wa bei, Dkt. Mponda alisema wizara itaangalia ili kuona kama kuna haja ya kuwepo kwa chombo hicho ambacho kitaangalia mfumko wa bei za dawa ambazo kwa sasa zinasababishwa na mfumo wa soko huria.
Kwa upande wa wafanyakazi waliowakilishwa na Mwenyekiti wa TUGHE, Bw. Baraka Maduhu, waliiomba serikali kuhakikisha inalifanya suala la mifuko ya afya kuwa agenda ya kitaifa ili wananchi wahamasike kujiunga zaidi.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment